Na Adam
Malinda Seif.
KWA mara
ya kwanza naomba kutumia nafasi hii niliyoomba mwenyewe katika mtandao huu (Blog
ya Handeni Kwetu) ili kuunganisha mawazo ya yangu kwa Watanzania wenzangu,
hususan wale wilaya ya Handeni na kupeana mawazo muafaka kwa mustakabali wa Taifa.
Adam Malinda, mwandishi wa makala haya.
Hii
itafanikiwa kwa kuleta usawa, kushauriana kwa njia ya amani kabisa kutoka kwa sisi
wananchi na viongozi tunaowachagua. Lengo ni si kupata sifa za mtu mmoja mmoja,
bali ni kutafuta jawabu la matatizo ya waliowengi na hatimae kuondokana na
ufukara uliokithiri.
Mkuu wa Wilaya Handeni, Muhingo Rweyemamu, pichani.
Kwa
nafasi hii lengo ni kuunganisha nguvu kila upande ili kuwa kitu kimoja ingawa
nafahamu kutoka hali fulani kwenda nyingine kuna changamoto nyingi ikiwa ni
baadhi ya watu kuona wanaingiliwa katika maslahi yao, bila wao kujali wangapi
wanaathirika na mfumo huo ambao wao kwao ni neema.
Lakini
mara zote linapokuwepo tatizo katika mifumo fulani ya maisha inakuwa
imetengenezwa kwa madhumuni fulani, hivyo tunapaswa kuwa wawazi katika
kubainisha haya tunayoyazungunza yana faida ipi kwa walio wengi, na
kuwasadikisha kuwa yakifanyika haya yataweza kufika kule wanakotarajia wengi,
hali itakayohamasisha maendeleo tunayokusudia.
Nilijisikia
hivi juzi aibu kubwa na kunichoma moyo pale jamaa mmoja ambaye sasa ni
mchungaji wa dhehebu moja tulipokutana katika ofisi ya chombo kimoja cha habari
akisahau kwa kuniuliza hivi wewe ni kutoka eneo gani la Tanzania?
Nikamwambia
natoka Handeni. Jibu lililofuata akaniambia ni wilaya moja ya watu waliochelewa
kimaendeleo. Nilichukia, lakini nikamwambia si kweli, huku nikiumia.
Baadae
kidogo nilimkumbuka kuwa ni mtu ambaye siku hizi amekuwa akitoa kauli za
upiganaji vita vya madawa ya kulevya kupitia kanisa lake. Tulikuwa kukikutana
Mbeya katika ofisi yake ya kupigania uhalibifu wa mazingira miaka 12 iliyopita.
Huyu
mchungaji hadi naandika makala hii bado ananisononesha, lakini kwa upande
wangu najiuliza wanahandeni tulikosea wapi. Tufanye nini, kwa kuwa
kumnyooshea mtu fulani kidole itakuwa si haki. Tujilaumu sisi wenyewe tutafute
jawabu la kweli, tuache majungu, fitna, tuwe wawazi kueleza uhalisia na njia za
kupita, badala ya kutafuta mchawi.
Naomba kila
mtu ajiulize anataka kuifanyia nini Handeni na Tanzania kwa ujumla? Kitu cha
kufanya ili kuondokana na hali ya kudidimia kwa uchumi, kukosa mwelekeo kwa
kizazi cha sasa na kijacho.
Vikwazo
gani vinasababisha kuwepo kwa hali hiyo, lakini pia tujitathimini
michango yetu ianzie katika changamoto ipi. Tusishike kila jambo tutapoteza
mwelekeo kwa kuwa shida ni nyingi kuliko uwezo wetu.
Kupitia
makala haya, ni vema kuanzia sasa kutafute njia za kuunganisha wana Handeni kwa
kuona tuanze kuchangishana, ama kubuni mradi upi utakao weza kuchangia fedha
kidogo kwa ajili ya kutatua kero za wananchi.
Huo utakuwa
mwanzo wa wananchi kukubali jitihada za jamii yote, ikiwa pia ni njia ya kuunga
mkono na kuwa kitu kimoja katika kuleta maendeleo yao kwa ujumla.
Naamini
kuna wasomi wengi waliotokea Handeni karibu kila eneo la nchi lakini mwitikio
ama mrejesho wa elimu zao hazijaonekana katika jamii, hasa katika kuhamasisha
wananchi kujiunga katika kuleta maendele bila kujali dini zao na itikadi za
siasa.
Wanapaswa
kukumbuka kila msomi hata wa kidato cha sita na zaidi ametumia kodi ya wana
Handeni kupata elimu na uwezo aliokuwa nao, deni hilo ni kama halipo kimtazamo
lakini kihalisia lipo, sababu Handeni ni sehemu ya serikali ya Tanzania ambayo
imejenga shule tulizosoma sisi wote.
Handeni
ni sehemu mojawapo katika Tanzania yenye neema ya maziwa na asali, matunda na
nyama, ambavyo kwa afya ya binadamu tunapaswa kunona, kujivunia, na kuheshimika
katika macho ya wengine.
Lakini
imekuwa kinyume chake. Je sisi wazawa tunafurahia hali hii? Kama tunafurahia
basi elimu tuliyonayo haina faida kwa wana Handeni. Kama tunachukizwa kwa dhati
toka mioyoni mwetu wakati ni huu.
Neema ya
dhahabu, ardhi isiyohitaji mbolea ya viwandani, mabonde yanayopitisha maji
mengi nyakati za masika, miti inayoweza kutengenezea samani na matumizi mengine
ya kibinadam tutumie fulsa hii kuona mrejesho wa rasilimali hizi kuinua uchumi
wa Handeni.
Tuanze
sasa kila mmoja wetu kusema ikiwa ni mchango wa kuleta maendeleo kuwa anafikiri
tufanye nini kuondokana na hali hiyo?, miradi gani tunaweza kubuni kujikomboa
na umasikini wa familia zetu, tukikutana pamoja kimawazo, naamini hatushindwi
kujua la kufanya, kwa kuwa wasomi wapo, hatukosi kujua tuanze vipi yapatikane
matrekta ya kilimo cha kisasa, hatutashindwa kutafuta wafadhili kwa ajili ya
miradi ya maji vijijini, hatutashindwa kukopeshwa zana na nyenzo za mashine za
ufyatuaji matofali kuboresha makazi yetu, zahanati na mashule.
Kila mtu
anapaswa kuwa makini katika ufanyaji kazi wake, sanjari na kushirikiana na
mwenzake kwa ajili ya kufanikisha maendeleo ya Handeni na Tanzania kwa ujumla.
Hatuwezi
kubeza hatua zilizofikiwa hadi hapa tulipo, viongozi waliopo wamefanya yale yaliyo
ndani ya uwezo wao, nasi wana Handeni tunapaswa kuwaunga mkono.
Waliochoka
wapunzike nasi tupokee vijiti tukimbie mbali zaidi na kupata ushindi wa
kimaendeleo. Hii ni kutokana na ukweli kuwa baadhi ya watu watapinga jitihada za
kimaendeleo kwakuhofia vyovyote watakavyojua wenyewe.
Nawaomba
wasiwe na moyo huo, uongozi ni kipaji toka kwa mwenyezi mungu, ikiwa
wanalitambua hilo, kila kiongozi ana zama zake hawezi kuwa milele na lazima
ujuwe kuwa kiongozi mwenye busara ni yule anayewapa wananchi wake fulsa ya
kutoa maoni yao, ushauri, na kuwaongoza.
Nasema
hivi kwa kuwa mjadala huu si wa kwanza kufanywa na wakazi wa Handeni, siku
nyingi zilizo pita tukiwa wadogo wengine tukiwa shule wakuu zetu walianzisha
mipango madhubuti, lakini ilihujumiwa na baadhi ya watu kwa maslahi ya
kiutawala, hali iliyozidisha kuidumaza Handeni.
Jambo
hili halikuwa jema, ni dhambi kubwa ambayo sasa tusikubali kuirejea upya kama
kweli tunahitaji maendeleo ya wilaya hii ambayo kwa sasa inatajwa kuwa Mkoa.
Kuhujumu uratibu
wa kimaendeleo ni hatari na sumu inayotafuna wanajamii waliopo na kizazi
kijacho. Naomba nisiwachoshe, tuandae fikra mpya, zenye mashiko, zisizojenga
chuki kati yetu na viongozi.
Tuwape
wananchi fulsa ya kuona nia njema ili nao wachangie mawazo yao, waeleze
dukuduku zao, waseme shida zipi ni kipaumbele kwa Handeni nasi tujue tuanze na
lipi kwa misaada toka wapi yaani wafadhili.
Lakini
kwa wale wenye kuonesha nia na kutaka msaada huku wakiwa wameshaanza kufanya
vitu vinavyoonekana machoni kwa watu.
Tukutane tena Jumamosi ijayo kwa makala za
kweinchili, ubala wa watu walongela kwenchili wakengila mo lwazo, hegu
mwenkondo wamanya houkukongela, ubala wa minde mwaawadole.
adam.seif70@yahoo.com
+255 716236171
No comments:
Post a Comment