Mlinda mlango wa Simba, Juma Kaseja.
Na Kambi Mbwana, Dar es
Salaam
MABINGWA watetezi, Simba
SC, leo wana kibarua kigumu cha kuhakikisha kuwa wanatoka na ushindi wa pointi
tatu muhimu katika mechi yao itakayopigwa katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es
Salaam, dhidi ya timu ya Coastal Union, kutoka Tanga kwa Wagosi wa Kaya.
Mechi hiyo inasubiriwa
kwa hamu na mashabiki wa soka wa Tanzania, huku upande wa Yanga na Azam FC,
wakiombea Simba iendelee kupoteza mechi hiyo ili ipotee katika mbio za kuwania
ubingwa huo.
Simba wanaingia uwanjani
kumenyana na Coastal Union, huku zote zikiwa na pointi 31, sawa na timu ya
Mtibwa Sugar ya Turiani mjini Morogoro, hivyo ina kila sababu ya kushinda ili
ijiweke kwenye nafasi nzuri ya kuendelea kuwa na matumaini ya kutetea ubingwa
wake.
Timu yoyote itakayoibuka
na ushindi leo, itafikisha pointi 34 na kushika nafasi ya tatu, jambo
linaloongeza ushindani katika mchezo huo ambao kila moja inataka ishinde na
kuwafurahisha mashabiki wake.
Hata hivyo, licha ya
timu hizo kudaiwa kuwa na undugu japo kwa kiasi kidogo, lakini zote zimepania
kushinda, huku joto kwa upande wa Simba likiwa juu zaidi kutokana na matokeo ya
migogoro inayoendelea kuwatafuna.
Juzi jioni, Malkia wa
Nyuki, aliyepewa nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati ya Ushindi, Rahma Al Kharoos,
alitembelea katika tawi la Mpira Pesa, akihitaji ushirikiano na kuvunja makundi
ndani ya Simba kwa ajili ya kuiwezesha kushinda katika kila mchezo unaokuja
mbele yao.
Hata hivyo, ujio wa
mwanamama huyo unakuja huku Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geoffrey Kaburu kuachia
ngazi, ikiwa ni uamuzi uliochukuliwa pia na Mjumbe wake Zacharia Hans Pope.
Kocha Mkuu wa Simba,
Patrick Liewing, yeye ana kila sababu ya kuona timu yake inaibuka na ushindi,
ili kulinda kibarua chake, ukizingatia kuwa baadhi ya watu wameanza kuhoji
uhalali wa kibarua chake ndani ya Simba.
Mechi hiyo ambayo kwa
upande wa Coastal inafundishwa na kocha wake, Ahmed Morocco, itachezeshwa na Martin
Saanya akisaidiwa na Jesse Erasmo na Vicent Mlabu wote kutoka mkoani Morogoro.
Timu zote zimepania
vilivyo kuibua na ushindi katika mchezo huo, akiwamo kocha msaidizi wa Simba,
Jamhuri Kihwelo Julio na bosi wake, Liewing, waliyetangaza hatari kwa Coastal
Union, ambayo nayo imejigamba kuwachachafya Wekundu hao wa Msimbazi, mechi
itakayokuwa na msisimko wa aina yake katika uwanja huo wa Taifa.
Endapo Simba itashindwa
kuifunga Coastal Union leo, basi huenda migogoro ikazidi kushika hatamu katika
klabu hiyo ambayo kila mtu ameanza kuiangalia kwa jicho la umakini mno, huku
baadhi ya viongozi wake wakiona kuwa wanastahili kukaa kando kwa kushindwa
kuiongoza timu yao katika nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wao.
No comments:
Post a Comment