https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Thursday, March 21, 2013

Stars kuvuna nini Morocco ikitua nchini kwa nguvu kubwa kesho?


Kikosi cha Timu ya Taifa Morocco

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
TIMU ya Taifa ya Morocco (Lions of the Atlas), inatarajiwa kuwasili nchini kesho Ijumaa kwa ndege ya Emirates tayari kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Tanzania (Taifa Stars), itakayochezwa Jumapili katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Msafara wa timu hiyo yenye watu 58 wakiwemo maofisa 19 na waandishi wa habari 12 utawasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 8.55 mchana na utafikia hoteli ya Kilimanjaro Hyatt Regency.


Akizungumza na Handeni Kwetu, Msemaji wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Boniface Wambura, alisema kuwa siku hiyo Morocco siku ya kwanza ya kutua kwa timu hiyo, itafanya mazoezi jioni yake katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, na Jumamosi itafanya mazoezi yake ya mwisho kwenye Uwanja wa Taifa kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezwa saa 9 kamili alasiri.

“Wachezaji walioko kwenye kikosi hicho chini ya Kocha Rachid Taoussi, ni Nadir Lamyaghri, Anas Zniti, Yassine Bounou, Younnes Bellakhadar, Abdellatif Noussair, Abderrahim Achchakir, Zoheir Feddal, Younnes Hammal, Zakarya Bergdich na Abdeljalil Jbira.

“Wengine ni Issam El Adou, Kamel Chafni, Salaheddine Saidi, Mohamed Ali Bamaamar, Abdelaziz Barrada, Salaheddine Aqqal, Abdessamad El Moubarky, Nordin Amrabat, Chahir Belghazouani, Abdelilah Hafidi, Youssef Kaddioui, Brahim El Bahri, Hamza Abourazzouk na Youssef El Arabi,” Alisema Wambura.

Wakati huo huo, tiketi kwa ajili ya mechi hiyo zitaanza kuuzwa keshokutwa katika vituo vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Uwanja wa Taifa na Dar Live Mbagala, huku milango siku ya mechi kwa ajili ya watazamaji ikifunguliwa saa 6 kamili mchana.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...