Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
LIGI yetu ya Tanzania Bara
inavyopambwa, hasa katika maandalizi yake, utasema ni nzuri na yenye mvuto
mkubwa hapa nchini. Utaona tambo za kila aina.
Leodgar Tenga, Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF).
Utaona jinsi wachezaji
waliosajiliwa kwa ligi hiyo wanavyopambwa katika vyombo vya habari wakiona wao
ndio kila kitu katika soka la Tanzania.
Lakini si ukweli huo. Katika
miaka nenda rudi, Tanzania tumekuwa soka la kawaida kabisa, japo si sawa na
wenzetu wa Tanzania Visiwani, yani Zanzibar.
Sisi soka letu zaidi lipo
katika kurasa za magazeti. Ndio maana siku zote tunazalisha wachezaji wa
kawaida na wasiokuwa na lolote katika soka la Tanzania.
Tuna wachezaji wenye majina
makubwa akiwamo Mrisho Ngassa, Jerry Tegete, Kelvin Yondan, Juma Kaseja, Haruna
Moshi ‘Boban’ na wengineo ambao miguu yao haijaweza kulifanya soka letu lipige
hatua.
Japo mapungufu ya wachezaji
wetu wa Tanzania mara kadhaa yanasababishwa na mfumo wa soka letu, kutoka
katika vichwa vya viongozi wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), ila kujitambua
nako kwa vijana hawa kunahitajika.
Hapo ndipo ninaposhindwa
kuvumilia. Ligi ya Tanzania Bara inaanza Agosti 24 mwaka huu kwa viwanja kadhaa
kuwaka moto kwa timu zinazoshiriki ligi hiyo kuingia uwanjani.
Timu hizo zinawania taji la
Vodacom linaloshikiliwa na Yanga iliyotwaa mwaka msimu uliomalizika ambapo
tulishuhudia bingwa mtetezi Simba, akiangukia pua, huku akikosa hata nafasi ya
pili.
Bingwa alikuwa ni Yanga ambayo
pia imepata nafasi ya kushiriki michuano ya Kimataifa, Ligi ya Mabingwa Afrika,
huku Azam iliyoshika nafasi ya pili ikikata tiketi ya kucheza mashindano ya
Kombe la Shirikisho.
Pamoja na kunyakua nafasi hiyo
kwa Yanga au Simba iliyoshindwa kulitetea, ila bado ligi yetu hatuoni ladha
halisi na ushindani unaoweza kunyanyua soka letu.
Mara kadhaa ligi huwa tamu
zaidi zinapokutana timu za kawaidam, yani Coastal Union ya mjini Tanga, Ruvu
Shooting, ila si kwa mechi ya Simba na Yanga.
Zaidi utamu zaidi hukolea pale
Yanga au Simba inapokutana na Azam au Coastal Union, ingawa wakati mwingine
nguvu ya umma, yani ushabiki huleta mkanganyiko.
Siwezi Kuvumilia hata kidogo.
Hivyo kuna kila sababu ya timu zetu za Tanzania kucheza soka la uhakika ili
ligi yao iwe na nguvu kwa muda wote.
Tunataka mashabiki wao
wafurahie burudani ya soka, ukizingatia kuwa wanalipa viingilio vyao halali kwa
ajili ya kuunga mkono sekta ya mpira wa miguu Tanzania.
Timu ya Yanga ambayo ndio
bingwa mtetezi, lazima ijuwe kuwa inaingia uwanjani kucheza soka la uhakika na sio
kutumia mtaji wa wadau wao kuvuruga utaratibu.
Ni mara kadhaa sasa timu za
Tanzania, hasa Simba na Yanga zinapoingizwa kwenye timu zinazopenda kutumia
mtaji wao wanachama kununua mechi.
Na ndio timu hizo pia zinatajwa
kuhujumu usajili wa wachezaji mara kwa mara. Simba ina uwezo wa kusajili
mchezaji yoyote hapa Tanzania, ila baadaye inashindwa kuwatumia na kutumbukia
katika shimo la upangaji wa matokeo.
Hii si njia nzuri ya kukuza na
kuendeleza soka letu, hivyo lazima tuwe makini kama tunahitaji kuwa makini.
Mpira ni ajira inayowapa utajiri watu wengi.
Dakika 90 tu za mchezo kati ya
Yanga na Simba zinaingiza mamilioni ya shilingi. Usajili mmoja tu kwa Dunia ya
leo, unamfanya nyota husika achote fedha lukuki.
Ukiacha wachezaji wa Tanzania
wanaosajiliwa kwa fedha za kununua soda, ingawa baadaye hudaiwa wamevuna fedha
nyingi, wenzao nje wanatembelea kwenye utajiri wa aina yake.
Hii ni kwasababu wameweza kuwa
makini, huku wakitumia muda wao mwingi kufanya juhudi zao binafsi. Tanzania
inaweza kufikia hatua hiyo, ila kwa kuendelea kujenga msingi imara wa soka
letu, hasa kwa kuifanya ligi iwe na nguvu.
Timu zishinde kihalali na sio
kununua mechi au wachezaji kucheza chini ya kiwango kwasababu mbalimbali,
yakiwmao mapenzi ya timu wanazokutana nazo au kupewa ahadi ya chochote kutoka
kwa wanazi wa Simba na Yanga.
Tukifanya hivyo, ligi yetu
itakuwa na nguvu nje na ndani ya uwanja, hivyo kuwa mtaji pekee unaoweza kuongeza
thamaani ya wachezaji wa Tanzania na kuwa thamani yao ya kuonekana duniani kama wanavyotamba wengine.
Tukutane tena wiki ijayo.
0712 053949
No comments:
Post a Comment