Kwa mazingira ya nchi yetu na mazingira ya
kibinadamu, sio rahisi katika Taifa kama hili lenye watu zaidi ya milioni
arobaini, tukawa na dhamira moja, tutajiridhisha kinadharia tu kuwa Muungano
utadumu kwa vile tuna dhamira nao, huku ni kujidanganya. Ni dhahiri kuwa
ikitokea katika mfumo huu wa serikali tatu, tukapata kiongozi mkuu, ama chama,
ama chombo chenye mamlaka ya kutunga sheria, ama kundi la watu ambalo dhamira
yao ni tofauti na dhamira ya wengi.
Ni wazi kuwa pamoja na dhamira nzuri ya walio wengi
wa kudumisha Muungano wa sasa, Muungano utavunjika kwa matakwa ya mamlaka
iliyopo. Kwa maoni yangu Dhamira ya Watanzania katika kudumisha Muungano ni
sehemu tu ya kuimarisha na sio suluhisho la kudumu kwa Muungano.
Muundo madhubuti unaozuia fursa ya kuvunja Muungano
ndio suluhisho sahihi na la kudumu kwa Muungano. Ni vyema Watanzania
tusisahau yale ya mwaka 1977, tulikuwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki, wote
wana Afrika Mashariki tuliipenda Jumuiya yetu, tulikuwa na dhamira ya dhati ya
kuidumisha.
Lakini alitokea mtu mmoja tu kwa matakwa yake, na
akili zake alizoziona zinafaa alisababisha Jumuiya ya Afrika Mashariki
kuvunjika sembuse Muungano wa Serikali tatu?
Waasisi wa Taifa letu, Hayati Abeid Amani wa
Zanzibar na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanganyika, karume
walipoanzisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hawakukurupuka, walikuwa na
sababu za msingi za kuunganisha nchi mbili hizi.
Miongoni mwa sababu hizo ni pamoja na Undugu wa damu
uliopo kati ya Wananchi wa Zanzibar na Tanganyika na pili ni sababu za kiulinzi
na usalama kwa nchi hizi wa mali, rasilimali na watu wake, ninaamini kuwa,
sababu hizi bado ni hai hadi sasa na ni sababu muhimu kwa mustakabali wa
Taifa letu.
Watanzania hivi sasa kupitia mabaraza mbalimbali
wanaendelea kutoa na kukusanya maoni juu ya katiba. wapo wanaopita huku na huko
na wale wanaotumia njia mbalimbali za kutoa maoni yao juu ya Rasimu ya Katiba
na hasa eneo hili la muundo wa serikali tatu.
Ni uhuru wa kila mtu kutoa maoni yake, lakini kuna
haja ya Watanzania kuwa na tahadhari sana, wapo wanaojua fika kuwa kuwepo kwa
serikali tatu, zenye Marais watatu katika nchi yenye mamlaka tatu, ni kuuvunja
Muungano.
Hivyo wapo wanaoshabikia serikali tatu, si kwa
kuimarisha Muungano ila wanajua kuwa ni kuuvunja Muungano. Wanachelea kuonyesha
dhamira yao ya kuuvunja Muungano bali wanashabikia Serikali tatu kwa kujua
dhamira yao itatimia.Watanzania tutafakari, tuchukue Hatua
Pamoja na Sababu nyingine nyingi unazoweza
kuzichambua juu ya kudumu au kutokudumu kwa Muungano wa Serikali tatu, nimeona
ni vyema nipitie maeneo ambayo binafsi nimeona yanaweza kuchochea kuunjwa kwa
Muungano wa serikali tatu.
Wengine wanajadili hoja ya gharama kubwa za
kuendesha serikali tatu, kwangu hili si hoja, naamini jambo lolote la kheri
linahitaji gharama na kama gharama zinaweza kuhimilika, hilo si tatizo.Maeneo
yanayoweza kuvunja muungano ni pamoja na:
(i)Uwezo uliosawa ki-uwiano katika kuchangia uendeshaji
wa Muungano
katika ibara ya 215 ya Rasimu, inazungumzia vyanzo
vya mapato ya serikali ya Jamhuri ya Muungano, na moja kati yake ni
"mchango kutoka kwa washirika wa Muungano" maana yake ni mchango toka
serikali ya Zanzibar na kutoka ya Tanzania bara.
Ni dhahiri muundo na mfumo wa uendeshaji wa serikali
ya Muungano kiasi kikubwa utategemea mchango huu ambao unategemea uchumi wa
serikali mbili zinazounda Muungano, katika mazingira halisi ya Tanzania kwa
kuzingatia rasilimali na mali zilizopo katika maeneo ya Muungano yaani Tanzania
Bara na Zanzibar ni dhahiri hayatawezesha mchango ulio sawa ki-uwiano katika
kuendesha serikali ya Muungano, hii itaifanya Serikali yenye mazingira mazuri
ya mali na rasilimali, kulazimika kuiendesha/kuichangia Serikali ya Jamhuri ya
Muungano na nyingine kushindwa kuchangia katika hali yoyote ile, mgongano wa
kiuchumi na kimaslahi hautaepukika.
Lakini pia katika mazingira ya umoja na mshikamano
uliopo sasa kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,
ambayo ushirikiano katika uendeshaji wa shughuli za kiserikali ni ule
usioepukika, (Gharama za uendeshaji na huduma katika serikali kwa mfano- Umeme
, Mafuta n.k.)
Hali hiyo katika serikali tatu, haitapata nafasi,
serikali itakayochangia zaidi tofauti na nyingine haitakubali hali hiyo. kwa
maana ya kiuchumi, pia upo uwezekano wa serikali itakayoshindwa kujiendesha au
hata kuchangia, kukopa nje katika mazingira ya kupoteza uhuru wake wa kiuchumi
na kiusalama.
Tukumbuke kuwa hadi sasa bado waptu nje ya nchi
wanaoitazama Zanzibar kisiwa chetu kizuri kama eneo lao, na bado wanandoto kuwa
siku moja watarudi Zanzibar kiutawala.Jee iwapo Zanzibar itashindwa kuchangia
katika serikali ya Muungano na kujiendesha kiuchumi ni nini kitatokea?
Ni lazima tukubali Watanzania kuwa uchumi wa nchi
hizi unatofautiana sana na kuishi kwetu katika Muungano ni kule kwa
kushirikiana kindugu kunakotokana pia na mfumo uliopo wa Muungano, vinginevyo
kwa muundo wa serikali tatu, zenye Marais watatu, hili linalofanyika sasa halina
nafasizi, ni wazi kuwa nafasi ya kudumu kwa Muungano itakuwa matatani.
(ii) Mgawanyo wa madaraka na mfumo wa kiutawala
Kwa mujibu wa Rasimu ya katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, kutakuwa na Marais watatu na serikali tatu na kwa mujibu
wa madaraka na mamlaka, kila Rais atakuwa na madaraka katika eneo lake la
utawala.
Katika mfumo wa miliki za mali na rasilimali na
utawala wa mali na rasilimali za nchi, kwa sehemu kubwa utakuwa katika mamlaka
za serikali ya Zanzibar kwa eneo la Zanzibar na Tanzania bara kwa yaliyo chini
ya Tanzania bara.
Hii ni pamoja na utawala wa serikali, serikali za
mitaa, tawala za mikoa na uteuzi wa mamlaka za utendaji, Ardhi, Maji, Barabara,
Huduma za kijamii ikiwemo Elimu, Afya n.k.
Kiutawala Rais wa Jamhuri ya Muungano hatakuwa na
eneo la utawala kirasilimali hasa rasilimali watu, Rais wa Muungano hatakuwa na
mamlaka na madaraka za kiutendaji, rasilimali na huduma za kijamii na za
maendeleo, mamlaka za kuagiza wala kukemea.
Katika hali hii utendaji kazi wa Rais wa Muungano
ambaye ndiye Kiongozi Mkuu, hautakuwa wenye mamlaka na madaraka. Uwepo wa
mgongano wa kimadaraka kati ya Jamhuri ya Muungano na serikali ya Zanzibar na
ile ya Tanzania bara hautazuilika. Na ni ukweli Rais wa Jamhuri ya Muungano
atakuwa Boya, ataelea hewani.
(iii) Mfumo wa utawala na Vyama vingi vya siasa
Kwa mujibu wa sura ya kwanza ya Ibara ya 1 (2) ya
Rasimu ya Katiba, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni shirikisho la kidemokrasia
linalofuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Kwa mtazamo wangu; katika mfumo wa kidemokrasia
unaozingatia vyama vingi vya siasa, ni dhahiri kuwa utawala na mamlaka za
utawala zinaweza kuwa katika matokeo ya mchanganyiko mkubwa wa Vyama mbalimbali
vya kisiasa, matokeo ya chaguzi za Rais, wabunge na Madiwani zinaweza kutoa
sura tofauti na katika maeneo tofauti.
Ni ukweli kuwa kila chama cha siasa, kina mfumo wake
na malengo yake, kisiasa tunaamini nchi ni moja, na wote tunajenga nyumba moja
kwa hiyo tofauti zetu za kisasa zisivuruge umoja na mshikamano wetu. Kwa
nadharai ya kisiasa, hii ni sahihi, lakini kihalisia ni dhana isiyotakiwa
kuiamini.
Upo uwezekano wa chaguzi katika serikali tatu,
zikapata vyama vinavyoongoza serikali kwa tofauti kwa kila eneo la utawala: kwa
mfano serikali ya Jamhuri ya Muungano ikaongozwa na chama kingine, Serikali ya
Zanzibar ikaongozwa na chama kingine na ile ya Tanzanzia Bara inkaongozwa pia
na chama kingine.
|
Kwa vyovyote vile mamlaka na madaraka yatawataka
Marais wa Bara na yule wa Zanzibar kutii mamlaka ya Rais wa Muungano. Ni rahisi
sana kusema hakuna tatizo lolote, wataongozwa na Katiba lakini yeyote anayejua
mwenendo wa siasa za Tanzania hivi sasa na matarajio za siasa za baadae
zinazoendelea hapa nchini, kwa tofauti ya sera, itikadi na mitazamo ya
kimaslahi katika vyama vyetu na jamii kwa ujumla.
Kwa mtazamo wa yeyote yule ni kuwa Muungano huu wa
serikali tatu, wenye Marais watatu ni ndoto kuamini kuwa utadumu katika
mazingira ya utawala wa vyama tofauti katika serikali zilizopo.
Tukumbuke Historia ya Muungano iliyoundwa kwa
utaratibu unaofanana na huu ambao umeishia kusambaratika kama vile Muungano wa
iliyokuwa Yugoslavia na Usavieti. Katika Yugoslavia, jimbo la Albania, ndilo
lilikuwa la kwanza kutaka kujitenga na hatimaye kulitumbukiza Taifa katika vita
vya wenyewe kwa wenyewe huku na majimbo mengine kama Serbia na Montenegro
yakidai kujitawala; hatima na matokeo ya Muungano huo ni Kuvunjika kwa Muungano
wao.
Zipo nchi nyingi zimesambaratika kutokana na
mifarakano midogo midogo ya kijamii: kumbuka Ethiopia, Eritrea, Somalia, Sudani
na Sudani ya Kusini n.k
"Mimi bado naamini kuwa suluhisho la kero la
Muungano siyo kuwa na serikali tatu, bado tunao uwezo na nafasi kubwa ya
mjadala zaidi.Tujiulize ni nchi gani duniani yenye Marais wa watatu, wenye
serikali tatu na wakakaa katika mfumo huu wa Muungano wakafanikiwa?
tujifunze kutoka kwa wenzetu walioungana duniani, Marekani imeundwa na
majimbo zaidi ya 52, lakini pamoja na majimbo hayo kuwa na nguvu na rasilimali
zote, bado Rais mwenye Nguvu ni mmoja tu.
Marekani haijagawa mamlaka, madaraka, usimazi,
utawala na maamuzi kwa mtu zaidi ya mmoja na ndio maana Taifa la Marekani
linaendelea kuwa imara sio ndani tu bali hata nje ya mipaka yake.
Watanzania wa Bara na Visiwani, kama tunadhamiria
kweli kujenga umoja wa kitaifa kwa mfumo wa Serikali tatu tungekuwa na Serikali
zenye muundo huu; Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenye Rais
aliyechaguliwa na Watanzania wote.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye Waziri Mkuu
mtendaji aliyechaguliwa na Bunge la Jamhuri Serikali ya Tanzania Bara
aliyechaguliwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Hili ndilo suluhisho pekee kwa wale wanaotaka
Serikali tatu, lakini nina hakika kwa sababu za tulio wengi kutawaliwa na homa
ya madaraka, wazo hili wengi watalipuuzia bila kujali kuwa ndilo suluhisho.
Tujiulize ni kweli tunautaka Muungano au tunasema
tunaimarisha Muungano kumbe dhamira zetu zinataka tuone Muungano unakufa kwa
vile eti kwa nini Zanzibar wana bendera yao, wana wimbo wao wa Taifa, wana
madai yao kila kukicha.
Watanzania wenzangu, Muungano unaondoka, chozi la
Baba wa Taifa litatushukia. Kuna tafsiri fulani nimesikia zikitolewa na wale
wanaotetea muundo wa serikali tatu, Jaji Warioba na kundi lake katika tafsiri
zao nimesikia wakimnukuu Baba wa Taifa kupendekeza serikali tatu.
Tuache kutafsiri na kupindisha maneno ya Baba wa
Taifa kwa kile tunachokitaka sisi, maana wapo wanaotumia maandishi mbalimbali
ya Baba wa Taifa, kumpandikizia tafsiri ya kutaka serikali tatu kwa matakwa
yao.
Baba wa Taifa amefariki akiamini na akiwa na msimamo
mmoja tu “Muungano wa Serikali mbili kuelekea serikali moja”. Mwanamapinduzi
Mzee Abeid Amani Karume amefariki akiamini juu ya Tanzania yenye Muungano wa
Serikali moja.
Mungu Ibariki Muungano wetu. Mungu ibariki Tanzania.
Makala hii imeandaliwa na Mwalimu Leonidas T. Gama
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.
haya ni Mawazo binafsi na Mapendekezo yangu!
No comments:
Post a Comment