Rais wa TFF, Leodgar Tenga
Na Mwandishi Wetu, Dar
es Salaam
Shirikisho la Kimataifa
la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA) limesema litaifungia Tanzania iwapo
itabainika kuwa Serikali imekuwa ikiingilia shughuli za Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF).
FIFA imesema kumekuwa na
shutuma kupitia taarifa mbalimbali za vyombo vya habari nchini kuwa Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imeonesha nia ya kuingilia uendeshaji wa
TFF.
Kwa mujibu wa barua ya
jana (Machi 10 mwaka huu) ya FIFA kwenda kwa Rais wa TFF, Leodegar Tenga,
vyombo vya habari vimemkariri Waziri (Dk. Fenella Mukangara) kuwa Serikali
imeiagiza TFF kutumia Katiba ya mwaka 2006 katika uchaguzi wakati tayari
imeshafanyiwa marekebisho.
“Pia imeelezwa kuwa TFF
imetakiwa kufanya Mkutano Mkuu pamoja na ule wa uchaguzi kwa tarehe ambazo
zimepangwa na Serikali. Vilevile imeelezwa kuwa Serikali inakusudia kuunda
Kamati ya Muda iwapo TFF haitatekeleza maagizo yake,” imesema sehemu ya barua
hiyo iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome Valke.
FIFA imesema iwapo
yaliyoripotiwa na vyombo vya habari yatathibitika kuwa kweli, maana yake huo ni
uingiliaji wa wazi wa Serikali kwa shughuli za TFF.
“Tunapenda kuwakumbusha
kuwa wanachama wote wa FIFA wanatakiwa kuendesha shughuli zao kwa uhuru bila
kuingiliwa na mtu mwingine kama ilivyoelezwa katika ibara za 13 na 17 za Katiba
ya FIFA.
“Hivyo kama maagizo hayo
yanayodaiwa kutolewa na Serikali yatatekelezwa, suala hili litapelekwa katika
mamlaka za juu za FIFA kwa hatua zaidi ikiwemo kuisimamisha Tanzania kama
ambavyo inakuwa pale panapokuwa na uingiliaji wa Serikali,” imesema barua hiyo.
Barua hiyo ambayo nakala
yake pia imetumwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) imeelezea baadhi ya
athari ambazo Tanzania itakumbana nazo endapo itasimamishwa ni timu za taifa
pamoja na klabu kutoshiriki mechi za kimataifa kwa mujibu wa Ibara ya 14 ya
Katiba ya FIFA.
Vilevile si TFF au
wanachama wake na maofisa wengine watakaoweza kunufaika na programu za
maendeleo, kozi au mafunzo yanayotolewa na FIFA na CAF.
“Madai ya uamuzi
uliofanywa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ni ya kusikitisha
kutokana na ukweli kuwa FIFA ilishatangaza itatuma ujumbe wake kuchunguza jinsi
hali ilivyo kwa sasa na kutoa mapendekezo yake. Kutokana na hali hii, ujumbe wa
FIFA uliokuwa uje kuchunguza (suala la uchaguzi) itabidi usubiri kwa vile ni
muhimu kushughulikia tatizo hili kwanza.
“Katika mazingira haya
tunaomba ueleze msimamo huu wa FIFA kwa mamlaka zinazohusika (Serikali) na
athari ambazo mpira wa miguu wa Tanzania utakumbana nazo. Tunakushuru na
tunatarajia utatufahamisha kila hatua inayoendelea katika suala hili,” imesema
barua hiyo.
No comments:
Post a Comment