Na Sadiki Mbwana, Handeni
Timu ya soka Mashorobaro wamefanikiwa kuibuka na ushindi wa
mabao 4-2 dhidi ya mahasimu zao Men Stone, zote za kijiji cha Komsala, wilayani
Handeni, mkoani Tanga, katika mchezo wa kusisimua wa kirafiki wa sherehe za Idd
El Fitri.
Mchezo huo ulikuwa na shangwe za aina yake kutokana na
burudani ya aina yake dhidi ya vipai vya kucheza soka kwa vijana hao wanaowika
pia katika mashindano mbalimbali yanayoanzishwa katika Kata ya Kwamatuku,
wilayani Handeni mkoani Tanga.
Mabao ya Mashorobaro yaliwekwa kimiani na Julius Mwashiti, Malilo
Gerevas, Juma Shaban na Joseph Goliama, wakati yale ya Men Stone yalifungwa na Hassan
Kamota na Ally Hausi, likiwa ni pambano lililojaa ufundi wa kila aina.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo, mmoja wa mashuhuda wa
mchezo huo, Said Ling’ande, alisema kuwa mechi hiyo ilikuwa na msisimko wa aina
yake, hivyo wanaamini watazamaji walipata burudani kamili.
“Kijiji hiki kimesheheni vipaji vya aina yake katika
uchezaji wa soka, hivyo kunaposekana mechi za mashindano, wenyewe wanaingia
uwanjani kwasababu kuna timu nyingi na zote zinacheza soka la uhakika.
“Tunashukuru Mungu kwa nguvu zake, hivyo hatuoni sababu ya
kuendelea kukaa tu wakati watu wana vipaji vyao, ndio maana tunajaribu
kujihusisha na michezo ikiwa ni kufanya mazoezi, ukizingatia kuwa michezo ni
afya,” alisema Ling’ande.
Komsala ni kijiji cha kwanza kilichopo wilayani Handeni,
mkoani Tanga, kinachopakana na wilaya ya Korogwe, huku kikiwa na vijana wengi
wenye vipaji vya kucheza soka, licha ya eneo hilo kuadimika masuala ya
kimichezo.
No comments:
Post a Comment