Na Kambi
Mbwana, Dar es Salaam
NITAMSHANGAA
Mtanzania yoyote anayeweza kufurahia nchi za Tanzania na Rwanda kuendelea
kurushiana maneno makali kuonyesha uhusiano mbaya ulioanza kwa siku za hivi karibuni.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete, pichani
Tangu Mwezi
Mei mwaka huu wa 2013, baadhi ya matamko mabaya yamekuwa yakitolewa na viongozi
wa Rwanda. Wanasema mengi kuonyesha chuki zao kwa Watanzania na rais wao kwa
ujumla.
Paul Kagame, Rais wa Rwanda
Kwa
kuangalia sakata lote linaloshika kasi, ila si sababu ya Tanzania kujibu
mashambulizi dhidi ya Taifa hilo linaloongozwa na Paul Kagame, maana ni kuzidi
kukuza uhasama huo.
Ni wazi kuwa
nchi ya Rwanda inayotajwa kufadhili machafuko nchini Kongo, hasa kwa kikundi
cha M23 inaleta chokochoko kwa Tanzania, pale Rais Kikwete, alipowataka wakae
na waasi kujadili tatizo.
Hali hii
inashangaza mno. Kauli ya furaha inapobadilishwa na kuwa chuki na uhasama, tena
bila sababu za msingi. Labda kuna sababu nyingine, ila si haya yaliyozungumzwa
na Kikwete.
Wakati
naangalia kwa kina mtifuano huo, kwa upande wangu nitakuwa wa mwisho kufurahia
au kuombea mabaya kwa mataifa haya mawili, yani Tanzania na Rwanda.
Tanzania ili
iweze kukua kiuchumi, inahitaji ushirikiano kutoka kwa majirani zake. Nchi hizi
zinategemeana. Rwanda wanaihitaji Tanzania na Watanzania wanahitaji uwapo wa
ndugu zao.
Sipendi kuona
uhusiano mbaya kwa nchi za Tanzania na Rwanda unakua, nikiamini ni hatua
isiyokuwa na faida zaidi ya hasara kwa mataifa haya mawili yanayopigania
kujitawala wenyewe.
Katika
hotuba yake aliyoitoa mwishoni mwa mwezi uliopita, Rais Kikwete alielezea mambo
mengi dhidi ya Rwanda, akisititiza kuwa alinukuliwa vibaya na ushauri wake
kupindishwa.
Rais Kikwete
aliwatangazia umma kuwa hakuna sababu ya kugombana na Rwanda, japo alikiri kutukanwa
na majirani zetu hao.
Haya ni
matatizo makubwa kwa viongozi wa Afrika. Kagame, akiwa kama rais wa Rwanda, ni
vyema akazingatia nidhamu katika utawala wake.
Kagame
anapaswa kujua faida ya amani inavyoweza kuwafanya wananchi wake waishi vizuri.
Wananchi wa Rwanda wasingependa kuona wapo viongozi wanaotamani kulifanya Taifa
hilo liingie kwenye hatari.
Kadhia
waliyoipata mwaka 1994 inatosha. Roho za Rwanda ziliangamia bila sababu. Kama
hivyo ndivyo, nani anaweza kusimama hadharani akachochea vita, huku akijua kuwa
hana faida navyo?
Nani
anayeweza kuelezea faida ya vita, hasa kwa Tanzania na Rwanda, ambazo zenyewe
zinahitaji kuishi kwa kutegemea wahisani, Mataifa makubwa?
Huu si
wakati wa kujenga uhasama. Huu ni wakati wa viongozi wa nchi za Afrika kukaa
pamoja na kusema kwa kauli moja namna ya kuyasaidia mataifa yao.
Mrwanda
apinge kwa nguvu zote kama kuna chokochoko zinazofanywa, zinazotakiwa kufanywa
na viongozi wao leo au kesho.
Mtanzania,
Mkenya, Mburundi, Mkongo na wengine wote wapinge kama kuna anayetaka kumsumbua
mwenzake kwa namna moja ama nyingine.
Inawezekana
wakati mwingine kunatokea migongano ya kimaslahi, ila hakuna ugomvi usiokuwa na
njia ya kusuluhishwa. Mazungumzo mara kadhaa huleta tija na kudumisha jamii
bora.
Hakuna nchi
iliyoendelea kwa kupenda vita, hasa hizi zinazoishi kwa misaada kutoka nchi za
watu. Ukiacha roho za watu zinavyoangamia katika machafuko, pia nchi zinatumia
gharama kubwa kujilinda au kujibu mashambulizi au kununua silaha kwa fedha za
kujenga shule, vituo vya afya na huduma nyingine muhimu kwa wananchi wao.
Rais Kikwete
ameyaona haya. Na kutokana na ustahimilivu wake, akabaini kuwa hakuna sababu ya
maana ya kulumbana na Rwanda, sababu ikiwa kuwashauri kumaliza tofauti zao na
waasi.
Kauli hii
haikuungwa mkono na Kagame. Maneno ya kejeli yakaanza kushika kasi, sambamba na
vijana wao, ikiwa ni njia ya kufikisha matusi kwa Watanzania kwa njia
mbalimbali, ikiwamo mitandao ya kijamii.
Ukiingia
katika mitandao mbalimbali na kufuatilia uhasama huu, utagundua kuwa umefikia
wakati mbaya mno. Inahitaji moyo mno kujitangaza kuwa wewe ni Mtanzania mbele
ya Mrwanda.
Hii si njia
nzuri kwa mataifa haya. Nchi ya Tanzania amani ni jambo la lazima kwa wananchi
wake. Ingawa ina makabila zaidi ya 120, ila yameishi kwa upendo wa hali ya juu.
Wanapokutana
Wazigua na Wasukuma, huwezi ona tofauti yao. Wanaishi kama ndugu. Huwezi kuona
malumbano kati ya Wangoni na Wachaga. Haya ni mambo ya kupongezwa na Watanzania
wote.
Amani hii ni
tunu kutoka kwa Mungu. Ingawa hatuna utajiri wa kupindukia, ila maisha yetu
yamekuwa na furaha tele, jambo linalotangaza sisi ni nani.
Kwasababu
hiyo, yoyote anayeona ana hamu ya kulichanganya Taifa hili, basi aangalie mara
mbili. Japo uwezo wa kufanya lolote upo, lakini nini chanzo?
Chanzo kiwe
hiki cha viongozi kushauriana? Kwani kuna ulazima kufuata ushauri ambao
huutaki? Kwanini sasa ubabaike kwa kushauriwa?
Alipokuwa
Tanzania katika ziara yake, Rais wa Marekani, Barrack Hussein Obama, aliulizwa
juu ya machafuko yanayoendelea nchini Kongo.
Obama
alijibu huku akionyesha kuwa rais wa Tanzania, Kikwete, ana uwezo wa kuyafanyia
kazi hayo, maana yapo ndani ya uwezo wake.
Kauli hii
sio tu imemjenga Kikwete nje ya mipaka yake, pia imeonyesha namna gani
Watanzania wanaongozwa na rais mwenye mtazamo wa kina.
Haya
yanapotokea, kwa rais asiyejitambua, rais mwenye ubinafsi na ubabe usiokuwa na
tija, ana uwezo wa kuchukia kama inavyoonekana sasa.
Anawaza
kwanini asiwe yeye? Na inapotokea mmoja wapo, ikiwamo Rwanda inaanzisha
chokochoko, kama mmoja wao anakuwa hajitambui, uhasama huo utaongezeka.
Ni vyema
wananchi wakapinga kwa nguvu zote kama viongozi wao wanataka kuwaingiza kwenye
uhasama. Watu zaidi 500,000 waliripotiwa kupoteza maisha katika mauaji ya
kimbari mwaka 1994.
Ni idadi
kubwa mno. Sitarajii kuona vifo hivyo vimesahauliwa na wananchi sambamba na
viongozi wao. Ndio maana nasema, suala la machafuko si la kuchekea.
Linazalisha
vizazi tegemezi. Linazalilisha watu kwa kiasi kikubwa mno, hivyo halistahili
kuchekewa. Watu wanazikimbia nchi zao bado wanazipenda.
Akina mama
wajawazito na watoto ndio wanakuwa wahanga wakubwa katika hilo. Wengine
wanapoteza maisha kutokana na njaa, shida ya maji na mengineyo.
Wengine
wanaingiliwa kimwili bila lidhaa yao. Kama haya yanatokea, nani anaumia? Ni
wakati sasa wa viongozi wa Afrika kudumisha umoja na mshikamano.
Hakuna
Tanzania, Rwanda, Kongo, Burundi, Kenya, Msumbiji ama Uganda. Hizi nchi zote
zinapaswa kuishi kwa upendo na kushirikiana kibiashara.
Hatuhitaji
uhasama wa aina yoyote kutoka Rwanda, kama njia ya kukuza uchumi wa nchi hizi
mbili. Wapo baadhi yao wanaochekea machafuko.
Hawa
wameshindwa kung’amua machungu wanayokutana nayo wana jamii wengine kutokana na
matokeo hayo. Mwisho kabisa, napongeza kwa nguvu zote kauli ya Rais Kikwete,
nikiamini kuwa ni mwenye busara.
Pamoja na
matusi yote anayotukanwa, akidhalilishwa, ila yeye anaona hakuna sababu ya
kujibizana vibaya na majirani zao hao, japo uwezo huo upo.
Rwanda ni
Taifa dogo mno. Kinguvu halina ubavu hata robo ya kupambana na ubavu wa
Tanzania. Na wenyewe wanajua hilo. Hata hivyo hakuna sababu kubwa juu ya suala
hilo.
Muhimu ni
viongozi wa nchi zote za Afrika kupendana, kuhubiri amani katika vikao vyao,
maana ndivyo vinavyoweza kuleta maendeleo kwa nchi zao.
Watanzania
tunawapenda na kuwaheshimu majirani zetu, japo sio sababu ya kuonekana si
lolote, maana tunajua uwezo tunao, tena mkubwa mno.
+255
712053949
No comments:
Post a Comment