Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage
SIKU zote ni aghalabu sana mtu
anayetangwa maji kwenye kinu akapata faida, kama anavyokusudia, zaidi ya hapo;
ataambulia kulowana kwenye kifua chake kwa kazi anayoifanya.
Kwa mtindo huu, kuna wajibu wa
kuwazindua wale wenzetu wanaofanya vitendo hivyo kujiangalia upya, maana daima
kazi hiyo haina malipo, isipokuwa kujisumbua.
Ndivyo ninavyoweza kusema
katika makala haya ya Siwezi Kuvumilia, kwa kuona kuwa wapo wadau wasiokuwa na
malengo sahihi ya kuokoa michezo, ukiwamo mpira wa miguu.
Huu ndio ukweli, maana wengi
wao wanaangalia faida yao katika sekta husika. Mtu yupo tayari kukanyaga baadhi
ya kanuni kwa ajili ya kujiweka katika nafasi ya mafanikio yake.
Angalia, licha ya kuwa na
wataalamu wengi kwenye Shirikisho la Soka nchini (TFF), lakini ligi yetu ni
mbaya haina mvuto. Hayo yanasababishwa na mbinu zetu kuegemea sana kwenye
kipato cha wachache kuliko wengi.
Dunia nzima wanaelewa kuwa
mpira wa miguu kazi inayolipa fedha nyingi, hivyo kama sisi Watanzania mipango
yetu si endelevu, ni waganga njaa, hakika matamshi yetu ni kama kutwanga maji
kwenye kinu.
Huo ndio ukweli wa mambo.
Utakuta watu licha ya kujigamba kuwa wana uchungu na michezo hasa mpira wa
miguu, lakini ameshindwa kabisa kuwa malengo ya kuendeleza vijana.
Mtu anao mtaji kabisa wa
kumuwezesha kufanya hivyo, lakini amefumba macho na kushuhudia nguvu kazi,
vipaji vingi vikikimbilia kulima, kukata mkaa na kugombana na maliasili kila
siku, hali ya kuwa wangekuwa matajiri wakubwa kama wangesimamiwa kwenye
michezo.
Matatizo kama hayo yapo vijijini.
Siwezi Kuvumilia imekuwa ikipokea simu nyingi kutoka kwa vijana wadogo, kila
mmoja akionyesha shauku ya kutaka kuonyesha uwezo wake, lakini wadau wenyewe
wamefumba macho.
Nimekuwa nikilizungumzia hili
kila siku kuwa, hata wabunge wetu, wanaweza kuendeleza vijana kwa kuwaanzishia
mashindano japo ya mwaka mara mbili, kama njia ya kuwapatia mwanga wapiga kura
wao.
Jimbo moja likiwa na msisimko
kwenye michezo, ina maana vijana wanajiweka katika nafasi nzuri, ukizingatia
kuwa tayari wana nafasi ya kuonyesa cheche zao, hivyo hili haliwezi kufumbiwa
macho.
Hakika siwezi kuvumilia, hasa
kwa kuona bado sisi ni watu wa kupiga porojo, kuhubiri siasa, kwa namna moja
ama nyingine, hali ya kuwa vijana wetu, wanaashia kuwa mashabiki.
Mapema wiki iliyopita
nilizungumza na Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Boniface
Wambura, ambapo yeye katika malalamiko yake, yaliegemea kwa wachezaji kuwa
licha ya kuwa na vipaji lakini hawajitambui.
Haya ni maneno kutoka kwa
Wambura, ingawa binafsi naona vipaji vingi vipo vijijini vinazagaa kwenye
vibanda vya pombe kali, maana hata hiyo nafasi ya kuonyesha vipaji vyao hawana.
Ndio hapo TFF inapotakiwa
kusimama kidete kuwakumbusha vyama vya wilaya, kuanzisha ligi zenye mashiko au
mashindano yenye mguso kwa ajili ya kuendeleza vipaji vya vijana.
Kinyume cha hapo, juhudi zetu
ni kazi bure. Hatutaweza kuwa na wachezaji wenye nguvu na mtazamo wa
kimaendeleo, ukizingatia kuwa ligi zetu, hazina mvuto na tunahubiri uzandiki.
Naamini tukifanya hivyo, hakika
mbinu zetu zitakuwa na mashiko, huku tukiwa na wachezaji wazuri na wenye mvuto
wa kusaka nafasi ya kushiriki ligi zenye nguvu duniani kwa kusajiliwa huko.
Kinyume cha hapo, Tanzania
haitakuwa na mbinu za kujiletea mafanikio Kimataifa, maana kila mtu ni
mwanasiasa na hakuna mtendaji kwa kuangalia mfumo mzima ulioozeshwa na viongozi
mbalimbali, wakiwamo wa TFF, ambao suala la Uchaguzi tu linawayumbisha kwa
kufanya fitina za kuwabana au kuwabeba wachache wao.
Hakika siwezi kuvumilia, maana
tunatwanga maji kwenye kinu.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment