Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Netiboli Tanzania, Rose Mkisi, amewataka wadau wa
michezo kujitokeza kwa wingi leo kuchukua fomu mbalimbali kwa ajili ya kugombea
katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Machi 24, mjini Dodoma.
Wakati Rose akiyasema hayo, leo saa tija alasiri ndio mwisho wa kuchukua
fomu za uchaguzi huo, huku nafasi ya uenyekiti ikiwa imeombwa na mtu mmoja tu,
ambaye ni Anna Kibira.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Rose alisema nafasi kama ya
mwenyekiti hadi jana jioni ilikuwa imeombwa na mtu mmoja tu, hivyo kuonyesha
kuwa vado kuna umuhimu wa wanamichezo kujitokeza katika nafasi mbalimbali.
Alisema kuwa wadau wamekuwa wazito kujitokeza katika kugombea nafasi hizo kwa
ajili ya kuhakikisha kuwa wanafanya kazi ya maana kuendeleza mchezo wa netiboli
hapa nchini.
“Naomba wadau na wanamichezo wajitokeze leo hadi kesho saa tija kwa ajili
ya kuomba nafasi za uongozi wa CHANETA kwa kuendeleza mazuri yaliyopatikana
katika kipindi kilichopita.
“Ingawa muda unaelekea mwishoni, lakini mtu anaweza kuchukua fomu hapo hapo
pamoja na kuirudisha, ukizingatia kuwa hadi sasa wamejitokeza watu 11 tu kwa
kuwania nafasi za uongozi CHANETA,” alisema Mkisi.
Uchaguzi huo umepangwa kufanyika mkoani Dodoma mwishoni mwa mwezi huu, huku
mwenyekiti anayemaliza muda wake, Anna Bayi, akidaiwa kuwa hatatetea tena
nafasi yake kwa nia ya kuwapisha wengine waongoze, hasa kama hadi leo jioni
hatajitokeza katika kuchukua fomu hizo.
No comments:
Post a Comment