Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KAMA kuna watu hawataki kuamini kuwa msanii Nassib
Abdulmalick maarufu kama 'Diamond Platinum' ni mkali na mwenye ukwasi wa kutosha tu, huu ndio muda wao wa kuamini kinachosemwa.
Hapa Diamond akiwa nchini Uingereza kwenye safari zake za kimuziki.
Ni pale alipoweza kuwakusanya wasanii, wadau wake na
waandishi wa habari katika hoteli ya Serena, iliyopo jijini Dar es Salaam kwa
ajili ya kuzindua video ya wimbo wake ujulikanao kama My Number 1.
Diamond alipokuwa anamkabidhi gari lake mzee Gurumo.
Watu wengi wanataka kusikia kinachotakwa kusemwa na msanii
Nassib Abdulmalick ama Diamond Platinum kama anavyopenda kutambulika hivyo
katika tasnia ya muziki wa kizazi kipya.
Msanii Diamond alipokuwa akizungumza wageni wake aliowaita katika Hoteli ya Serena, juzi jijini Dar es Salaam.
Wapo waliokuwa wakibashiri labda anataka kumtambulisha
mpenzi mwingine kama ilivyokuwa kawaida yake. Hizi zilitokana na kauli ya
msanii Diamond alipowakalibisha wadau walioalikwa katika tukio la kuonyesha
video yake mpya ya ‘My Number 1’.
Hakika kulikuwa na maswali kadhaa yaliyoshangaza wengi.
Kwanini Diamond? Huyu ni nani? Mbali na kutaka kuonyesha video yake mpya, kipi
kingine anataka kusema?
Ikumbukwe huyu ni miongoni mwa wasanii waliozaliwa katika
familia za kimasikini mno ndani ya ardhi ya Tanzania. Amekulia katika mitaa ya
kifukara, Tandale jijini Dar es Salaam.
Mbali na kuzaliwa katika familia hiyo, Diamond wa leo
anatajwa kuwa moja ya wasanii matajiri hapa Tanzania. Kwa kushihirisha hilo,
Diamond amekuwa msanii wa kwanza wa kizazi kipya kuweza kuandaa tukio la aina
yake katika hoteli ya nyota tano, yani Serena Hotel.
Amealika wadau kadhaa wa muziki akiwamo Mzee Muhdin Gurumo,
bila kusahau waandishi wa habari. Miaka mine iliyopita, Diamond alikuwa na
ndoto za kuhakikisha kuwa Tandale wanaishi kwa raha kwa kuwapatia huduma
muhimu, ikiwamo misaada ya kujikinga na malaria.
Kwa kawaida hali ndani ya Hoteli ya Serena ilikuwa shwari na
kilaa mmoja kuwa na mshawasha wa kuangalia kila kinachojiri kwenye pilika
pilika hizo za Diamond wa Tandale hadi wa Serena.
“Maisha yangu yamekuwa yakichangiwa mno na kujituma kwangu,
kufanya kazi kwa bidii bila kuchoka, ndio maana nimekuwa nikifikia katika
mazingira kama haya,” alisema Diamond.
Wakati hayao yakijiri ndani ya viunga hivyo ambapo idadi
kubwa ya watu ilikuwa imejitokeza kama vile Profesa Jay, Mwana FA, AY, Madee,
Queen Doreen, Sheta bila kusahau nyota wa filamu Tanzania, wakiongozwa na Jacob
Stephen, Vicent Kigosi Ray, Irene Uwoya na wengine wengi, watu walikuwa
wakiendelea kujadili hili na lile, sanjari na kupata vinywaji kupoza makoo yao.
Msanii huyo anayeijua vyema kazi yake, aliweza kupanda
jukwaani na kufanya shoo moja matata, ikiwa ni utambulisho wa mtindo mpya wa
uchezaji katika video yake hiyo.
“Hii video yangu nimeifanya nchini Afrika Kusini ambapo
iliweza kunigharimu Shilingi Milioni 50 za Kitanzania sanjari na kunifanya
nionekane Diamond mpya kabisa.
“Ukifanya kazi nzuri ni sababu ya kukupandisha juu, japo
katika kuandaa video hii nilichanganywa na vitu vingi, hasa mazingira mazima ya
kuhakikisha nafanya kazi nzuri,” alisema.
Wakati hayo yakiendelea, msanii Diamond alishika tena kipaza
sauti kwa ajili ya kuzungumza jambo jingine ambalo alikusudia kuwaambia
Watanzania.
Ni pale alipotangaza kumnunua gari mwanamuziki mkongwe
Muhdin Gurumo, aliyetangaza kustaafu muziki akiwa ndani ya bendi ya Msondo
Ngoma.
Diamond anasema kuwa alishikwa na uchungu alipomsikia mzee
Gurumo akilalamika kuachana na muziki huku akiwa hana chaa kujivunia, jambo
ambalo kwake linamkera.
Aidha, hayo yote yametokea yakichaangiwa pia na Gurumo
kuwaambia Watanzania kuwa anapenda kazi za Diamond, akiwa ni msanii anayefanya
vyema katika tasnia hiyo.
“Jambo hili lilinifanya nipate furaha kupita kiasi
nilipomsikia mzee Gurumo akisema kuwa anapenda kazi zangu, ukizingatia kuwa
sisi wasanii wote tuliopo sasa tumetokana na kuangalia kazi za wakongwe wetu.
“Kwasababu hiyo basi, nimeamua kwa mapenzi yangu kwake
kumnunua gari mzee Gurumo ili liweze kumsaidia katika mambo yake, ukiwa ni
sehemu ndogo ya mchango wangu kwake,” alisema.
Hatua ya msanii huyo kumkabidhi ilizua gumzo ndani ya hoteli
hiyo, kila mmoja akisema lake, hasa baada ya kuongozana hadi nje kulikopaki gari
hilo aina ya Toyota Von Cargo FunCargo lenye thamani isiyopungua milioni saba.
Baada ya kupewa gari hilo, mzee Gurumo alishindwa kuzungumza
kwa kirefu, akisema kuwa pumzi yake imegubikwa na furaha, hivyo sauti yake
inashindwa kutoka kwa urahisi.
“Hili ni jambo kubwa linalonifanya nishindwe kuaamini mke
wangu nyumbani atasema nini, hasa kwa kijana Diamond kuninunulia gari bila hata
kutarajia.
“Namuombea kwa Mungu na hakika kila lenye kheri liwe ndani
yake kwa kitendo chake cha kiungwana ambapo ameweza kunikomboa na kunifuta
machozi,” alisema Gurumo.
Pamoja na yote hayo kutokea, wajuzi wa mambo wanaendelea
kuwaza, kwanini msanii huyo ameamua kufanya mkutano wake katika hoteli ya
Serena, yenye hadhi?
Jibu linalopatikana ni kutokana na mafanikio anayoendelea
kuyapata siku hadi siku, ndio maana amekuwa mwepesi kubuni mambo ya
kumtenganisha na nyota wengine.
Ni kama kuweka historia katika sanaa hiyo. Kwa wale
wanaoendelea kupata msoto, lazima waamini kuwa kuna siku isiyokuwa na jina
wanaweza kufikia walau robo ya mafanikio ya Diamond.
Kila kona anatajwa yeye. Akina dada ndio usiseme hadi
Diamond kujipachika jina la Sukari ya warembo. Haya ni mafanikio ambayo yeye
mwenyewe anasema yanatokea kwasababu ya kujituma kwake katika tasnia hiyo ya
muziki wa kizazi kipya nchini.
Ukiacha wimbo huo wa My Number 1, Diamond pia anatamba na
nyimbo zake za Kamwambie, Nataka Kulewa, Mbagala, Nimpende Nani, Kesho na
nyinginezo lukuki.
Baada ya kuyaona hayo ya Diamond, swali linabaki vichwani
mwa wadau wa muziki hapa nchini kuwa nani anaweza kufuata nyayo zake? Je,
kwanini wadau wasiamini kuwa msanii huyo ana mafanikio makubwa kiasi cha
kufikia kumnunulia gari mzee Gurumo?
No comments:
Post a Comment