Na Kambi Mbwana, Dar
es Salaam
BINADAMU anazidi
kuandamwa na mabalaa mengi, yakiwamo mabaduliko ya tabia nchi yanayosababishwa
na uchafuzi wa mazingira sehemu mbalimbali duniani.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete
Uzalishaji viwandani
na ukataji wa miti usiozingatia utamaduni wa kutunza mazingira yanasababisha
mkanganyiko mkubwa duniani.
Kama hivyo ndivyo,
walau sasa kunahitaji maandalizi ya kutosha. Kinyume na hapo, Tanzania kama
moja ya nchi zinazoathiriwa na suala hilo, itajiweka katika mazingira magumu.
Jamii ya Tanzania na
Serikali kwa ujumla inahitaji kuliangalia hilo kwa mapana, ikiwa ni pamoja na
kutunza mazingira ili iwe chanzo cha watu kuishi katika Dunia salama.
Bila kuzingatia hilo,
hata wakulima wetu wa Tanzania hawawezi kuishi maisha bora ukizimngatia kuwa
mazao yao mengi yanashindwa kustawi kutokana na ukosefu wa mvua au kunyesha
bila mpango.
Tanzania inaamini
kuwa uchimi wake ili ukuwe kunahitajika juhudi za wakulima wetu waliosambaa
kwenye mikoa mbalimbali.
Je, Watanzania
wangapi wanamasika katika kujishughulisha na kilimo? Je, ni vijana wangapi
wanajiingiza kwenye sekta hiyo iliyopewa jina la uti wa mgongo?
Hayo yanasababisha
watu wengi kuona hawawezi kuishi bila kufanya kazi za kuajiriwa, ikiwa ni
tofauti na uzalishaji mali kwa kupitia sekta ya kilimo yenye changamoto
mbalimbali.
Wanafanya hivyo bila
kujua kuwa sekta ya kilimo ndio inayoweza kutoa nafasi nyingi za ajira, tofauti
na fikra za waliokuwa wengi.
Mbali na kujiongezea
kipato kwa kujiingiza kwenye kilimo, pia tunaweza kujiweka kando na baa la njaa
kwa kuhakikisha kwamba tunakuwa na akiba ya kutosha, tofauti na sasa kila
wakati kusikia habari mbaya zinazohusu njaa kwa vijiji na wilaya mbalimbali za
Tanzania.
Njaa barani Afrika ni
tatizo kubwa. Ndio maana Nchi nane tajiri duniani, maarufu kama G-8,
zimekuwa zikifanya mikutano ya kila wakati kujadili namna ya kupambana na hilo.
Katika mikutano hiyo,
nchi ya Tanzania ni miongoni mwa zile zinazojadiliwa mara kwa mara kwa ajili ya
kupewa misaada, ambapo hata hivyo sio jambo geni kutokana na viongozi wake
kuona hilo ni jambo la maana kwao.
Pamoja na misaada
hiyo inayotolewa mara kwa mara kutoka kwenye mashirika ya Kimataifa au
serikali, ila ni vipi tunaweza kufanya kazi hiyo kwa unafanisi kwa ajili ya
kuboresha maisha yetu?
Hii ni kwasababu
baadhi ya viongozi wengi wa Tanzania ni wasemaji wasiozingatia vitendo katika
harakati zao. Tunaishi kwa ahadi. Tutafanya hivi na kufanya lile, ila hakuna
kitu. Ndio maana hata kwenye kujikita katika suala la kilimo bado hatuna jipya.
Mipango yetu mingi
inaishia kwenye makaratasi. Kwa miaka 51 ya uhuru, kumekuwa na mipango mingi
ingawa yote haina matunda. Hadi leo, bado hatuwezi hata kujiendesha wenyewe.
Serikali pia
inashindwa kuwaongoza wakulima kama inavyotakiwa sambamba na kuwapatia pembejeo
za kilimo, kuwa karibu nao kila wakati, hasa wakati wa majanga ya wadudu
kushambulia mazao yao.
Suala hili ni kati ya
changamoto nyingi zinazoongeza joto la ugumu wa maisha, maana wote wanakosa akiba
ya chakula cha kujikimu wao na familia zao sambamba na kuuzwa nje.
Mwaka 2008, Serikali
na wafanyabishara waliweza kukaa na kuliangalia hilo suala la kilimo. Lakini
mpango wa kuendeleza kilimo, naweza kusema kwamba haukufanikiwa kwa vitendo.
Kitendo cha kukaa
pamoja, ni kuonyesha kwamba wanatambua changamoto za kilimo, lakini ajabu ni
maoni yao yanavyoishia kwenye karatasi.
Hii ni mbaya na ndio
sababu ya nchi inakwenda ndivyo sivyo na hakuna mipango ya kuinusuru zaidi ya
kusubiria hisani kutoka kwa wengine. Nchi sasa inaendeshwa kwa hisani ya watu
fulani.
Tumekubali kuwa watu
wa misaada kutoka kwa wanaojiweza. Tukiliangalia hili, kila mtu ataelekeza
lawama zake kwa serikali, ambayo kwa bahati mbaya ipo chini ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM).
Hapo tutasema na
kujikuta kuamini kumbe tatizo ni serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Jakaya
Kikwete. Hawa wameshindwa kabisa kutuletea maisha bora kwa kila Mtanzania. Na
wameshindwa walau kuwasimamia na kuwaendeleza wakulima ili kazi zao zikuze
uchumi wa Taifa lao. Nao wanufaike ili waone kazi hiyo ni nzuri.
Wameshindwa hata
kusimamia sera ya kilimo kwanza walioasisi kwa mbwembwe nyingi. Pamoja na yote
hayo, je Watanzania nao wamekubali kukaa na kusubiria ahadi za serikali?
Watu wa aina hiyo
wapo wengi katika jamii. Wanalalama sana. Hata hivyo, wale ambao pamoja na
kukabiriwa na changamoto za aina hiyo lakini wanajihusisha na kilimo hoja
wanayo.
Ni wakati wa kukaa
chini na kuamua sasa tufanye kazi za kweli kwa ajili ya kuinua uchumi wa Taifa
letu, ikiwamo changamoto zinazowasumbua wakulima wetu ziweze kufanyiwa kazi.
Kama serikali
inashindwa kuwakopesha wakulima walau kiasi kidogo cha pesa, tunawezaje
kuwaongezea morali wa kufanya kazi?
Hii vita ya tatu ya
Dunia ambayo ni maji na chakula, hakika kwa sisi Watanzania, upo uwezekano wa
kutuangamiza.
Maana wenyewe hatuna
na mipango wala uelewa wa kujiingiza kwenye kilimo. Katika sekta hiyo kuna
matatizo mengi mno.
Zipo sehemu zilizokumbwa
na migogoro mikubwa ya wakulima wakubwa na wadogo. Hilo linapaswa kuangaliwa
upya kwa ajili ya kuhakikisha tunainua uchumi wetu.
Bila hivyo vita ya
umasikini ama maisha bora kwa kila Mtanzania ni ndoto. Hatuwezi kusonga mbele
kama hatuna mipango endelevu ya utendaji kazi kwa vitendo na sio porojo na
hadithi.
Tufanye kazi kwa
nguvu zote ili tuweze kukwamua uchumi wetu kwa kupitia sera ya kilimo. Kilimo
kinachoweza kufanywa na kila mmoja wetu na sio kukaa na kusubiri hisani ya
Wamarekani kama tulivyozea.
Hapa sina lengo la
kulaumu upande wowote, maana mambo hayo licha ya kushamiri sana, ila hayajaweza
kutusaidia. Malalamiko ya wapinzani bado sio suluhu la kuwapatia maisha bora
kwa Mtanzania kama wote hatuna uthubutu katika utendaji wa kazi.
Tunahitaji moyo wa
uzalendo, ushirikiano kwa ujumla, maana ndio mbeleko ya kutuweka katika nafasi
nzuri na kuacha kasumba zisizokuwa na mpango wowote ule.
Huo ndio ukweli wa
mambo. Kuna mengi yametufanya tushindwe kusonga mbele, ikiwa ni pamoja na kutojua
makosa yetu, hasa kuachia sekta muhimu kama kilimo kuendeshwa kienyeji.
Suala kama hilo
tusipokuwa makini nalo basi hakuna tutakachoweza zaidi ya kusubiria hisani ya
Wazungu. Na bado tujiandae kusubiria chakula kutoka kwao, wakati Tanzania ina
ardhi kubwa yenye rutuba.
Hakuna tutakachopata
zaidi ya aibu, maana licha ya kuzunguukwa na mapori kila mahali, kama vile
Tanga, Rukwa, Morogoro, Mbeya, Iringa na mikoa mingine ila hatuwezi kuitumia
ipasavyo.
Suala la kilimo
linahitaji mkazo na watu wote bila kuangalia nafasi zao kwenye jamii ili tija
kwao.
Kila Mkuu wa Wilaya
na Mkuu wa Mkoa, lazima ahakikishe kwamba katika eneo lake, wananchi wake
wanatembelewa na kusaidiwa katika kazi zao za kilimo.
Pale wakulima
wanapovamiwa na wadudu hatarishi, Serikali iwasaidie kwa kuwanunulia dawa,
pembejeo za kilimo na sio kuwaangalia tu, maana huo sio mtindo utakaonusuru
sekta ya kilimo.
Tukiweza kufanya
hivyo, sio tu tutakuwa na akiba ya chakula, bali pia tunaweza kuingiza fedha za
kigeni kwa kuuza nje na kukuza uchumi wa Taifa letu.
kambimbwana@yahoo.com
+255 712053949
+255 712053949
No comments:
Post a Comment