Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
TANZANIA ni miongoni mwa nchi ambazo watu wake wanaishi
maisha ya kubangaiza, huku wakisumbuliwa pia na changamoto za ukosefu wa nyumba
za kuishi.
Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank, Dk Charles Kimei akizungumza katika uzinduzi wa huduma ya 'Jijenge' inayohusiana na mambo ya mikopo ya nyumba kwa wateja wao.
Katika jiji la Dar es Salaam, tunashuhudia wakazi wake wengi
wakiishi katika nyumba za kupanga, tena zile zisizokuwa na ubora.
Mtu anaishi kwa mashaka wakati wote, hasa pale kinapoingia
kipindi cha mvua na kusababisha maji kujaa kwenye nyumba zao.
Hii ni kwasababu Mtanzania wa kawaida kuweza kumiliki nyumba
kunahitaji mihangaiko ya kutosha, huku baadhi yao wakilazimika kudokoa kwenye maeneo
yao ya kazi ili wafanikishe ndoto zao.
Wakati hayo yakiendelea kuwa kero kwa Watanzania, benki ya
CRDB imekuja kufuta changamoto hizo baada ya kuzindua huduma ya kuwakopesha
wateja wao nyumba bora za kuishi.
Mkopo huo unaojulikana kama (Jijenge) utakuwa majibu tosha
kwa wanaohangaika na maisha yao, ukizingatia kuwa sasa kila mwenye ajira yake
anayelipwa kiasi cha Sh 200,000 ana sifa za kukopeshwa nyumba na benki ya CRDB.
Katika mazungumzo yaliyofanyika wiki iliyopita, Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB Tanzania, Dk Charles
Kimei, anasema kuwa wameamua kuanzisha huduma hiyo ili kuwapatia maisha bora
Watanzania wote.
Anasema kuwa baada ya kuwaza namna gani ya kuchangia maisha
bora kwa Watanzania, ndipo benki yao ilipobuni wazo hilo la aina yake.
“Watu wanaishi maisha magumu na hawana matumaini ya kuweza
kuishi kwenye nyumba zao, hivyo kwa kuchukua mkopo wa CRDB basi kila kitu
kinawezekana.
“Tumeweka utaratibu rahisi mno kwa wafanyakazi kuanzia
kipato cha laki mbili 200,000 kwa mwezi ambapo tunaamini tumejibu vilio vyao,”
alisema.
Tanzania ina upungufu wa nyumba milioni tatu, huku kiasi
kidogo kilichokuwapo kuleta joto kali kwa wananchi.
Ongezeko la nyumba laki 200,000 kwa mwaka halisaidii
kupunguza msoto wa upatikanaji wa nyumbaa bora kwa Watanzania wote.
Hakuna masharti magumu ya kuweza kupewa mkopo huo
uliogawanyika katika makundi matatu muhimu.
Kuna wale wanaokuwa tayari kuchukua mkopo wa kujenga nyumba
zao, kununua zilizojengwa au wale wanaotaka kuboresha nyumba zao.
“Kila mkopo umewekewa utaratibu wake, huku mkopaji akiishi
bila presha maana atapewa miaka 20 hadi kukaamilisha kumaliza deni lake.
“CRDB tunachoweza kufanya ni kumpatia mkopo anaotaka mteja
wetu, ila hati yake itabaki katika mikono yetu hadi atakapomaliza kulipa, huku
marejesho yake yakiwa madogo kupita kiasi,” alisema.
Anasema kuwa wananchi wengi wameshindwa kumiliki nyumba
kwasababu ya kupanda kwa gharama ya kumiliki ardhi, kupanda kwa gharama za
ujenzia sanjari na vifaa vyake, ikiwamo saruji, nondo na vinginevyo.
Changamoto hizo zinasababisha pia kuwafanya watu wengi
waaishi kwenye nyumba zisizomalizika (mahame) hali inayoharibu mwonekano wa
jiji katika macho ya wageni wanaokuja kutembelea Tanzania.
Dk Kimei anasema mara kadhaa Watanzania wamekuwa wakiishi
kwa kujenga kutokana na akiba wanazojiwekea, ukiwa ni mfumo uliopitwa na
wakati, ukizingatia kuwa Dunia ya leo inahitaji mipango na ubunifu wa hali ya juu,
hasa ukopaji wa nyumba.
Watu hao wanapokopa katika mashirika ya fedha na benki
kunafanya waishi kwenye nyumba imara na zenye ubora, ambapo marejesho yake
hayaonekani kuwa magumu tofauti na zamani.
Kwa wale wanaoishi kwenye za kupanga huku wakilipa zaidi ya
100,000 kwa mwezi, ni ajabu kama watashindwa kukopa nyumba ili waondokane
katika matatizo yao ya kuishi kwa kubahatisha.
Mtu akihamishwa, anaweza kuuza nyumba yake na kuendelea na
maisha yake sehemu nyingine ambapo pia fedha hizo anaweza kununua jingo jingine
sehemu anakoelekea.
“Haya ni mambo yasiyohitaji gharama kubwa katika mfumo wa
maisha ya sasa, hivyo kuna kila sababu ya Watanzania wakiwamo wateja wetu wa
CRDB kushawishika katika utaratibu huu,” alisema Kimei katika uzinduzi huo wa
huduma hiyo.
Dk Kimei anasema mikopo hiyo ya ‘Jijenge’ ikitumiwa vizuri, watu
wataishi kwenye nyumba bora na zenye furaha pamoja na familia zao, huku
wakipata huduma zote za jamii kama vile umeme, maji na barabara.
Huduma hiyo ya Jijenge inawahusu watu wote, wakiwamo wafanyakazi
walioajiriwa kwenye sekta zote, sambamba na wale waliojiajiri wenyewe.
Kwa mujibu wa wataalamu wa mambo ya makazi, soko la mikopo
ya nyumba kwa jiji la Dar es Salaam (Mortgage Business), linakadiriwa kufikia
Shilingi Bilioni 480 kutokana na takwimu za mwaka 2012.
Aidha, Mtanzania wa kawaida ili aweze kumiliki nyumba yake
mwenyewe inamchukua miaka 10, huku chanzo cha ukopaji kwa kutumia dhamana ya
kitu kisichohamishika, ambacho mara nyingi ni nyumba au kiwanja ikiendelea kuwa
mwiba mkali.
Dk Kimei anasema kwamba kiwango cha mwisho cha ukopaji
katika benki yao kwa ajili ya kukopeshwa nyumba ni Milioni 500.
Malengo na sifa ya mikopo ni
mshahara, michango ya pensheni (sio zaidi ya asilimia 50), mapato ya kodi ya
pango, huku matawi yote ya benki ya CRDB yakiweza kumhudumia mteja juu ya
huduma hiyo ya Jijenge ya inayohusika na ukopaji wa nyumba.
Mahitaji muhimu kwa mkopaji
ambaye ni mjasiriamali ni pamoja na historia pamoja na maelezo ya mteja juu ya
biashara yake, taarifa ya fedha iliyokaguliwa na mtaalamu (auditor) kwa kipindi
cha miaka mitatu ya karibuni na makadirio ya mtiririko wa fedha.
Mizania na ripoti ya hesabu za
faida, hasara za miaka mitatu, pamoja na taarifa ya hesabu za benki kwa miaka
12 kutoka benki ya CRDB na nyinginezo kama zipo, bila kusahau maelezo na
viambatanisho vyote juu ya mikopo kutoka benki zote.
Mteja ambaye ni mwajiriwa
anatakiwa awe na stakabadhi ya malipo yake ya mshahara kwa kipindi cha miezi
sita ya karibuni, taarifa kutoka benki ambayo mshahara wake ulipopitia, barua
kutoka kwa mwajiri yenye maelekezo ya kutosha juu ya aina ya mkataba wake, umri
wake na taarifa ya mfuko wa fao la uzeeni, mshahara na posho zake kwa ujumla.
Kuanzishwa kwa huduma hiyo, ni
wazi Watanzania watakuwa wamejikomboa katika changamoto ya ukosefu ya nyumba
bora za kuishi.
No comments:
Post a Comment