LEO Jumapili, Wakristo wote Tanzania wanaungana wenzao
duniani kote kuadhimisha Sikukuu ya Pasaka, ikiwa ni kufufuka kwa Yesu Kristo.
Siku ya leo ni muhimu kwa Wakristo wote, huku ikianzia tangu
juzi Ijumaa Kuu, hivyo ni wakati wa waumini wote na wale wasiokuwa waumini wa
dini hiyo kuadhimisha kwa Amani na upendo.
Mara kadhaa, wapo baadhi ya watu ambao hutumia siku za
Sikukuu
kufanya uhalifu, hivyo jeshi la Polisi linapaswa kuwa makini katika
siku hizi kwa ajili ya kuhakikisha watu wanaishi kwa amani katika Taifa lao.
Tunajua kuwa wapo watu ambao siku kama hizi hutumia kwa
kutembelea mahala popote, hasa kwenye kumbi za starehe, lakini kwasababu hayo
ni maamuzi yao, muhimu ni wao kuona wanakuwa walinzi wa amani kwa kila mmoja
wao.
Itakuwa ni picha mbaya kama kila mmoja atakuwa akifanya
fujo, kama vile kumwaga vileo au kuendesha magari wakiwa wamelewa, jambo ambalo
pia si la kiungwana.
Mitaa mingi ya jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine ya
mijini, wapo madereva ambao hupita wakiwa kwenye mwendo wa kasi pamoja na kutia
mbwembwe, kuendesha magari yao bila kufuata sheria za usalama barabarani, jambo
ambalo hakika husababisha ajali na kuzua balaa kubwa.
Hatupo tayari kuona watu wanaofanya vitendo hivyo wanazidi
kupewa nafasi, hivyo ulinzi kila mmoja wetu anapaswa kuulinda kwa namna moja
ama nyingine.
Amani ndio silaha kwa kila mmoja wetu. Hata zile pombe za
kupitiliza, zinapaswa kuangaliwa, maana ndio chanzo cha mitafaruku katika maeneo
mengi.
Tunajua hatuwezi kuwakataza watu hao, ukizingatia kuwa
wanatumia gharama zao wenyewe, lakini si vibaya tukiwashauri hasa kwa kuwa
watulivu, kutumia kwa ustarabu, pamoja na kurudi makwao kistaraabu pia.
Kwenye fukwe za Bahari ya Hindi na maeneo mengine
yanayoshirikisha watu wengi kwa wakati mmoja, pia wazazi wanatakiwa wadumishe
ulinzi kwa watoto wao.
Kuna watu ambao huenda kwenye fukwe na watoto wao, lakini
hushindwa kuwalinda kiasi cha kuwaachia wakienda na maji na kusababisha mauti
kwao.
Tunaamini haya tukiyafanyia kazi, Sikukuu zote, ikiwapo hii
ya Pasaka inayofanyika kesho Jumapili na nyinginezo zote zitakuja kwa amani na
kuondoka kwa amani pia.
Tunamaliza kwa kuwatakia tena watu wote afya njema katika
Sikukuu hii ya Pasaka. Mungu Ibariki Tanzania
No comments:
Post a Comment