Rais wa TFF, Leodgar Tenga kulia akiwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho hilo, Sunday Kayuni.
SIWEZI KUVUMILIA
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
SASA nimeamini kuwa Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF),
Leodgar Tenga, hana washauri. Na kama anashauriwa, basi wanamdanganya katika
baadhi ya uamuzi unaoleta utata katika Shirikisho hilo.
Kwanini nasema hivyo? Kwa mtu makini, ambaye anajua fika kuwa
kila atakaloamua kwa maslahi ya Tanzania, basi kitachunguzwa kwa kupimwa na
wenye akili na wasiokuwa na akili pia.
Katika hilo, nilifikiri kuwa kila jambo linalofanywa sasa,
lazima lipimwe na kuwekwa sawa kwa ajili ya maslahi ya Taifa letu. Hakika
siwezi kuvumilia. Nimeshindwa baada ya kuona Tenga akiwadanganya Watanzania,
kuwa eti Shirikisho la Mpira wa Miguu duniani (FIFA), wametoa tishio la kuifungia Tanzania.
Sawa FIFA wanaweza kutufungia kwa sababu ya makosa yetu ya
kizembe yaliyofanywa au yanayoendelea kufanywa, hasa pale wanapokataa kuwa
masuala ya mpira wa miguu yasifanywe na serikali.
Hadi sasa, ni kama vile tunastahili kufungiwa. Amri na kanuni
za serikali kuwa mbali na maamuzi ya soka, imevunjwa hasa pale Waziri wa
Habari, Vijana, Uramduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara kuwaagiza TFF
watumie Katiba ya mwaka 2006 na kuiacha ile ya mwaka 2012.
Mbali na Katiba hiyo, kikao kilichofuata kati ya serikali na
TFF, pia waliamuliwa waitishe Mkutano Mkuu na kufanya Uchaguzi, baada ya ule
waliopanga kufanya awali, kuvunjwa kwa sababu za kupingana kikanuni.
Pamoja na hayo yote, lakini nimeshangazwa na jambo moja
kubwa. Hivi hawa FIFA, kwanini watangaze kuifungia Tanzania kwa kupitia
magazeti?
Hivi kweli chombo kama
FIFA kinachoaminika duniani, kinaweza kukaa na kujadili yalioandikwa kwenye
magazeti?
Wakati nawaza haya,
nakumbuka kuwa siku tatu kabla ya Tenga hajazungumza hayo, alikuwa kwenye
mkutano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), ambao huko alikutana pia na watendaji wa FIFA, sasa kwanini wasingempa
ujumbe huo hadi watume kwa barua.
Kiukweli kabisa, nina
hofu na utendaji wa TFF pamoja na malengo yao, hasa kwa kuamua kuwadanganya
Watanzania. Huu ni uongo wa aina yake.
Kwa mujibu wa TFF, eti ujumbe
huo umetumwa unaoleza kuwa itaifungia Tanzania kama serikali yake itakuwa
inaingilia mambo ya michezo, huku ujumbe huo ukitumwa na Jerome Valke, ambaye
ni Katibu Mkuu wa chombo hicho kikubwa duniani kwa sekta ya mpira wa miguu.
Sawa, lakini hapa wakubwa wamejaribu kukimbia kivuli. TFF
inapaswa kujua kuwa hata kama FIFA itaifungia nchi, lakini si jambo la busara
kujaribu kuifanya serikali yetu haina meno kwa yale inayokusudia kuyafanya.
Kila mtu anajua kuwa Watanzania hatuna maendeleo katika sekta
ya michezo, hivyo ili tufike tunapohitaji, hatuhitaji ubabaishaji wa aina
yoyote. Viongozi wanaofanya ‘madudu’ wasichekewe.
Ndio inauma, hasa kama
TFF itafungiwa na FIFA, lakini hata wao wanapaswa kuambiwa kuwa TFF ipo chini
ya serikali japo inajiendesha yenyewe bila kutegemea chochote kutoka
serikalini.
Na ndio maana tuna Waziri wa Michezo. Kama uamuzi wa serikali
hauwezi kuheshimiwa, basi sheria zetu zitakuwa na matege. Huo ndio ukweli wa
mambo na hapana shaka unapaswa kufuatwa.
Tenga na jopo lake anapaswa kujua kuwa alichokisema, kila mtu
anajua kuwa sio kweli, zaidi ya kukaa na watu wake kupanga la kuwadanganya watu
ili waone kuna umuhimu wa kuwafuata wanachosema.
Wakati mwingine nafika mbali zaidi kwa kuwaza; labda ni bora
tufungiwe ili tujipange, maana hata hapa hatujafungiwa hatuna maendeleo
kwasababu ya wachache wao kutokuwa na dhamira ya kweli.
Nayasema haya kwa uchungu, maana siwezi kuvumilia kuona kuwa
kumbe mtu anaweza kukaa na kujipangia mambo kwa faida yake. Hii sio njia nzuri
kwa ajili ya kukuza sekta ya michezo.
Ni wazi katika haya yanaoendelea sasa, mgogoro huu utaendelea
kushika kasi, maana wachache wao hawataki kufuata maagizo ya serikali kwa kufanya
vikao na marafiki zao, kasha wakaandika barua za kuwapiga mkwara serikali ili
kesho ionekene si lolote katika Taifa hili.
Hapana. Na katika hili, ni bora wadau na viongozi wa michezo
kuwaambia FIFA, kuwa kwenye masuala ya ndani watuachie wenyewe. Hata kama
wakiamua kutufungia, lakini itakuwa njia ya kujiandaa, kujiweka sawa katika
kipindi cha miaka ambayo watafungia.
Bila hivyo hatuwezi kufika pale tunapohitaji, maana wapo watu
wanaofanya mambo ama kwa bahati mbaya au wanafanya makusudi kwa faida wanayojua
wenyewe, jambo ambalo hatuwezi kukubaliana nalo.
Hakika katika hili, kamwe siwezi kuvumilia na iwe tiba kwa
wale wanaona kuwa Watanzania sasa ni majuha, eti hatujui lolote katika
ulimwengu huu.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment