Mbwana Samatta, mshambuliaji wa Taifa Stars
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
Washambuliaji wa Taifa
Stars, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) wamewasili nchini jana usiku na kwenda
moja kwa moja kambini.
Ujio wa washambuliaji
hao unafanya idadi ya wachezaji walioripoti kambini kufikia 20 kati ya 23
walioitwaa baada ya mshambuliaji Khamis Mcha aliyekuwa na kikosi cha timu yake
ya Azam nchini Liberia naye kuripoti kambini leo asubuhi.
Wachezaji John Bocco na
makipa Mwadini Ally na Aishi Manula ambao pia nao walikuwa Liberia na timu yao
ya Azam wataripoti kambini leo alasiri. Wachezaji hao ni sehemu ya msafara wa
timu ya Azam ambao utakuja na ndege ya mchana kutokea Nairobi kwa vile ile ya
asubuhi waliyotangulia nayo wenzao kuwa imejaa.
Taifa Stars
inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ikiwa chini ya Kocha Kim Poulsen
leo inaendelea na mazoezi Uwanja wa Taifa. Mazoezi hayo yataanza saa 9 alasiri.
Wakati huo huo, kiingilio cha chini
katika mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Tanzania (Taifa Stars) na
Morocco (Lions of the Atlas) itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya kijani.
Viti vya kijani katika
uwanja huo wenye uwezo wa kumeza watazamaji 60,000 viko 19,648. Kwa upande wa
viti vya rangi ya bluu ambavyo viko 17,045 ni sh. 7,000. Kiingilio kwa viti vya
rangi ya chungwa ambavyo viko 11,897 ni sh. 10,000.
Viingilio vya daraja la
juu ni kama ifuatavyo; VIP C yenye watazamaji 4,060 ni sh. 15,000 wakati sh.
20,000 ni kwa VIP B yenye watazamaji 4,160. VIP A yenye watazamaji 748
kiingilio chake ni sh. 30,000.
Tiketi kwa ajili ya
mechi hiyo itakayoanza saa 9 kamili alasiri zitaanza kuuzwa siku mbili ya
mchezo (Ijumaa na Jumamosi) katika vituo vifuatavyo; Shule ya Sekondari
Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora,
Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni na Dar Live Mbagala.
Katika vituo hivyo
tiketi zitauzwa katika magari maalumu. Magari hayo pia yatafanya mauzo ya
tiketi uwanjani siku ya mechi.
Vilevile tunapenda kuwakumbusha watazamaji
kutonunua tiketi mikononi mwa watu au katika maeneo yasiyohusika ili kuepuka
kununua tiketi bandia, hivyo kukosa fursa ya kushuhudia mechi hiyo.
No comments:
Post a Comment