Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
RAIS wa Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amewataka viongozi wa vyama vya
mpira wa miguu vya mikoa kuhakikisha wanaingiza wachezaji wenye umri sahihi
katika michuano ya U15 FIFA Copa Coca-Cola 2013.
Rais wa TFF, Leodgar Tenga
Ametoa mwito huo leo
(Machi 26 mwaka huu) wakati akifungua semina elekezi ya michuano ya Copa
Coca-Cola ambayo kuanzia mwaka huu itakuwa ikishirikisha watoto wenye umri
chini ya miaka 15.
Rais Tenga amesema
hakuna jambo la kipuuzi kama kuchomekea wachezaji ambao wamezidi umri
unaotakiwa kwa vile lengo la michuano ya aina hiyo ni kubaini vipaji na
kuwafanya watoto wapende kucheza mpira wa miguu.
“Kwanza nawashukuru kwa
kutenga muda wenu na kuhudhuria semina. Lakini ni vizuri pia mkahakikisha
mnakuwepo kwenye mashindano ili kutekeleza haya ambayo tutakubaliana katika
semina hii. Mkileta mtu mwingine anaweza kutuanzishia mambo mengine badala ya
yale tutakayokubaliana,” amesema Tenga.
Pia ameishukuru kampuni
ya Coca-Cola ambaye imekuwa ikidhamini michuano hiyo tangu mwaka 2007 ambapo
semina hiyo elekezi inayoshirikisha makatibu wa vyama vya mpira wa miguu vya
mikoa na waratibu wa mikoa wa michezo ya UMISSETA ni ya saba mfululizo.
Ratiba ya michuano hiyo
kuanzia mwaka huu imebadilika ambapo sasa itaanzia ngazi ya wilaya Aprili
wakati fainali katika ngazi ya Taifa itachezwa Septemba.
No comments:
Post a Comment