Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MCHEZAJI wa zamani wa Simba, Shomari Kapombe, amepata ulaji
baada ya klabu yake ya Simba, kumuunganisha katika klabu ya AS Cannes ya nchini
Ufaransa kwa makubaliano kuwa atakapouzwa Wekundu hao wa Msimbazi wapate mgao
wao.
Shomari Kapombe mbele, akiwa kwenye heka heka za timu ya Taifa, Taifa Stars
Hayo yamebainika kwa kupitia Mwenyekiti wao Ismail Aden
Rage, ambapo Simba imekubali mchezaji huyo achezee timu hiyo ya Ligi Daraja la
nne nchini humo kwa makubaliano ya makubaliano ya kumtafutia timu ya kucheza
ndani ya miaka miwili.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa
Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema kuwa timu hiyo itamgharimia Kapombe kwa kila
kitu wakati atakapokuwa nchini Ufaransa, ikiwa ni sambamba na kutafuta timu ya
kuchezea soka la kulipwa.
Alisema endapo Kapombe atauzwa kwenda katika timu nyingine
yoyote, Simba itapata gawio lake kupitia mauzo hayo na lengo la mchezaji huyo
kubaki Ufaransa ni kumtengeneza ili awe kwenye kiwango bora zaidi.
“Katika makubaliano hayo, Simba haitapata chochote kwa sasa,
isipokuwa pale atakapopata timu nyingine ya kuchezea, utaratibu ambao umekuwa
nuru kubwa kwake sanjari na kumuwekea mazingira mazuri ya kukuza soka lake.
“Naamini mambo yatakwenda sawa kwa kuhakikisha kuwa Kapombe
anafika mbali katika mpira wa miguu duniani, ambapo makocha wa Ulaya wamebaini kuwa
Kapombe ni mchezaji mzuri anayehitaji kuboreshewa kwa baadhi ya vitu ili aje
kuwa nyota duniani,” alisema.
Wakala wa Kapombe, Denis Kadito, alisema ingawa Kapombe
ameonekana kuwa mchezaji mzuri, kutofahamika kwa jina la Tanzania kumekuwa
kikwazo kikubwa kwa kupata kwake nafasi ya moja kwa moja na ndiyo maana imebidi
aanzie kwenye hatua ya chini.
Kutokana na mkataba huo wa Kapombe na Cannes, Simba sasa
imeongeza mkataba wake na mchezaji huyo kwa muda wa miaka mitatu zaidi, kwa
vile mkataba wake wa sasa unamalizika Aprili mwakani, huku akirejea katika
klabu yake endapo hatapata timu ndani ya miaka miwili.
No comments:
Post a Comment