Na,
Albert Sanga, Iringa.
Leo ni mwaka mmoja kamili umepita tangu nilipoandika makala
hapa safuni iliyokuwa na kichwa, “Njooni shambani mtajirike”. Ilikuwa ni makala
iliyotoa shime kwa watanzania kuchangamkia fursa ya uwekezaji kwenye kilimo cha
miti.
Mchambuzi wa makala haya, Albert Sanga
Katika makala ile niliwaeleza watanzania upana wa faida ya
kuwekeza katika miti aina mbalimbali huku nikijikita katika miti ya mbao,
karatasi na nguzo. Nilichambua kwa kina
sana gharama za upandaji wa miti hiyo, muda wa kuvuna, soko lake lilivyo na
matarajio ya biashara hiyo kwa miaka ya baadae.
Leo ninaandika tena makala hii huku nikiwa na furaha tele
moyoni mwangu kwa sababu makumi ya watanzania waliuitikia mwito wangu na
wakachangamkia fursa hii. Kama ambavyo nilitamani iwe, ndivyo ilivyokuwa kwani
wengi wamenijulisha kuwa hawakulazia damu, walichangamka na kuanza kuwekeza.
Ingawa mimi ni mmoja ya watanzania ambao wanajishughulisha
na uwekezaji katika mashamba ya miti mkoani Iringa, kiu yangu ilikuwa ni kuona
watu wakichangamkia fursa hii mahali kokote inakopatikana. Mikoa ya Tanga,
Njombe, Mtwara, Tabora, Mbeya, Bukoba na kwingine kwingi kunastawi miti ya aina
mbalimbali.
Kwa hakika wengi wameendelea kufanya hivyo kwani wamekuwa
wakinijulisha. Wapo makumi waliosafiri hadi hapa Iringa kujifunza na kujionea
fursa hii inavyowanufaisha na kuwatajirisha watu; kati yao wapo walioamua
kuanza kuwekeza na wapo ambao walirudi makwao ili kujipanga kwa ajili ya
kuwekeza wakati ujao.
Furaha yangu ilikuwa kubwa zaidi pale ambapo wapo waliofika
kujifunza hapa Iringa kasha wakaenda katika maeneo yao na kuanza kuwekeza. Wapo
mamia ambao walizungumza nami kwa simu kutoka maeneo mbalimbali wakiwa
wamevutiwa na habari zile.
Nami kwa moyo mkunjufu nilishirikishana nao uzoefu wangu na
kuwahamasisha waanze hata kama ni kidogo kidogo mahali popote wanapoona inafaa.
Ni jambo la kujivunia na la fahari kutamka kwamba makala ile imekuwa na
‘impact’ kubwa mno kwa mamia ya watanzania ambao walihamasika kuanza kuwekeza
katika miti kule Tanga, Tabora, Mbeya, Mtwara, Morogoro na wengine wengi hapa
Iringa.
Kama ambavyo nimekuwa nikisema mara kwa mara katika makala
zangu; ni kwamba muda wa kulalamika lalamika umekwisha. Mazoea na utamaduni wa
watanzania wengi kudhani kwamba tunaonewa wakati wote haujatusaidia mpaka hapa
kwa jinsi hii hakuna sababu ya kuendelea nao.
Mtindo wa kuishi maisha ya kutaka kuhurumiwa yanatupotezea
muda wenye thamani. Tumekuwa tukilalamika kuwa wageni (wanaokuja kwa jina la
wawekezaji) wanatupora ardhi; lakini tusichokitafakari ni hiki, “Mimi kama
mtanzania kwa nafsi yangu na kwa uwezo wangu nimefanya nini cha maana katika
ardhi ninayoweza kuipata hapa nchini ama ninayomiliki?”.
Bahati nzuri ni kwamba idadi kubwa ya watanzania tunafahamu
kuwa ardhi ni utajiri; lakini hatufanyi juhudi za makusudi kuuvumbua na
kuutumia utajiri huo. Tunayo mamilioni ya hekta za ardhi zenye rutuba na
zinazofaa kwa kilimo cha aina mbalimbali lakini bidii zetu hazijatosha hata
tufike mahali tuseme ardhi haitutoshi.
Itakumbukwa kuwa wakati nikiandika makala ile mwaka jana pia
nilizindua kampeni ya kimazingira niliyoibatiza jina la “Green The World And
Become Rich”. Kimsingi kampeni hii
nililenga kuwahamasisha watanzania washiriki kikamilifu katika utunzaji wa
mazingira na wakati huo huo wakitengeneza utajiri.
Unapochukua fedha yako na kuwekeza kwenye shamba la miti
moja kwa moja unakuwa umetunza mazingira kupitia miti uliyopanda lakini pia
usiku na mchana kadiri miti inavyoendelea kukua unakuwa ukitengeneza mamilioni.
Na hii ni namna moja nzuri ambayo watanzania tunaweza
kuwekeza kwenye ardhi. Leo unapanda miti inakaa miaka saba ama kumi unavuna
halafu baada ya hapo ardhi yako unaitafutia matumizi mengine. Si hivyo tu,
lakini katika hiki hiki kilimo cha miti; ndani ya shamba lako unaweza kufuga
nyuki, ukawa unavuna asali hukuku ukisubiri kuvuna miti yako.
Msukumo wa kuanzisha kampeni hii ya “Green The World And
Become Rich” niliupata baada ya kutafakari nafasi walizonazo watu wengi wenye
nia ya kuwekeza katika kilimo cha miti na katika ardhi kwa ujumla. Nilifahamu
kuwa sio rahisi sana kwa mtu kutumia fedha zake na kupanda miti kwa faida moja
tu ya kutunza mazingira.
Nilijaribu kufikiri namna ya kuongeza thamani; hivyo
ilinibidi nifanye kazi ya kuwaelimisha watu mbalimbali mambo mengi kuhusu miti,
biashara yake na namna inavyolipa.
Ninafahamu kuwa mamia ya wanaoendelea
kuwekeza kwenye miti sehemu mbalimbali Tanzania, kufuatia kampeni yangu;
wanawezekeza kwa mtazamo wa kupata faida kifedha huko mbeleni.
Hilo ni jema sana lakini wakati huo huo mimi na wadau
wengine wa mazingira tunashangilia kwa sababu mazingira yanaimarika huku watu
wakitajirika.
Vile vile Nilitambua kuwa wengi wanaweza wasiwe na taarifa sahihi
kuhusu kilimo hiki, kwa maana ya maeneo kinakostawi, taratibu za upataji
maeneo, lakini kubwa kuliko yote ni namna ya usimamiaji pindi wakiwa mbali.
Nilifahamu mtu angeweza kujiuliza maswali mengi yakiwemo;
“Nitawezaje kumiliki shamba Tabora wakati mimi kikazi nipo DaresSalaam?”,
“Nitawezaje kufahamu biashara ya mbao, magogo, pindi ukifika muda wa kuvuna?”,
“ Mbali na faida nitajuaje gharama za uendeshaji na je nitazimudu?”.
Katika kampeni hii kulikuwa na majibu yote ambao kwa wale
waliovutiwa kuwekeza Iringa katika maeneo inakowekeza kampuni yangu,
nilijitolea kuwapa usaidizi wa kuwatunzia na kuyahudumia mashamba yao. Fursa
bado zipo nyingi, watanzania wenzangu tusilale.
Ninapoandika makala haya leo ninatumia wasaa huu
kuwakumbusha wale jamaa zangu wa kule Tanga, Tabora, Mbeya na kwingine ambao
waliniahidi kuwa wataanza kuwekeza katika maeneo yao mwakani (yaani mwaka huu).
Msimu ndio umeanza, kuandaa mashamba, kuaandaa miche na
maandalizi mengine. Hapo hapo mlipo fanyeni kitu katika ardhi zenu, wekezeni
kwa manufaa yenu na ya watoto wenu, isaidieni dunia kwa kuboresha mazingira
yake.
Wale waliofika Iringa wengi wao nilikuwa ninawapa zawadi ya
nakala ya sheria ya ardhi ya mwaka 1999. Na wengine waliokuwa wakiwasiliana
nami nilikuwa ninawapa semina fupi kuhusu sheria ya ardhi. Kiujumla sheria hii
inatupendelea mno wazawa tofauti na malalamiko mengi ambayo huwa ninayasikia.
Pengine Watanzania tuna tatizo katika ubunifu na inapotokea
wengine wamebuni tunakuwa wepesi wa kudhani wametuibia. Mathalani, tunaishi na
ardhi tusiyoifanyia kazi miaka nenda rudi, akitokea mwekezaji akabuni mradi
Fulani katika ardhi hiyo; tunaanza kuja juu! Hatujiulizi tulikuwa wapi na kwa
nini hatukuchangamkia?
Kingine kinachotumaliza Watanzania wengi ni ile dhana ya
kudhani kuwa kilimo ni utumwa, shamba tunaona ni kwa ajili ya waganga njaa na
waliokosa nafasi ya kupata ajira nzuri.
Hii ni dhana mbaya na inachangia sana
watanzania kutokuwa na mikakati ya kuitumia ardhi kikamilifu.
Hata hivyo nikiri kuwa wapo watanzania ambao wanatambua
thamani ya ardhi na wanaitumia ardhi vizuri kwa uzalishaji na uwekezaji wenye
tija. Lakini idadi hiyo haitoshi ukilinganisha na idadi ya wasiotambua nguvu na
utajiri wa ardhi ambao wanaendelea kulalamika ugumu wa maisha na waliopoteza
tumaini.
Jambo jingine linalotumaliza watanzania ni kutokuwa na maono
ya muda mrefu. Wengi wetu tunataka mambo ya papo kwa papo, hatupendi kuangalia
mambo ya vipindi virefu mbele. Mfano mzuri ni katika hili la uwekezaji katika
ardhi.
Mtu anaona ni kupoteza fedha kununua shamba leo ambalo
pengine linaweza kuja kutumika miaka ishirini huko baadae. Mtu anaona ni kama
kupoteza fedha kupanda miti leo ambayo atakuja kuivuna miaka saba ama miaka
kumi ijayo.
Wasichokumbuka wengi ni kuwa unachopuuza kufanya leo kwa
gharama ndogo miaka ishirini ama kumi ijayo hutakuwa na uwezo wa kukifanya hata
kama ukitamani. Mzee wangu mmoja hapa Iringa alinisimulia namna alivyopuuza
kununua kiwanja kimoja hapa mjini Iringa mtaa wa Miyomboni mwaka 1994.
Wakati huo anasema kiwanja hicho kilikuwa kikiuzwa kwa shilingi
laki nne; lakini mwaka jana, 2012 kimeuzwa kwa milioni 320! Mzee wangu huyu anasema
mwaka huo 1994 laki nne kwake zilikuwa ni hela ndogo sana lakini akapuuza. Leo
hii miaka 20 baadae kiwanja kile kile kimeuzwa mara mia nane ya bei aliyoipuuza
ilhali yeye (mzee wangu huyu) leo hana hata ujanja wa kupata milioni kumi!
Kwa maneno yake anasema, “Ningekuwa na mipango ya muda mrefu
katika kuwekeza kwenye viwanja, ardhi na mashamba, leo mimi ningekuwa milionea
hapa mjini” Anachofanya mzee wangu huyu ni utekelezaji wa ule msemo, “Majuto ni
mjukuu”!
Watanzania tusilale, ushindi wetu kiuchumi umo ardhini!
stepwiseexpert@gmail.com
+255 719 127 901
No comments:
Post a Comment