https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Friday, August 23, 2013

Kivumbi cha Ligi ya Tanzania Bara kuanza kesho kwa viwanja saba kuwaka moto

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MICHUANO ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu wa 2013/2014 inaanza kutimua vumbi kesho (Agosti 24 mwaka huu) katika viwanja saba tofauti huku mabingwa watetezi Yanga wakianza kutetea ubingwa wao kwa kuikaribisha Ashanti United kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Wachezaji wa Simba katika moja ya matukio ya mazoezi yao.
Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Azam ya Dar es Salaam na wenyeji Mtibwa Sugar. Oljoro JKT itaikaribisha Coastal Union kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha.

Mgambo Shooting itaoneshana kazi na JKT Ruvu ambayo hivi sasa iko chini ya Kocha Mbwana Makata. Mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga wakati Rhino Rangers itakwaruzana na Simba katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

Mbeya City iliyopanda VPL msimu huu itapimana ubavu na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya huku Ruvu Shooting ikiialika Mabatini, Mlandizi timu ya Tanzania Prisons kutoka Mbeya.

Mzunguko wa pili wa ligi hiyo utachezwa Agosti 28 mwaka huu. Baada ya hapo ligi itasimama kupitisha mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Gambia na Tanzania (Taifa Stars) itakayochezwa Septemba 7 mwaka huu jijini Banjul. VPL itaingia mzunguko wa tatu Septemba 14 mwaka huu.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...