Rais wa TFF, Leodgar Tenga, akiwa na Sunday Kayuni.
Na Mwandishi Wetu, Dar es
Salaam
Shirikisho la Soka nchini na Serikali kupitia Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo, wamekubaliana kuwa mchakato wa uchaguzi wa
Shirikisho hilo utaendelea kwa sharti la kuhakikisha haki inatendeka kwa
wagombea waliofika mbele ya Kamati ya Rufani ya Uchaguzi nchini.
Akizungumza na Waandishi
wa Habari leo mchana, Rais wa TFF, Leodegar Tenga amesema uamuzi huo umefikiwa
kwenye kikao kati ya uongozi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
chini ya Waziri Dk. Fenella Mukangara, TFF na Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Baada ya
maafikiano hayo, TFF italiandikia barua Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa
Miguu (FIFA) ambalo ndilo lililosimamisha mchakato huo ili litume ujumbe wake
kwa ajili ya kusikiliza malalamiko ya wagombea walioenguliwa.
Rais Tenga ambaye
ameishukuru Serikali kwa kuruhusu mchakato huo uendelee, pia ameahidi kuwa
uchaguzi wa TFF utafanyika kabla ya Mei 25 mwaka huu kama walivyokubaliana na
Serikali, na kuwa haki si tu itatendeka bali ionekane imetendeka.
“Serikali imetuelekeza
uchaguzi ufanyike kabla ya Mei 25, hivyo sisi tumewaambia huko ni mbali na FIFA
hata kama wakija kesho, wakituambia tuendelee tupo tayari.
“Hesabu zetu ziko
tayari, makabrasha yote yako tayari yanasubiri mkutano tu. Labda itakuwa kutoa
muda tu kwa wajumbe walioko mbali waweze kujiandaa, maana wajumbe huwezi
kuwaita ghafla,” amesema.
Amesisitiza kuwa TFF
ilishapanga tarehe ya uchaguzi, lakini ukasimamishwa na FIFA baada ya baadhi ya
walioenguliwa kulalamika huko. Hivyo maneno kuwa TFF hawataki uchaguzi kwa
sababu wanataka kuendelea kubaki madarakani haya maana hata kidogo.
Hivyo amewataka wagombea
wote waliofika kwenye Kamati ya Rufani ya Uchaguzi na wakaendelea kujiandaa
vizuri, kwani FIFA watakapofika watawasikiliza wao na vyombo vilivyowaengua.
Pia amesema TFF ina
heshimu Serikali na itaendelea kufanya hivyo, lakini vilevile lazima iheshimu
FIFA sababu iko kwenye mpira wa miguu, na FIFA ndiyo wasimamizi wa mchezo huo
duniani.
Amewakumbusha wanachama
wa TFF, hasa wajumbe wa Mkutano Mkuu kufahamu kuwa TFF ina katiba, lakini ni
lazima pia wafahamu kwanini kuna FIFA.
Rais Tenga
amewahadharisha watu wanaopitapita mikoani kuomba saini za wajumbe ili kuita
Mkutano Mkuu wa dharura wakati wanajua mkutano ulishaitishwa, lakini
ukasimamishwa na FIFA. Jambo hilo kikatiba ni kosa.
No comments:
Post a Comment