Kikosi cha Yanga SC
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MKUTANO Mkuu wa Dharura unaotarajiwa kufanyika Machi 17 mwaka huu katika
Hoteli ya Star Light, Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, umepangwa kuwa suluhu
ya kuiweka Simba imara katika muendelezo wa ligi ya Tanzania Bara, ikiwapo
mechi dhidi ya Yanga.
Mkutano huo umetangazwa tena jana jijini Dar es Salaam na Mratibu wa
wanachama zaidi ya 600, Mohamed Wande, akieleza kuwa wamefuata taratibu zote za
kisheria, likiwapo jeshi la Polisi wilayani Ilala, Ofisi za Utamaduni Ilala,
pamoja na msajili wa vyama vya michezo.
Akizungumza kuhusu maadalizi ya mkutano huo wa kesho, Wande alisema ni dhahiri klabu yao
ipo kwenye hali mbaya, kiasi cha kutishia huenda wakapata mvua ya mabao kutoka
kwa mtani wao wa jadi Yanga, kama hawatakutana haraka na kujadili mwenendo
mbaya wa timu yao.
Alisema kuwa ingawa mwanzo mkutano wao ulizuiwa hatua za mwisho kutokana na
hila za mwenyekiti wao, Ismail Aden Rage, lakini wanaamini wanachama wa Simba
wataendelea kuipigania klabu yao.
“Tumefuata hatua zote za kufanikisha mkutano huu muhimu wa Simba, huku
tukiamini kuwa utarudisha heshima za timu yetu, ikiwamo mechi yetu na Yanga,
itakayopigwa baadaye mwezi ujao.
“Sisi wanachama na wapenzi wa Simba, tunaona njia kuu ya kuiwezesha timu
kuwa pazuri kwa kufanya mkutano huu wa dharula ambao kwakweli tunaomba watu
wote waje bila kuchoka,” alisema.
Wande alisema kuwa katika mkutano huo hakutakuwa na vurugu zozote, huku
akiamini kila mwanachama anayestahili kuwapo atahudhuria kwenye mkutano wao wa
kuinusuru klabu ya Simba.
Mkutano wa Simba unafanyika huku wanachama wakiwa na kumbukumbu ya viongozi
wao wa juu, akiwapo Makamu Mwenyekiti Geoffrey Kaburu na Mwenyekiti wa Kamati
ya Usajili, Zacharia Hans Pope kuachia ngazi na kuundwa pia Kamati ya Ushindi,
ikiwa chini ya Malkia wa Nyuki, Rahma Al-Kharoos.
Kwa
upande Msemaji wa klabu ya Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema kuwa hawautambui
mkutano huo, maana umeitishwa na watu wasiokuwa na uwezo wa kufanya hivyo,
isipokuwa mwenyemkiti peke yake.
Alisema
hakuna mwanachama mwenye uwezo wa kuitisha mkutano, badala yake wangesuburi
mwenyekiti wao apone na kurudi Tanzania, ili ashughulikiea masuala ya mkutano
huo wa Simba.
“Nashauri
wanachama wa Simba wajiepushe na mkutano huo, maana tumetoa taarifa sehemu
husika, huku tukiamini kuwa hautafanyika kwasababu haujakidhi vigezo vyote.
“Hata
hivyo, Katiba ya Simba SC, Ibara ya 22, inatamka wazi kuwa wanachama
wasiopungua 500 wana uwezo wa kuitisha Mkutano wa Dharura, endapo
watajiorodhesha kwa Kamati ya Utendaji.
Kutokana
na orodha hiyo, wanachama zaidi ya 600 wamejitokeza na kusaini juu ya mkutano
huo, hali inayoupa uhalali kwa kiasi kikubwa, hasa katika kipindi hiki ambacho
mwenyekiti hayupo, Makamu mwenyekiti amejiuzulu.
No comments:
Post a Comment