https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Monday, August 12, 2013

SIWEZI KUVUMILIA: Na bado, msusie na Uwanja wa Azam, Chamazi



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WADAU wa michezo hususan wa mpira wa miguu, wapo kwenye mshike mshike wa kusikiliza malalamiko kutoka kwa Yanga, hali inayowafanya wagomee mechi zao kuonyeshwa kwenye televisheni mpya ya Azam, itakayoanza hivi karibuni.
Rais wa TFF, Leodgar Tenga, pichani
Yanga kama timu kongwe hapa nchini, ikiwa chini ya mwenyekiti wake Yusuf Manji, imetangaza kugomea kuonyeshwa kwa mechi zao zote, wakisema sheria hazijafuatwa.

Wanafika mbali zaidi kwa kusema kuwa hakujatangazwa tenda ya kuifanya Azam tv ishinde kuonyesha mechi hizo za ligi kuu. Wengine wanasema kuonyesha mechi hizo kwenye luninga ni kupunguza mapato.

Eti watu hawataingia kwasababu wengi wao wataangalia kwenye luninga hiyo ya Azam. Kampuni ambayo licha ya kukusudia kuonyesha ligi hiyo, pia inamiliki timu ya Azam.

Inawezekana Yanga wapo sawa kwenye kusudio hilo la kugomea mechi zao kurushwa hewani, ila watagomea vingapi kutoka Azam? Ndio kwanza shughuli inaanza.

Ni kama vile moto wanavyojaribu kuuzima kwa petrol. Yanga watafanikiwa kweli kuzima cheche za Azam? Hii Yanga wanajidanganya. Na ndio maana Siwezi Kuvumilia.

Yanga wanajaribu kuweka hoja ya mechi kuonyeshwa na Azam tv ambayo nao wanamiliki timu kwenye ligi hiyo hiyo. Kweli? Kwa mtindo huo kamwe vilabu hivi vikongwe haviwezi kupunguza makali ya timu ya Azam, sanjari na Kampuni yao yenye mipango.

Udhamini wa Azam TV una manufaa makubwa kwa soka la Tanzania. Hii ni kwasababu klabu zote zinazoshiriki ligi Kuu sasa zitaambulia chochote kitu, hivyo kujimudu kiuchumi.

Timu ya Coastal Union ya Tanga kwa Wagosi wa Kaya, walau sasa wataweza kupata pesa tofauti na kusubiri mfuko wa wadhamini wakuu, yani Vodacom Tanzania.

Walau wadau sasa wanaweza kupunguziwa majukumu kutokana  na udhamini huo wa Azam TV, ambao kwa bahati mbaya timu ya Yanga inaona si mahali pake.

Na ndio maana ili kujisafisha, uongozi wa Yanga inapeleka suala hilo kwa wanachama wao katika Mkutano Mkuu wa Dharula, ili kuujadili udhamini huo wa Azam TV.

Ukiacha kusudio la kuonyesha mechi hizo kwenye luninga ya Azam tv, pia kampuni hiyo ya Said Salim Bakheressa imekuwa ikijihusisha na mambo mengi ya kimichezo.

Inamiliki Uwanja wa kisasa maeneo ya Mbagala Chamazi, ambao timu zote zinaweza kuutumia uwnaja huo. Jiji la Dar es Salaam leo lina uwanja mzuri unaomilikiwa na klabu.

Ni tofauti kubwa na mtazamo uliopo kwa wadau wengine wa michezo, wakiwamo wa Simba na Yanga. Timu kongwe zisizokuwa na kitu chochote cha kujivunia.

Kazi yao kubwa ni kupiga soga kwenye vibao vya kahawa. Hakuna mipango mizuri na wale wanaotaka kuofanya wanaingiza fitina mara kwa mara. Sasa wakongwe hawa watasusia vingapi?

Mashindano ya vijana yanadhaminiwa na Azam. Wao wenyewe wanajua Shirikisho la Soka nchini (TFF), limekosa mipango ya kuanzisha mashindano yenye mguso, yakiwamo ya vijana.

Timu zote za vijana zinashiriki. Yanga, Simba, Mtibwa Sugar, Coastal Union na zote zinazoshiriki Ligi ya Tanzania Bara, vijana wao wanashiriki katika mashindano hayo.

Kwanini wasianzie kukataa huko? Bado Azam inaendeleza juhudi za kuendeleza michezo, ndio maana timu yao imekuwa na mipango kabambe, hivyo hakuna haja ya kuwapunguza kasi.

Sisi tunaamini wapo wengine wenye uwezo wa kuonyesha mechi hizo, lakini leo waachwe Azam kwanza. Mkataba wao ukiisha wengine wataingia, wakiweka dau kubwa zaidi yao.

Huo ndio ukweli wa mambo. Na ndio maana siwezi Kuvumilia. Angalia, licha ya Kampuni hiyo ya Azam Media kumwaga Milioni 25 kwa kila timu, ukiacha Yanga waliogomea, bado hawajakamilisha mipango yao ya kurusha hizo mechi zinazopigiwa kelele.

Timu zisizokuwa na mtaji mkubwa, zimeambulia chochote kitu kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya Ligi ya Vodacom itakayoanza Agosti 24 mwaka huu kwa timu 14 kuwania taji hilo.

Timu hizo kila mmoja itavuna Shilingi Milioni 100 kutoka Azam tv kwa ajili ya mechi zake kurushwa kwenye luninga. Nani akatae dau kubwa kiasi hicho? Timu ya Ashanti United na Rhino zinaweza kweli kuingiza fedha hizo kwa mechi zao?

Kwa mtindo huo, ligi ijayo itakuwa na ushindani wa aina yake, maana timu zinajimudu kwa kiasi fulani, ukiacha Simba na Yanga wanaolingia mtaji wa mashabiki na kutawala soka miaka nenda rudi.

Ndio maana nasema wadau hao watasusia vingapi? Hii Siwezi Kuvumilia.
0712 053949

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...