Tuesday, August 13, 2013
Extra Bongo kutambulisha wapya Mamaz & Papaz Kigamboni
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WAKALI wa muziki wa dansi nchini Extra Bongo 'Next Level Wazee wa Kizigo' keshokutwa Alhamisi wanatarajiwa kuwatambulisha wanenguaji wake wapya wawili iliyowatwaa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo (DRC) katika onyesho maalumu litakalofanyika katika Ukumbi wa Mamaz & Papaz Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Msemaji wa bendi hiyo, Juma Kasesa, alisema, kuchukuliwa kwa wananguaji hao ni sehemu ya mkakati wa Extra Bongo kuzidi kuimarisha safu yake ya unenguaji inayoongozwa na mkongwe Super Nyamwela na Otilia Boniface.
Alisema onyesho hilo litakuwa ni maalumu kwa wakazi wa Kigamboni na vitongoji vyake kuona shoo mpya za bendi hiyo zikichagizwa na ujio mpya wanenguaji hao ambao wametokea katika bendi ya Wenge Maison Merre ya Werrason Ngiama Makanda na kwa mwanamuziki Ferre Gorra.
Aliwataja wanenguaji hao kuwa ni Jolie Kindu aka Mrisho Ngassa na Fatuma Grace aka John Bocco ambao mara baada ya onyesho hilo watatambulishwa Ijumaa ndani ya Ukumbi wa Eliada Port View Pugu kwa Mjomba huku Jumamosi zoezi hilo likiendelea ndani ya kiwanja chao cha nyumbani Meeda Club Sinza na kuhitimisha Jumapili kwenye bonanza lao ndani ya jumba la maraha Dar West Park Tabata.
Aliwataka mashabiki na wadau mbalimbali kujitokeza kwa wingi kushuhudia staili na nyimbo mpya za bendi hiyo kama 'Hafidhi' utunzi wa Athanas Muntanabe, 'Mgeni' Khadija Mnoga 'Kimobitel' na 'Wanawake' wa Papii Catalogie.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment