Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
HATIMAE filimbi ya hujuma, pilikapilika, mnyukano ndani ya
Ofisi ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) imepulizwa, baada ya Kamati ya
Uchaguzi kutangaza mchakato na siku ya Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho hilo.
Mdau wa mpira, Michael Wambura
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Hamidu Mbwezeleni,
aliwatangazia Watanzania uchaguzi huo sasa utafanyika Oktoba 20 mwaka huu.
Kwa kauli yake hiyo, ni wazi kuwa sasa wadau wa michezo
hususan mpira wa miguu wameingia kwenye mihemko ya uchaguzi huo.
Ni wazi wajiandaye kwa lolote kutoka TFF. TFF ambayo imekuwa
ikisababisha malalamiko ya aina yake, ndio maana hata Uchaguzi huo ulishindwa
kufanyika kwa wakati.
Nikiwa kama mdau wa michezo hususan mpira wa miguu, ni wazi
nina hamu ya kuona uchaguzi huo ukifanyika kwa wakati bila kuleta mzozo wa aina
yoyote.
Kamati hiyo isijaribu kuweka hila za aina yoyote, huku
ikiwaacha wale wanaopenda kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kutumia haki
zao za msingi.
Uchaguzi huu ambao ulivunjwa baada ya kuibuka kwa
mkanganyiko wa aina yake, uliichafua pia soka la Tanzania, hasa pale
tulipolazimika kuwaita wageni waje kutuamulia mambo yetu ya ndani.
Hii siwezi kuvumilia hata kidogo. Ni wakati sasa wa kuwa
wakali juu ya wale watakaoendelea kuturudisha nyuma kila wakati kwa faida
wanazojua wenyewe.
Sura mpya za uongozi za TFF zitaonekana katika siku hiyo ya
Uchaguzi, ambapo tutashuhudia pia Rais anayemaliza muda wake, Leodgar Tenga,
akielekea mwishoni.
Kwa wale wanaofuatilia soka, watakubaliana na mimi kuwa
heshima ya Tenga ya zamani ilitoweka kama barafu juani, hasa kutokana na
kushindwa kuwasimamia vyema watendaji wake au Kamati za TFF.
Mara kwa mara tulishuhudia majibizano na kutoelewana kwa
kiasi kikubwa, hivyo wadau wa soka kushangaa umuhimu wake ndani ya Shirikisho
hilo.
Wahenga wamesema yaliyopita si ndwele. Hebu tugange yajayo
kuona kuwa Shirikisho hilo linapata viongozi wake kama inavyotarajiwa na wengi.
Hatuhitaji tena malumbano yasiyokuwa na msingi, maana ndio
kitu kitakachotuangamiza katika soka la Kimataifa. Watanzania licha ya kuwa na
vipaji vya aina yake, lakini tunashindwa kuwika nje ya mipaka yetu.
Wakati hayo tukiendelea kujipa moyo, tunagundua kuwa nchi za
Kenya na Uganda zimetuacha mbali mno. Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars)
inapata kazi kubwa inapokutana na timu za Harambee Stars na Uganda The ‘Cranes’,
timu ilizokuwa inajipigia mara kwa mara.
Kama hivyo ndivyo, kwanini tusibaini mapungufu yetu? Kwanini
tusiweze kushikwa na usongo kiasi cha kufanya bidii ili soka letu lisonge
mbele?
Tunaweza kufanya hivyo na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa,
lakini kama hakutakuwa na njia za panya wala malumbano juu ya uchaguzi huo wa
TFF.
Uchaguzi ndio kila kitu kwa soka la Tanzania. Tunahitaji
viongozi wanaopatikana kwa haki na sio wale wanaobebwa au wale wanaokandamizwa
kila wakati.
Sheria zifuatwe katika kuelekea kwenye Uchaguzi huo unaovuta
hisia za watu wengi. Inapofikia wakati huo, mambo mengi yamekuwa yakiwaka moto,
hasa kwa nafasi za Urais na Makamu wa Rais wa Shirikisho hilo.
Kuchangamkia fursa hiyo kwenye uchaguzi huo wa TFF, ni wazi
wamebaini fursa na mafanikio katia nafasi hizo, ila lazima kiu yao hiyo ilete
mabadiliko katika mpira wa miguu.
Kama tusipokuwa makini katika hilo, ni wazi hatutakuwa na
mafanikio katika sekta ya mpira wa miguu, maana kwenye msingi wa kwanza ambao
ni uongozi tulishindwa kuwa makini na kuweka mipango ya kimaendeleo.
Katika hili kamwe siwezi kuvumilia, hasa pale nitakapobaini
watu wachache wanaendelea kufanya mambo yanayoweza kuangamiza soka la Tanzania
badala ya kuingia watu wa mpira, wenye kujua mbinu za kupiga hatua Kimataifa.
Tukutane wiki ijayo.
+255 712053949
No comments:
Post a Comment