Diamond, mkali wa Bongo Fleva Tanzania
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WIZI wa kazi za wasanii waelimishwe kwanza wanunuaji kabla
ya wauzaji, maana ndio wenye kutoa pesa zao kwa kununua CD feki.
Bila hao kutoa pesa zao, hakika hao wauzaji hawawezi
kuendeleza kufanya madudu yao. Unapozungumzia wizi huo, upo kwa aina zaidi ya
mbili.
Wapo wale ambao wana mitaji mikubwa, kiasi cha kutoa CD feki
zinazoelekea kufanana na urijino. Hata hivyo haitoshi, wapo wale wanaotoa CD
feki kabisa, zikikosa alama yoyote ile.
Wafanyabiashara hao, ni wale wanaomiliki kompyuta, wachoma
CD zao kama njugu na kuwauzia wateja wao, ikiwa ni njia mbaya mno katika sanaa.
Nasema hivyo, huku nikijua kwamba wapo watu ambao katika
kutafuta namna ya wizi huo, wanajidanganya kwamba wizi huo upo kwa
wafanyabiashara wakubwa, wale wenye maduka.
Lakini sivyo. Wezi wabaya zaidi ni wale wa mitaani.
Wanaendeleza wizi huo hadharani kabisa. Wanafikia hadi kutangaza machoni mwa
watu.
Utaona, ‘Tunakodisha CD hapa’. Tangazo la aina hii ni sumu
kwa sanaa na wasanii kwa ujumla. CD moja wanayonunua orijino, hakika inaweza
kutoa zaidi ya CD 50 na kuzikodisha kwa watu.
CD moja ya kukodi inalipiwa Sh 500 kwa siku moja. Hivyo, kwa
haraka haraka, muuzaji huyo anaingiza Sh 50,000 kwa siku, wakati msanii wake
ameingiza kiasi cha Sh 5000 itakayogawanywa na msambazaji wake.
Huo ndio wizi unavyoendelea. Kabla ya kuingia kwa
wafanyabiashara hao wakubwa, ipo haja pia ya kuingia mtaani na kuwakomesha.
Biashara yoyote ile, haiwezi kufanikiwa, endapo inakosa
mnunuzi. Sidhani kama kuna gazeti linaloweza kuendelea kuwapo mtaani, kama
halinunuliwi.
Hivyo hata hao wauzaji wa CD feki, hawawezi kuendeleza wizi
wao, kama Watanzania wataelimika juu ya kuwakataa kwa vitendo wauzaji hao.
Najua ninachokiema. Siku hizi kila baada ya nyumba kumi
katikati ya jiji, hakika yapo mabanda zaidi ya mawili yakifanya biashara hizo
haramu.
Tuyaseme haya bila kuoneana haya. Nasema hivyo, maana
Serikali yetu ipo kimya, ikisubiria kuzungumza kila baada ya Bunge la Bajeti.
Hao ni wabunge wetu, ambao wapo bungeni kwa sababu ya siasa.
Na siasa siku zote maneno yanakuwa mengi, huku vitendo vikiwa vichache.
Tujiulize kelele za bajeti ya mwaka jana, mangapi
yametekelezwa? Kama hakuna, wabunge hao mwaka huu watarudia kusema waliyosema
mwaka jaja.
Inauma sana, maana jeshi la polisi lipo lakini halitumiwi
kwa vitendo juu ya kuwakamata wale wanaofanya kila wawezalo kutengeneza maisha
yao.
Huo ni wizi na utakiwa ukomeshwe kwa vitendo na sio kupiga
porojo zisizokuwa na mpango, zikiendelezwa sana na wabunge wetu.
Samahani kama nitakuuzi kama wewe ni miongoni mwa mbunge,
ambaye umekuwa ukisema yale yale kila unapopewa nafasi, wakati yote
hayatekelezwi kwa wakati.
Huo ndio ukweli wa mambo. Mitaa yote sasa inauza CD feki,
inakodisha CD feki, wakinemeeka na ndugu zao wakiishi maisha magumu.
Nadhani tuingie kwenye mapambamo rasmi sasa ya kudhibiti
wezi hao, wakiwamo wale wa mitaani ambao ndio sumu kabisa.
Sitaki kuwatetea hao mchwa wakubwa, lakini hata hawa wadogo
ndio baadaye huwa wakubwa, kwakuwa wanatumia elfu tano na kuingiza nyingi
zaidi.
Tuwe makini katika hilo. Sanaa ni kazi, lakini hainufaishi
wasanii na watengenezaji wao. Ndio maana wengi wao wananunua vigari vya bei
chee, kwa kupitia kazi nyingine, baada ya kupata majina kwenye sanaa.
Huo ndio ukweli wa mambo. Tuanze kupanga mbinu nzuri, za
kuwakamata, ama kutaifisha biashara zao kwa kila aina, kama mchango madhubuti
wa kuwasaidia wasanii wetu Tanzania.
Vinginevyo wanasiasa wasiutumie wizi huo kama mtaji wao kwa
kuzungumza yale yale wanapokuwa kwenye vikao vya Bunge, maana wanaoumia ni
ndugu zao na wao wana sababu ya kufanikisha hilo.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment