Vida akiwa amesimama kwa kufotolewa picha....
Vida, akisisitiza jambo kwa Handeni Kwetu Blog.
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
UKIPATA nafasi ya kusikiliza wimbo wa 'Baba Awena', hakika
utasuuzika nyoyo yako kwa kiasi kikubwa mno, maana umeimbwa kwa hisia na
mtazamo wa aina yake katika ulimwengu wa nyimbo za mapenzi, hapa nchini.
Msanii Vida kutoka THT, akizungumza na mwandishi wa habari mwandamizi, Arodia Peter, wiki iliyopita.
Wimbo huo wa aina yake umeimbwa na mwanadada anayeibukia
katika taasisi yenye jina la kutisha, Tanzania House of Talent (THT), Pili
Juma, anayejulikana kwa jina la Vida.
Vida umeniona?
Ni wimbo mzuri na wenye ujumbe wa aina yake, huku akishirikiana na msanii mwingine wa THT, Linex, anayejulikana pia kwa kutunga nyimbo zenye mashairi ya hadithi za kusisimua.
Vida, akiwa kwenye pozi...
Pamoja na mambo mengine yanayoufanya wimbo huo kuwa juu
katika vituo vya redio, bali pia wimbo huo ni ishara kuwa nyota nyingine imeibukia
katika taasisi hiyo ya THT na kufuata nyayo za wakali wengine, kama vile
Mwasiti, Vumilia, Linah na Recho ambao wote wamefanikiwa kupata majina makubwa
kisanaa.
Ni hodari haswa, huku akiimba kwa kiwango cha juu pamoja na
umakini wake anapokuwa katika kazi hiyo ya sanaa. Katika mazungumzo
yaliyofanyika mapema wiki hii, Vida anasema kuwa anafanya juhudi kubwa pamoja
na kumuomba Mungu kazi zake zikubaliwe na mashabiki.
Anasema kuwa kutokea katika taasisi yenye mguso na majina ya
wasanii wengi wenye mipango kabambe ya kuwapatia mafanikio, kunamfanya aongeze
kasi na aina ya utendaji wake wa kazi chini ya jopo la wataalamu wa muziki
katika taasisi hiyo.
"Ukiona msanii hapa ndani ya THT anatoka, ujuwe ameshapikwa
na kuiva vizuri, ndio maana wengi hulazimika kusubiri kwanza utaratibu
uliowekwa kwa ajili ya kuhakikisha kuwa wasanii waliopo wanafikia malengo yao.
"Naamini katika hilo, ukweli utajulikana kuwa nahitaji
kufikia malengo kama wenzangu waliotangulia hapa THT, huku nikishukuru kwa
kiasi kikubwa jinsi ninavyolelewa na kutolewa tangu chini hadi hapa nilipokuwa
sasa,” alisema Vida.
Mwanadada huyo anasema kuwa sanaa ni kitu anachopenda katika
maisha yake, ndio maana hata wazazi wake
hawajaweza kumtilia kauzibe walipogundua kuwa anapenda kuwa msanii, huku akianzia
na sanaa ya uchezaji shoo.
Anasema alipokuwa na miaka 16 tangu kuzaliwa kwake, alianza
kujiwekea mikakati ya kuwika kisanaa kwa kuanzia na sanaa ya uchekeshaji.
Mwanadada huyo anasema kuwa aliamua kujipeleka THT kwa sababu ndio sehemu
maalum ya kukuza na kulea vipaji.
“Nilipokwenda THT, nashukuru nilipokelewa vyema kama mcheza
shoo, lakini sikudumu sana, maana wakati huo bado nilikuwa nasoma, hivyo
sikuweza kufanya kazi kwa moyo na muda zaidi, nilikuwa naenda na kuondoka.
“Hata hivyo, baada ya miaka mitatu, nilirudi tena na
kufanyiwa usaili ambapo nilipita moja kwa moja kama mwimbaji badala ya densa
kama nilivyokwenda mwanzo, maana wakati huo vipaji vyangu vilizidi kujionyesha
kwa kasi ya ajabu,” alisema Vida.
Msanii huyo anayevutiwa kwa kiasi kikubwa na muziki wa Ali
Kiba, anasema kuwa mpaka sasa ameshakamilisha nyimbo tano zinazoweza kuwapo
kwenye albamu yake ya kwanza itakayokamilika hibi karibuni, kadri ya mashabiki
watakavyoendelea kumpokea.
Nyimbo hizo ni pamoja na Malingo, Nahisi, Umenikumbuka, Rafiki
na Baba Awena ambao umezidi kufanya vyema katika vituo vya redio; huku makali
yake yakizidi kuimarika kwa kiasi kikubwa katika tasnia ya muziki wa kizazi
kipya, maarufu kama Bongo Fleva.
Vida anasema kuwa matarajio yake ni kuwa msanii mkubwa kwa
kuhakikisha kuwa anafuata ushauri wa wadau wake, wakiwamo wataalamu wa muziki
waliokuwapo katika taasisi ya THT yenye kutoa wasanii bora na wenye makali ya
kutisha.
Wasanii ambao wanafanya vyema na wametokea katika taasisi
hiyo ni pamoja na Linah, Mwasiti, Barnabas, Mataruma, Dito, Kwea Pipa, Amini, Recho
pamoja na makundi zaidi ya matatu ambayo nayo yapo ndani ya taasisi hiyo.
Msanii huyo anasema kuwa wasanii wote waliokuwapo katika
taasisi hiyo ni wakali na wanaweza kufanya vyema zaidi katika muziki wa kizazi
kipya. Kilichopo hapo ni utaratibu na namna inavyowekwa mipango ya kuwatoa kwa
mpango.
“Naomba kuwataka wadau na mashabiki wangu wakae mkao wa
kula, maana nimejipanga kwa kiasi kikubwa kuona kuwa mwaka huu nakuwa imara na
mwenye mafanikio makubwa zaidi, nikiwa chini ya taasisi ya THT.
“Naamini kwa kushirikiana kwa pamoja na wasanii wenzangu,
malengo yatatimia, ukizingatia kwamba najifunza kwa kupitia wenzangu
waliotangulia, huku nikiomba dua njema kwa wazazi wangu, ukizingatia kuwa tangu
zamani walinipa moyo,” alisema Vida.
Mwanadada huyo
anasema kuwa mbali na kuwa na kipaji cha uimbaji na uchezaji, lakini pia
anahusudu mambo ya urembo, hasa katika tasnia ya uanamitindo, ikiwa ni kazi
ambayo ina nafasi katika maisha yake leo au siku za usoni.
Vida ni mzaliwa wa mkoani Morogoro, katika wilaya Kirombelo,
huku sanaa yake ikionekana kama amerithi kwa mama yake, ambaye naye anafanya
sanaa ya maigizo, akicheza filamu kadhaa, ikiwamo ile ya Pigo.
Kwa sasa msanii huyo anaishi Mbagala, huku akiwa na imani
kuwa Mungu ataendelea kumuongoza na kumbariki uwezo wa juu katika maisha ya
sanaa duniani.
Mwanadada huyo anasema kuwa serikali inatakiwa kufanyia kazi
changamoto zinazoyumbisha maisha ya wasanii, maana wote wanategemea sanaa kama
sehemu za ajira zao, hivyo ukimya huo unaweza kuwa sumu kwa nguvu kazi ya
Taifa.
Msanii huyo alizaliwa mwaka 1994, huku elimu yake ya msingi
akiipata katika shule ya Annex iliyopo Mbagala, jijini Dar es Salaam alipoanza
mwaka 2002 na kumaliza mwaka 2008.
Kutokana na matatizo ya kiafya yaliyodumu kwa muda mrefu,
mwanadada huyo alilazimika kukomea elimu ya kidato cha pili, huku akiwa na
mikakati ya kuendelea na shule mara baada ya kuweka mambp yake sawa.
Vida mwimbaji wa Baba Awena, anamaliza kwa kuwataka wasanii
waendelee kuongeza bidii katika maisha yao, ikiwa ni njia ya kutangaza muziki
na sanaa kwa ujumla, ingawa kumekuwa na changamoto za aina yake kwenye tasnia
hiyo.
No comments:
Post a Comment