https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Saturday, March 23, 2013

Kagasheki ataka mapambano ya vitendo ya ujangili nchini



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, amewataka wafanyakazi wa Wizara yake kutumia mkutano wa 20 wa Baraza la Wanyakazi uliyoanza jana jijini Dar es Salaam kufikiria mbinu  na mikakati ya kupambana na majangili kwa vitendo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Khamis Kagasheki, akizungumza jambo huku akisikilizwa na Naibu wake, Lazaro Nyalandu kulia na Katibu Mkuu wake, Maimuna Tarshi.

Mkutano huo ulifunguliwa rasmi jana na Kagasheki pamoja na Naibu Waziri, Lazaro Nyalandu, huku Mwenyekiti wa Baraza hilo akiwa ni Katibu Mkuu wake, Maimuna Tarshi na kuhudhuriwa na wawakilishi wa mikoa mbalimbali.


Akizungumza katika uzinduzi huo, Kagasheki alisema kuwa mbinu ya kupambana na majangili katika sehemu zote za Wizara yake zinastahili kuongezwa mara dufu.

Alisema bila kufanya hivyo, mafedhuli hao wataendelea kutamba na kutishia uchumi wa Taifa kutokana na kufanya kazi hiyo ya ujangili kwa maslahi yao kwa kuvuna mali kutoka katika hifadhi mbalimbali za Taifa.

“Nawaomba wafanyakazi wote wa Wizara ya Maliasili na Utalii mkiwapo nyie ambaye mnashiriki katika Mkutano huu wa 20 wa Baraza lenu kuhakikisha kuwa mnatafuta mbinu mpya za kupambana na majangili.

“Hizi ni miongoni mwa changamoto ambazo kila mmoja wetu anastahili kuzijua na kuziamulia kisawa sawa kwa ajili ya kulimaliza tatizo la ujangili nchini,” alisema Kagasheki.

Katika hatua nyingine, Kagasheki aliwahakikishia wafanyakazi hao kuwa serikali yao itafanya kila iwezekanalo kuboresha vitu vinavyowapa makali ya maisha katika maeneo yao ya kazi, zikiwamo nyumba chache zilizokuwapo, licha ya kuwa na wafanyakazi wengi.

Awali wakati anafungua mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Maimuna Tarshi, alisema kuwa lengo la Mkutano huo ni kujadili changamoto mbalimbali wanazokutana nazo kwa ajili ya kuhakikisha kuwa serikali inapiga hatua katika seta zote, ikiwamo hiyo ya Maliasili na Utalii.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...