TIMU ya Polisi Morogoro, leo
itakuwa na kibarua kigumu mbele ya vinara wa ligi ya Tanzania Bara, Yanga SC,
pale zitakapovaana katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, katika mfululizo wa
mechi za Ligi hiyo inayodhaminiwa na Kampuni ya Vodacom Tanzania.
Wachezaji wa Yanga wakijifua
Yanga inaingia uwanjani huku
ikiwa kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa Bara kwa kujikusanyia jumla ya
pointi 48, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 40, wakati Simba yenyewe ina pointi
34.
Mbali na Yanga na Polisi
Morogoro, timu nyingine zinazoingia uwanjani leo ni pamoja na Simba watakaokuwa
wageni wa Toto African ya jijini Mwanza, wakati Azam wenyewe wataingia uwanjani
kucheza na Ruvu Shooting uwanja wa Chamaz, wakati Kagera Sugar watashuka uwanja
wa Kaitaba kucheza na Mtibwa Sugar ya mjini Morogoro.
Timu zote tayari zimeshafika
katika mikoa hiyo kwa ajili ya kuhakikisha kuwa wanatoka na ushindi, hali
inayosababisha ushindani wa aina yake katika patashika hiyo ya Tanzania Bara.
Yanga, wamedhamiria kuifanyia
umafia Polisi Morogoro kwa kuwatandika ili wajiweke kwenye naafsi ya kunyakua
ubingwa wa Bara unaoshikiliwa na Simba, ambao mpaka sasa wameuweka rehani
ubingwa huo.
Kocha wa Yanga, Ernest Brandit,
ametangaza hali ya hatari kwa wapinzani wao, akisema kuwa lazima wawatandike
wenyeji wao, Polisi Morogoro ili waunuse ubingwa na kuwapa shangwe mashabiki
wao.
Kwa upande wa Simba, kocha
msaidizi, Jamhuli Kihwelo Julio, alisema kuwa vijana wake wapo imara, ingawa
kumekuwa na propaganda zinazofanywa ili kuwaweka kwenye wakati mgumu.
“Watu wanataka tuendelee kufanya
vibaya kwa maslahi yao, lakini hakika vijana wapo imara na wana kila sababu ya
kushinda mbele ya Toto African.
“Tumewasili jijini Mwanza tukiwa
na ari kubwa, ingawa wapo waliozusha eti tumezuiwa kwa sababu wanazojua wenyewe
na fitina zao,” alisema Julio.
Simba wanaingia uwanjani huku
wakiwa na kumbukumbu ya kutoka Bukoba huku wakiwa wamefungwa bao 1-0 dhidi ya
Kagera Sugar.
Endapo Simba itafungwa na Toto
leo, basi si tu itajiondoa kwenye ubingwa zaidi, bali hata ile nafasi ya pili
itakuwa ngumu, kwa kuangalia mahesabu ya msimamo wa ligi, huku Yanga wao wakiwa
kileleni kwa tofauti ya pointi 8 dhidi ya Azam yenye 48, huku Simba wao wakiwa
na pointi 34.
Naye kocha wa Mtibwa Sugar, Mecky
Mexime, alisema kuwa wamefika mkoani Kagera wakiwa na matumaini ya kuibuka na
ushindi mbele ya Kagera Sugar, ingawa wanaamini mchezo utakuwa mgumu.
Kagera Sugar wenyewe wana pointi
34 sawa na Simba, wakati Coastal Union
na Mtibwa Sugar wamejikusanyia pointi 32 katika ligi ambayo imezidi kuwa
na msisimko hasa nafasi za juu na chini, hasa zile zilizokuwa kwenye hatari ya
kushuka daraja.
Mwisho
No comments:
Post a Comment