Mwanamuziki mkongwe wa muziki wa dansi wa bendi ya Msondo
Ngoma, Mzee Muhidin Gurumo, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uamuzi
wake wa kustaafu rasmi kazi ya muziki aliyoifanya kwa muda wa miaka 53 sasa.
Gurumo alitoa kauli hiyo leo katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo jijini
Dar es Salaam. Picha na Magreth Kinabo.
Na Jennifer Chamila, Maelezo.
MWANAMUZIKI mkongwe wa bendi ya Msondo Ngoma Mzee Muhidin
Gurumo amestaafu rasmi kazi ya muzika alioifanya kwa muda wa miaka 53.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo
Mzee Gurumo mwenye umri wa miaka 73
amesema ameamua kustaafu kazi hiyo kwa hiari yake mwenyewe kutokana na umri
wake kuwa mkubwa.
“Muziki kwangu umekuwa kama asili yangu na kazi yangu lakini
nimeamua kustaafu kutokana na umri wangu na nitabaki kuwa mshauri tu kwa
mwanamuziki yeyote atakayetaka ushauri wangu,”alisema Mzee Gurumo.
Pamoja na kufanya kazi ya muziki Gurumo alisema kuwa
hakupata mafanikio makubwa zaidi ya kujenga nyumba anayoishi na familia yake.
“Mimi nimeimba kwa muda mrefu sana lakini hata
baiskeli sina,”alisema Mzee Ngurumo. Hata hivyo alisema nashukuru kuwa ana nyumba ya kuishi na
familia.
Vilevile Mzee Gurumo amewaasa vijana kuwa wabunifu na
kuupenda mziki wa zamani kwani ndio chimbuko la bongofleva na kuwashauri
wanamuziki wa sasa kuwa wavumilivu kukaa muda mrefu kwenye bendi moja ili hata
wanapoondoka mchango wao uthaminiwe.
Mzee Gurumo
ambaye ana mke na watoto wanne alisema kuwa katika maisha yake ya muziki
alifanikiwa kutunga nyimbo 60,000 na anavutiwa zaidi na mwanamziki Hussein
Jumbe na Hassani Lehan Bichuka na kwa wanamuziki wa kizazi kipya anavutiwa na
Nassibu Abdul ’Diamond’.
Mwanamuziki huyo mkongwe alianza kufahamika katika tasnia ya
muziki wa dansi kwenye miaka ya 1960 ambapo mwaka 1964 alikuwa miongoni mwa
waanzilishi wa bendi ya Nuta Jazz na Mlimani Park.
Alidumu na Mlimani Park mpaka mwaka 1985 na kuhamia Safari
Sound aliyofanya nayo kazi mpaka mwaka 1990 na kujiunga na Msondo Ngoma mpaka
sasa alipoamua kutangaza rasmi kustaafu kazi hiyo ya Kimuziki.
No comments:
Post a Comment