Na Mwandishi Wetu, Dar
es Salaam
SHIRIKISHO la Kimataifa
la Mpira wa Miguu (FIFA) ambalo lilisimamisha mchakato wa uchaguzi wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutokana na baadhi ya wagombea
kulalamika kuenguliwa sasa litatuma ujumbe wake nchini katikati ya mwezi ujao.
Msemaji wa TFF, Boniface Wambura
Ujumbe huo ambao moja ya
shughuli zake kuwasikiliza wote walioenguliwa na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi
ya TFF na hawakuridhika na uamuzi huo, utakuwepo nchini Aprili 16 na 17 mwaka
huu.
Kwa mujibu wa barua ya
Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome Valcke kwenda kwa Rais wa TFF, Leodegar Tenga, kazi
ya ujumbe huo ni kubaini tatizo lililopo na kutoa ripoti kwa mamlaka
zinazohusika ndani ya FIFA kwa ajili ya kutoa mwongozo.
Ujumbe huo utakutana na
pande mbalimbali zinazohusika wakiwemo wagombea, kamati za uchaguzi za TFF. Lakini
pia ujumbe huo unatarajia kumtembelea Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo, Dk. Fenella Mukangara pamoja na watendaji wake wizarani.
Uchaguzi wa viongozi wa
TFF ulikuwa ufanyike Februari 24 mwaka huu, lakini ukasimamishwa na FIFA baada
ya baadhi ya wagombea walioenguliwa kulalamika kuwa hawakutendewa haki na
wangependa shirikisho hilo liingilie kati.
No comments:
Post a Comment