Na Kambi Mbwana, Dar es
Salaam
NI ajabu kama kuna Mtanzana mwenye
mapenzi mema na Taifa lake, bila kuanagalia anatokea Tanzania Bara au Visiwani,
kisha akatembea akicheka kwasababu ya matukio yanayoichafua nchi yake.
Watu hao ni wale wanaopita kona zote wakifanya fujo au hata kumwagia wageni acid tindikali, wakiwamo mabinti wawili wa nchini Uingereza waliojikuta wakikumbwa na balaa hilo mjini Zanzibar.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete kushoto akifurahia jambo na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.
Kirstie Trup na rafiki
yake Katie Gee walikutana na dhahma hiyo, wakiwa sehemu ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, yani Zanzibar, ambapo sasa wamerudishwa nyumbani kwao kwa
matibabu.
Baada ya kutokea kwa kadhia hiyo
ambapo ni mwendelezo wa matukio yanayoichafua Tanzania nje ya mipaka yake, kila
mtu anasema lake, hasa vyombo vya habari vya Kimataifa vinavyoandika habari
zinazoonyesha namna gani watalii hao wametiwa vilema vya maisha.
Wapo wanaondika kwa kupoza, akiwamo
mhariri wa masuala ya Utalii wa Gazeti la Mirror, nchini Uingereza aliyeandika
kwa kupoza kidogo katika tukio hilo ambalo kila Mtanzania anapaswa kulikemea
kwa vitendo.
“Ninaweza kusema kwamba hakuna
sababu ya kutokwenda Zanzibar kwa vile ni mahali salama, panafurahisha na kuna
fukwe nzuri na mambo ya kihistoria yenye umaarufu mkubwa,” aliandika Nigel
Thompson kwenye gazeti hilo.
Hizi ni miongoni mwa
kauli mbalimbali zilizotolewa na wadau wa amani, utalii duniani, ikiwa ni saa
chache baada ya raia wa Uingereza kumwagiwa tindakali, wakiwa mjini Zanzibar,
Agosti 8 mwaka huu.
Kwa tukio kama hilo,
hakika Dunia inatupa jicho lake visiwani Zanzibar, huku hisia za kila aina
zikishika kasi katika wakati ambao kila Mtanzania anatamani kuona nchi yake
inapiga hatua.
Japo uchunguzi haujaweza
kuthibitisha chanzo cha tukio hilo, zaidi ya wale wanaodhamiwa, akiwamo Sheikh
Ponda Issa Ponda, aliyetajwa hadharani katika vyombo vya habari vya Kimataifa
kuwa anajua kilichotokea juu ya tukio la kumwagiwa tindikali kwa mabinti wa
Uingereza.
Hilo halijabainika, japo
najua kuwa kitendo kama hicho ni kuichafua nchi katika ramani za Kimataifa,
ukizingatia kuwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, hakuna anayepaswa kuchekea
hilo.
Endapo nchi itatumbukia
katika hatari hiyo ya kumwagia watalii tindikali, sekta ya utalii inaweza
kushuka kwa kiasi kikubwa mno, hivyo kuufanya umasikini uote mizizi kwa
Watanzania wote.
Watalii zaidi ya 17,000
kwa mwaka wanaotembelea Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watasusa, wakihofia
usalama wao ambao kwa siku za hivi karibuni habari mbaya zinaripotiwa kutokea.
Vyama vyote vya siasa
sambamba na wadau wa utalii wanapaswa kuwa makini katika suala hili,
ukizingatia kuwa ndio kinachoweza kukuza uchumi wan chi endapo suala la utalii
litapiga hatua.
Chama Cha Wananchi
(CUF), Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama Cha Mapinduzi (CCM) TLP,
UDP na vinginevyo vinatakiwa kuizungumza hoja hii bila woga kwa wanachama wao.
Dk Ali Mohamed Shein
kama Rais wa Zanzibar kwa kushirikiana na serikali yake ya Umoja wa Kitaifa
(SUK) sambamba na CUF, huku Maalim Seif Sharrif Hamad ambaye ndio Makamu wa
Kwanza wa Rais, wanapaswa kuwa wamoja kujadili tukio hili na mengineyo
yasiyokuwa na tija kwa Watanzania.
Hatuhitaji matukio hayo
yawe sehemu ya kawaida kwa Tanzania, bila kusahau Zanzibar inayotegemea utalii
ili kukuza uchumi wao.
Vikundi vya kidini
vinavyoibuka vinaishia kuivua nguo Zanzibar inayopendeza na kuvutia watu
kuingia humo kujionea mambo ya kale na madhari inayovutia kuitazama kila
wakati.
Uamsho wanaotajwa kila
pembe ya nchi yetu nao wanapaswa kufahamu kelele zote zinazotokea sasa, ni kwa
sababu ya amani iliyopo na uchumi unaokuzwa na sekta ya utalii.
Lazima wajuwe kuwa
wakitumia vibaya nafasi zao, kuheshimiwa kwao mbele ya jamii wataiweka Zanzibar
katika wakati mgumu mno. Vizazi vijavyo havitaweza kuishi kwa amani na utulivu.
Watoto wao watakufa njaa na kushindwa kuongoza, maana sekta ya utalii
inayotegemewa itakuwa imeanguka.
Nani asiyejua kuwa Tanzania
imekuwa ikitegema misaada ya wahisani kutoka nchi mbalimbali duniani. Wahisani
ambao wanapojaribu kuja, wanahofia usalama wao, hivyo hili haliwezi kuchekewa.
Sekta ya utalii ni
muhimu na imekuwa ikitegemewa na Mataifa mengi duniani, ili kukuza uchumi wao,
ingawa Watanzania wao hawaoni thamani hiyo na kujikuta wakiwakimbiza watalii.
Kuwamwagia tindikali
wageni wetu ni kurahisisha umasikini wetu. Hatuna tunachoweza kuambulia katika
suala hilo. Nini faida ya vitendo hivi? Nani
amekusudia kuliangamiza Taifa nje ya mipaka yake.
Hakuna dini inayoruhusu
machafuko au kuwamwagia binadamu wenzao tindikali kwa faida wanayojua wenyewe.
Kama hivyo ndivyo, hatuwezi kubaki kimya wakati nchi yetu inaangamia.
Haya ni mambo
yanayotakiwa kupigwa vita na Watanzania wote, ndio maana hata Mjumbe wa Baraza
la Wawakilishi ambaye pia ni kiongozi kutoka CUF, Ismail Jussa, hajabaki nyuma
kukemea suala hilo.
Lazima serikali ifanye juhudi katika
hili ili vikomeshwe. Kuna hatari ya Tanzania kushindwa kupiga hatua, kama
watalii wataona nchi hii sio mahali sahihi kwa kuishi wala kutembelea.
Doria
za polisi ndani ya Mji Mkongwe ambao bado unabakia kuwa ndiyo mji mkuu wa
Zanzibar na pia kituo kikuu cha harakati zote za kiuchumi ikiwemo biashara na
utalii, ziongezwe ili kupambana na watu wenye mtazamo wao usiokuwa wa Kitaifa
zaidi.
Wananchi
nao waingie kwenye imani ya kulitetea Taifa, huku vitendo visivyokuwa na tija
kupingwa, ukiwamo utaratibu wa kuwafichua watu wanaofanya uhalifu wa aina hiyo.
Ni
kweli Zanzibar inavutia. Inapendeza kutembelewa na kila mmoja wetu, lakini kama
hakuna amani hizo ni porojo. Hakuna anayeweza kujitoa mhanga katika hilo, ndio
maana kuna haja sasa ya kuliwekea mkazo suala la amani, ushirikiano na
kuwakemea wanaofanya vitendo vya uhalifu, hasa kuwamwagia tindikali na
mengineyo.
Zaidi
Watanzania wenyewe tutajaribu kuharibu mfumo mzima wa utalii wetu, bila kujua
athari zinazoweza kulitia Taifa katika umasikini wa milele.
Naungana
na Jussa aliposhauri kamera za mitaani za kufuatilia nyenendo za watu (Surveillance
Cameras).
Mpango
huu pia utaleta amani na kuondoa hofu watalii wanaoamua kuitembelea Tanzania
ili wajionee vivutio vya utalii vilivyozagaa kila pembe ya nchi yetu.
Kuiweka
Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika hali ya amani na utulivu ni jukumu letu
sote, maana jambo hilo litatuweka katika mazingira mazuri kwenye sekta ya
utalii duniani.
Wapo
wanaotaka Zanzibar liwe Taifa la Kiislamu. Hao wanafika mbali kwa kuingiza
chokochoko za kila aina, ukiwamo mgogoro wa Muungano unaoleta vuta nikuvute kwa
Watanzania wote.
Kama
kuna anayetaka kuleta chokochoko kwasababu za Muungano, basi ni bora akatumia
njia nzuri ya maelewano, mazungumzo huku akichambua kwa hoja namna gani nchi
ifuate anachotaka.
Lakini
kuonyesha hasira zake kwa kutoa uhai wa mwingine au kumpa kilema cha maisha, ni
jambo lisilovumilika hata kidogo. Tuyaseme haya bila woga kwa ajili ya
maendeleo ya nchi yetu.
Tanzania
ni nchi yote. Tukiichafua kwa namna yoyote ile, hasara yake ni kubwa mno, hivyo
lazima tuwe makini katika suala hili. Huu ndio ukweli wa mambo. Tuujuwe na
kuuzingatia pia.
+255 712053949
Mwisho
No comments:
Post a Comment