Full Tank, mkali wa comedy Bongo
Full Tank: Soma makala yake hapo chini
Full Tank
EDWARD PETER CHAGULA ‘FULL TANK’
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KUNA vitu ambavyo binafsi huwa napenda kuviangalia, vikiwamo
hivi vya kuangalia komedy kutoka kwa wasanii mbalimbali wa Tanzania. Hata kama
nikiwa na mawazo vipi, hakika kazi hizo zinanifanya nijione mwenye furaha na
amani tele.
Katika kuangalia filamu hizo, ni wasanii wengi wanaovutia
akiwapo Edward Peter Chagula, maarufu kama Full Tank. Ni kibonge kweli. Ni
mkali pia katika sanaa, huku akimudu kuutumia mwili wake kwa uwezo wa juu
kupita kiasi.
Kwa wasiofahamu uwezo wa kijana huyu, waangalie komedy
nyingi, ikiwamo ile ya Kibonge Mtukutu, Miss Tandale, Choo cha Kulipia na
nyinginezo . Katika mazungumzo yaliyofanyika mapema wiki hii, Full Tank,
anasema kwamba sanaa ni kipaji chake.
Anasema tangu zamani alipenda kuigiza, hasa upande wa
vichekesho, ndio maana aliweza kupigania maendeleo kwa kupitia ndani ya jukwaa
hilo kwa ajili ya kuonyesha makali yake katika tasnia ya filamu hapa nchini.
"Nilikuwa napenda kuigiza tangu zamani, hivyo nadhani katika
njia ya kutafuta jinsi ya kutoka, nimefikia hatua hii nzuri, huku nikiamini
kuwa nitaendelea kuwa juu na imara kwenye maisha ya sanaa.
"Nafanya juhudi kubwa katika kuonyesha sanaa yangu ikiwamo ya
uchekeshaji, hivyo wadau wangu na wanaopenda kazi zangu naomba waendelee
kuniunga mkono katika maisha sana yangu,” alisema Full Tank.
Mkali huyo mwenye uwezo wa juu katika sanaa ya maigizo na
uchekeshaji anasema kuwa sanaa ni ngumu na yenye ushindani wa aina yake, lakini
anaamini kuwa changamoto hizo wasanii wanazitumia vyema kwa maisha yao.
Full Tank anasema kutokana na kufanikiwa kujitangaza katika
kipaji chake, wadau wengi, zikiwamo taasisi zimekuwa zikifanya naye katika kazi
katika sherehe mbalimbali za kiofisi ndani na nje ya jiji la Dar es Salaam,
ikiwamo mkoani Kilimanjaro.
Huko, msanii huyo kazi yake kubwa ni kuwachekesha kwa
kuelimisha jamii katika matukio ya wafanyakazi alipoalikwa, jambo ambalo
limezidi kumuweka katika nafasi nzuri katika tasnia ya filamu na uchekeshaji
Tanzania.
“Huwa najisikia faraja kuona kuwa ndani ya saa moja au
mawili naona kazi yangu kwenye luninga, yakiwamo matangazo ya kampuni
mbalimbali yanayorushwa kwa kasi muda wote.
“Hilo linanipa imani na hamu ya kuendelea kupiga hatua
katika kutafuta maisha yangu kwa kupitia sanaa, maana nimechagua kuwa msanii,
ingawa naelewa sanaa ni ngumu na idadi kubwa ya watu wanaingia kwa nia ya
kujikomboa,” alisema.
Full Tank anasema kwamba wasanii wote ni wazuri, ingawa kwa
kipaji cha Mzee Majuto, hakika ni sehemu ya kuwapatia mwangaza wakali wengine,
huku mzee huyo akiwa na ushirikiano na wasanii wengi, wakiwamo wale
wanaochipukia.
Full Tank aliyetokea kupendwa na kuhitajika na watu wengi
kutokana na umahiri wake wa kutumia mwili mkubwa, anasema kuwa yeye ni mtoto wa
kwanza kuzaliwa katika familia ya mzee Peter Chagula, huku akiwa na watoto
wawili, ambao ni Mathias mwenye miaka tisa na Veronica, akiwa na miaka sita.
Aidha msanii huyo anajiwa na kumbukumbu mbaya ya kuona
wazazi wake wameshindwa kuona vipaji vyake baada ya kutangulia mbele ya haki
miaka kadhaa iliyopita.
Full Tank anasema kuwa katika kuhakikisha kuwa mambo yake
yanakuwa mazuri zaidi, amepania kufanya kazi yenye maana kwa kutunga filamu
zake au kushirikishwa na wandaaji wengine wanaothamini vipaji vyake.
Kijana huyo mwenye mwili mkubwa anasema kuwa sanaa ni kipaji
chake alichozaliwa nacho, ingawa rasmi alianza mwaka 1995. Kundi lake la kwanza
kujiunga nalo lilikuwa la Mahokazi likiwa chini ya Bambo na kushiriki kwenye
filamu kadhaa.
Mbali na filamu hizo nyingi zikiwa za uchekeshaji, pia Full
Tank ameshiriki katika tamthilia ya Ndio Mzee iliyokuwa ikirushwa na
televisheni ya DTV mwaka 2002 ambapo nyota yake ilizidi kuonekana na
kujitabiria mafanikio makubwa.
Full Tank aliyezaliwa mwaka 1986 katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili, amecheza filamu kadhaa, ikiwamo ya Grammar, Pete ya Ajabu, Sangoma,
Sabra, Mpango uliokwenda Vibaya, Born Stone, Akili ni Nywele na nyingine zipo
njiani kutoka.
Mbali na kucheza filamu hizo, pia kijana huyo amefanikiwa
kutengeneza filamu zake za mtindo wa uchekeshaji ‘komedy’, ambazo ni Kibonge Mtukutu,
Miss Tandale, Choo cha Kulipia na nyinginezo zilizotangaza zaidi makali yake.
Mkali huyo anasema kuwa sanaa ni ngumu na inahitaji ujasiri
wa aina yake, hivyo wasanii wachanga wanatakiwa kuongeza bidii katika kutangaza
uwezo wao.
Anasema hakuna haja ya kurudi nyuma au kuogopeshwa na ugumu
uliopo, ukiwamo ule wa kusota katika makundi kwa miaka kadhaa kabla ya
kufanikiwa kutoka, wakati wote huo, wengineo wakiendelea kuishi maisha ya raha.
Kibonge huyo mtukutu anasema katika kuliweka juu zaidi jina
lake, lengo kubwa ni kufanya kazi zenye ujazo wa juu, ikiwa ni njia ya kumletea
mafanikio, ingawa atakuwa mwepesi wa kuiga nyendo zenye tija kutoka kwa wasanii
anaowakubali.
No comments:
Post a Comment