SERIKALI imedhamiria kutenga sehemu ya Pori Tengefu la
Loliondo lenye ukubwa wa Kilomita za Mraba 1,500 kutoka kwenye sehemu ya
Kilomita za Mraba 4000 za pori hilo ili kutatua migogoro inayoendelea katika
hifadhi hiyo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi
Khamis Kagasheki, akizungumza na waandishi wa habari.Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki.
Waandishi wakimsikiliza Waziri Kagasheki jana.
Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi
Khamis Kagasheki, alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari juu ya eneo la
Loliondo linavyoendelea kutafunwa na migogoro kutokana na muingiliano wa
matumizi ya ardhi katika eneo lililotengwa na kutangazwa na serikali kuwa pori
tengefu la Loliondo.
Waziri Kagasheki alisema kwamba katika adhma hiyo
itakayochukuliwa bila kuingiza hisia zozote za kisiasa, wataokoa hadhi ya Pori
hilo na kulinda pia mazalia ya wanyama pori, mapitio na vyanzo vya maji kwa
ajili ya ustawi wa hifadhi na manufaa kwa Watanzania wote.
“Serikali itasimamia eneo litakalobaki kuwa Pori Tengefu kwa
mujibu wa Sheria za Uhifadhi wa Wanyamapori, huku ardhi itakayobaki baada ya
kuondoa eneo hilo likiachwa kwa wananchi, kijiji namba 5 ya mwaka 1999.
Wananchi watawezeshwa kuanzisha eneo la Jumuiya ya Hifadhi
za Wanyamapori (WMA), katika ardhi itakayobaki ya kijiji kwa mujibu wa sheria,
huku tukijua kuwa huo utakuwa mpango bora wa matumizi ya ardhi katika vijiji
vya eneo la Loliondo, yakiambatana na mifugo, ikienda sanjari na majosho,
malambo ya maji ya mifugo, minada na mengineyo,” alisema Kagasheki.
Aidha Kagasheki alisema kuwa muhimu ni wananchi hao kufuga
kisasa na kuzingatia ukubwa wa eneo lao (Carrying Capacity), ili isilete
madhara kwa kwa eneo husika.
Waziri alisema kuwa katika uamuzi wao huo, kamwe
hawataangalia wanasiasa wanataka nini, hasa wale wanaopita na kurubuni watu kwa
ajili ya kuendelea kukuza mgogoro huo kwa ajili ya kuhitaji kura au kulinda kwa
kujipendekeza kwa wapiga kura wao bila kufuata sheria za nchi.
Kwa mujibu wa Kagasheji, serikali itapitia na kuangalia ukubwa wa maeneo waliyopewa baadhi ya
wawekezaji, wakiwamo OBC na ikibidi kupunguzwa na kuwagawa kwa wananchi, huku
tukishirikiana kwa karibu na wenzetu, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi ili kuona uhalali wa Kampuni zinazomiliki ardhi katika eneo
linalohifadhiwa kwa madai kuwa wameuziwa na serikali za vijiji.
No comments:
Post a Comment