Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
LEO ni Sikukuu ya Idd el Fitr.
Waislamu wote duniani na wale wasiokuwa waumini wa dini hiyo wanafurahia siku
hiyo baada ya kumaliza mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Waumini wa dini ya Kiislamu wakifanya ibada
Takribani siku 30 Waislamu
walikuwa kwenye mfungo huo, ambao kuna kila sababu ya waumini hao kujitafakari
upya. Kila siku ya Mungu, wenye imani ya dini ya Kiislamu wanatumbukia kwenye
mkanganyiko wa aina yake duniani.
Kumekuwa na changamoto nyingi,
hasa hili la dini moja kuwa na madhehebu lukuki, tena hata yale yasiyokuwa na
tija. Naomba niwe muwazi
Mimi ni muumini wa dini hii ya
Kiislamu. Nimezaliwa katika misingi ya dini hii, hivyo lolote linaloweza
kutokea tofauti, nabaki nawaza namna ya kudumisha jamii bora.
Naelewa kuwa Tanzania haina
dini lakini watu wake wana dini. Rais Jakaya Mrisho Kikwete anaongoza nchi
isiyofungamana na dini yoyote, ila yeye mwenyewe ana dini yake.
Ni wazi tunapaswa kuthaminiana
na kuheshimiana pia. Hata hivyo, ni vyema kwenye mapungufu yasemwe kwa ajili ya
kujenga jamii bora na kuacha mkanganyiko huu.
Ingawa leo ndio siku ya Idd,
lakini jana baadhi ya waislamu waliswali kuonyesha kuwa ndio siku sahihi. Hapa
dini moja, lakini inagubikwa na mkanganyiko mkubwa.
Walioswali jana wamezingatia
nini tofauti na hawa walioswali leo, yani siku ya Ijumaa? Inawezekana
walioswali jana wapo sahihi, lakini ni vyema masheikhe na wanazuoni wakalitolea
ufafanuzi suala hili, kwanini ibada moja inayoangaliwa kuandama kwa mwezi na
kuzama inapokuwa tofauti bila sababu za msingi?
Sheikhe Mkuu wa Tanzania,
Shaban Simba kwa kushirikiana na wanazuoni wengine wa dini ya Kiislamu
wanapaswa kujua kuwa dini yao inapotezwa na mitazamo ya kukanganya.
Mtu anaweza kuhoji, huyu
anayeswali leo na yule aliyefanya hivyo jana kuna otofauti gani wakati wote
wanapaswa kufunga au kufungua kwa kuangalia kuandamana kwa mwezi.
Watu wanasema kuwa mwezi
umeandama Oman, Arabun, hivyo ni wakati wao kuswali Idd. Suala hili
linachanganya na kuumiza sana vichwa, maana hali hii isipoangaliwa huenda ikaharibu
thamani ya Uislamu.
Mtaa mmoja malumbano mengi
yanaibuka. Kila mtu anajiona yupo juu ya mwenzake. Huyu amefunga na yule
amefungua. Hali hii inauma na kukera kupita kiasi.
Vyema suala hilo likaangaliwa
kwa mapana yake. Kuna hatari watoto wanaozaliwa leo wakashindwa kutambua wasimame
wapi.
Dini ya Uislamu inakabiriwa na
changamoto nyingi na ndio maana hadi leo waumini wake wanalia kukandamizwa,
wakati wenyewe wamegawanyika.
Hakuna kinachofanywa kwa ajili
ya kuujenga Uislamu na ndio maana hata uwapo wa Simba Baraza la Waislamu
Tanzania (BAKWATA), linachanganya kuona wengi wao hawakubaliani nalo.
Lengo si kukashifu ila
kuwakumbusha watu wawe makini katika mfumo huu unaoibua maswali kedekede kwenye
jamii.
Nakutakia Idd Njema mdau wa
Handeni Kwetu.
No comments:
Post a Comment