Rais wa TFF, Leodgar Tenga
Na Mwandishi Wetu, Dar
es Salaam
RAIS wa Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amemshukuru Waziri wa Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenela Mukangara kwa kukubali ombi la
Shirikisho la kutaka kukutana naye kwa mazungumzo na kumsihi asitishe hatua
anazodhamiria kuchukua hadi hapo kikao hicho kitakapofanyika.
Waziri Mukangara
ameiagiza TFF kuitisha Mkutano Mkuu wa marekebisho ya katiba ifikapo tarehe 15
Aprili 2013 na Mkutano Mkuu wa Uchaguzi ifikapo tarehe 25 Mei 2013 na kwamba
tamko la TFF kutekeleza maagizo hayo liwe limetolewa katika muda wa siku tano
zinazoishia Jumatatu (Machi 11, 2013).
Katika barua pepe ambayo
amemuandikia Waziri ambaye kwa sasa yuko nje ya nchi, Rais Tenga ameeleza kuwa
alikwenda ofisini kwake tarehe 7 Machi 2013 kujaribu kumuona lakini akaambiwa
amesafiri, hivyo kuomba kukutana na Katibu Mkuu wa Wizara, ambaye pia hakuwepo
ofisini na hatimaye akakutana na Naibu Katibu Mkuu.
Katika barua hiyo pepe,
Rais Tenga ameeleza madhumuni ya kutaka kuonana na Waziri Mukangara kuwa ni
kwanza “kukushukuru kwa kukubali kuonana na ujumbe wa TFF ulioongozwa na mjumbe
wetu wa Kamati ya Utendaji, Bw. Alex Mgongolwa, akiongozana na Katibu Mkuu wa
TFF, Bw. Angetile Osiah, jana tarehe 6 Machi 2013.
“Kukushukuru kwa
kukubali kukutana nasi tena siku ya tarehe 19 Machi, kwa ajili ya mazungumzo
juu ya maagizo yako.
“Kukuarifu kuwa
nimepokea maagizo yako uliyoyatoa jana kupitia kwa Mjumbe wetu wa Kamati ya
Utendaji na kwa njia ya barua; na
“Kwa heshima na taadhima, kukuomba usitishe hatua yoyote ile unayodhamiria kuchukua hadi hapo tutakapokutana na kupata maelezo yetu, TFF, juu ya maamuzi na maagizo uliyoyatoa.”
“Kwa heshima na taadhima, kukuomba usitishe hatua yoyote ile unayodhamiria kuchukua hadi hapo tutakapokutana na kupata maelezo yetu, TFF, juu ya maamuzi na maagizo uliyoyatoa.”
Tenga, ambaye ni mjumbe
wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika (CAF) aliondoka
jana (Machi 7 mwaka huu) kwenda Marrakech, Morocco kuhudhuria kikao cha kamati
hiyo na pia Mkutano Mkuu wa CAF ambao umepangwa kufanyika Machi 10 mwaka huu
ukihusisha pia ajenda ya uchaguzi wa rais.
No comments:
Post a Comment