SIWEZI KUVUMILIA
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WACHAMBUZI wa soka waliowengi
wanasema hakuna maendeleo ya mpira wa miguu bila kuzitaja klabu za Simba na
Yanga. Sawa, kutokana na ukongwe wao, hilo haliepukiki.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage
Wao Simba na Yanga lazima
watajwe, ingawa mara kadhaa wamekuwa wakitajwa kwa mabaya na sio mazuri.
Kwasababu hiyo, huwezi kutaja mafanikio ya soka kwa miaka ya hivi karibuni, eti
ukaitaja Simba na Yanga na kuiacha Azam FC.
Kwanini? Umetumia vigezo gani? Hata
hivyo, katika kuwaza yote hayo, najikuta nikiangalia nyendo za viongozi wa
klabu hizi za Simba na Yanga, na kuona kuna dalili kubwa za mmoja wao kusonga
mbele na kumuacha mwenzake akibaki kama alivyo.
Kwanini nasema hivyo?
Ukiangalia nyendo za viongozi wa Simba, utagundua kuwa wamekuwa wakipiga porojo
na kukosa mbinu nzuri za kuendeleza klabu yao.
Simba ikiwa chini ya Ismail
Aden Rage, imekuwa ikiandamwa na malalamiko ya wanachama wao, kiasi cha
kutangaza mkutano wao na kufikia kusimamisha uongozi huo.
Uamuzi huo ni baada ya Makamu
Mwenyekiti wa Simba, Geoffrey Nyange Kaburu na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili
ya Simba, Zacharia Hans Pope kujiuzulu nafasi zao.
Hata hivyo, mkutano wa
wanachama uliofanyika katika Hoteli ya Star Light Kariakoo, ulitangaza kuwaingiza
katika uongozi huo Pope na Rahma Al Khgarous, jambo ambalo uongozi wa Simba
umepinga na kudai kuwa mkutano wao ulikuwa ni kama kikao cha harusi.
Sawa, huenda ni kweli wanachama
hao wamefanya kikao cha harusi, lakini huu ni mwendo mzuri kwa ajili ya Simba?
Binafsi naona kama vile Simba imezidi sana porojo kuliko vitendo.
Ukiangalia wenzao Yanga,
wamekuwa na mipango mingi yenye tija katika siku za usoni. Juhudi zao
zinaonekana, lakini sio hawa wanaojiita Wekundu wa Msimbazi.
Kuna hatari kuwa miaka mitatu
ijayo, Yanga wao watakuwa wamefanya mambo makubwa, wakati wenzao Simba
wanaendelea kutukana na kuitana vikao vya harusi kama anavyodai mwenyekiti wao.
Hakika siwezi kuvumilia.
Mwenyekiti wa Yanga, Yusuph Manji, alitangaza kumuingiza katika Kamati ya Maendeleo
ya Mafia, mtoto wa rais, Ridhiwani Kikwete kwa ajili ya kuhakikisha kuwa Yanga
inakuwa na jingo kubwa la kibiashara.
Hakika uwezekano huo upo.
Wakijipanga na kuweka mtaji huo wenye dhamira ya aina yake, mambo mengi mazuri
yatapatikana kwa namna moja ya kuiweka Yanga sehemu nzuri.
Haya lazima yasemwe na kupingwa
kila yanapoonekana kuwa baadhi yao hawataki na wanaendelea kufanya mambo ya
kushangaza. Simba hii inataka kuwa mtani wa jadi kwa mechi tu au hata mipango
ya kimaendeleo kwa klabu yao?
Simba hii ambayo haina uhakika
wa kutetea taji lao, hivi kweli ina walau mpango wa kumiliki uwanja wao wa
michezo? Ukisema hivi wenye Simba yao watakwambia ndio. Kisa, Rage aliahidi.
Rage aliahidi siku 90 za mafanikio ya Simba, je, bado hazijafika?
Rage huyu amekuwa hana jipya
katika uongozi wake, hivyo kuna hatari kuwa kama mambo yakiendelea hivi, basi
Simba itakuwa mtazamaji mkubwa wa masuala ya maendeleo ya Yanga.
Hii itakuwa aibu ya karne. Na
ndio maana nimeshindwa kuvumilia, nikiamini kuwa viongozi wa Simba sasa
watashtuka na kufanya kazi kwa ajili ya maendeleo ya klabu yao.
Huu ndio ukweli. Vingine,
nitaendelea kuwa karibu na wanachama maana ndio wenye klabu yao, maana uongozi
wao hauna mpango mzuri zaidi ya kutaka kuipoteza klabu yao.
Namaliza kwa kuwapongeza Yanga
na kuwatakia mipango mema kwa ajili ya maendeleo ya soka na klabu yenu kwa
ujumla.
Tukutane wiki ijayo.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment