Na Kambi Mbwana, Dar es
Salaam
NI ngumu kuwa na familia
bora na yenye kila jema, kama wazazi hawajitambui. Mzazi anaposhindwa kufahamu
mbinu za kuiweka familia yake, ni dhahiri ameamua kuyumba na kuwafanya watoto
wake waishi kama ndege.
Rais wa TFF, Leodgar Tenga
Kama hivyo ndivyo, tusuburi
matusi kutoka kwa wanajamii. Yapo maneno mengi ya kufanana na hayo, huku muktadha
wote ukihusiana na Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Leodgar Tenga.
Katika mpira wa miguu,
Tenga ni miongoni mwa wadau wenye heshima kubwa. Kila mtu aliheshimu utendaji
wake.
Wengi wanatamani rais
huyo wa TFF ajiuzulu ili kuokoa soka letu, maana anachofanya ni kujipaka
kinyesi usoni mwake.
Badala ya kujenga, anabomoa.
Watanzania hatufahamu kwa kupita ili tutokee peupe, hasa migororo inayochipua
na kukosa mbinu zenye tija, kama vile ligi bora, timu za Taifa zenye ushindi na
kuendeleza soka la vijana ambao ndio msingi wa maendeleo ya mpira wa miguu
duniani.
Tenga anachofanya ni
kuweka njia ya maswahiba wake, bila kujua kuwa anachafuka mtaani. Ule umahiri
wake unaotajwa kila kona, unapukutika kama barafu juani.
Hali inavyoonekana,
Uchaguzi wa TFF kufanyika mwaka huu ni ndoto, ukizingatia kuwa hakuna mipango,
ingawa ulikuja ujumbe kutoka Shirikisho la Kimataifa (FIFA) kwa ajili ya
kukutana na wadau wa michezo, wakiwamo wale walioenguliwa Michael Wambura,
Jamal Malinzi na wengineo.
Watu wanajiuliza, hivi
kweli heshima ya Tenga imetoweka kiasi cha kushindwa kusimamia Uchaguzi hadi
waje Wazungu? Wao ndio nani? Je, Tenga aliwekwa na Wazungu madarakani?
Hata Mkutano wa Dharula
uliyoitishwa na kufanyika Julai 13 mwaka huu kwa ajili ya kurekebisha Katiba
yao, haukuwa na jipya zaidi ya kuleta malumbano zaidi.
Hata serikali ilipinga
kupitia kwa Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla aliyewakosoa
TFF, akisema sheria hazijafuatwa, hasa wajumbe theluthi mbili kupiga kura za
ndio.
Kauli ya Makalla ilikuwa
tata kwa TFF ambapo Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, yeye aliunga mkono na
kusema wanasubiri baraka ya Msajili wa Vyama vya Michezo.
Katibu Mkuu wa
kilichokuwa Chama Cha Soka nchini (FAT) sasa TFF, Michael Wambura, yeye aliungana
na serikali, akisema kuwa Katiba ya TFF ya 2012 ilifutwa
na MsajIli wa Vyama vya Michezo na vilabu kwa kuwa ilibadilishwa kinyume cha
sheria (BMT) pamoja na Katiba ya TFF
ibara ya 30 kwa kutumia njia ya waraka badala ya Mkutano Mkuu.
Kwa sababu hiyo, Katiba halali kisheria
inayotambulika ni ile ya 2006 na mabadiliko yake. Hali ya utata ilizidi kupamba
moto, maana FIFA na Serikali kupitia
wizara yenye dhamana na michezo iliiagiza TFF iitishe Mkutano Mkuu ili ifanye
mabadiliko ya Katiba.
Hili lilifuatwa na TFF, japo bado wadau
wanaendelea kupinga, wakisema kuwa mchakato mzima unafanywa kiubabaishaji,
kutaka kuwekana katika nafasi za uongozi.
Haya yote yaliibuka pale TFF ilipojaribu kuwaengua
wadau mashuhuli katika mpira wa miguu. TFF ilimuengua Wambura, watu wakajua
labda ni lile sakata lake la kupeleka mambo ya soka mahakamani.
Likatokea pia kwa Malinzi. Kwa kupitia Kamati ya
Uchaguzi na Nidhamu, ilimtupa tena aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Urais wa TFF,
Malinzi na kuzua taharuki.
Hata wale waliokuwa kimya waliona uozo wa TFF.
Waliona hata wale vipofu wasiojua mchanganuo wa sheria na Katiba ya Shirikisho
hilo linaloendeshwa kwa rimoti kwa sasa.
Haya ni matatizo makubwa. Udhaifu wa Tenga katika
miaka miwili hii, ikiwa ni harakati zake za kutaka kumuachia mtu anayefanana
naye.
Kwa mujibu wa sheria, msajili husajili mabadiliko
yoyote ya Chama kilichosajiliwa chini ya Sheria ya BMT kwa kuzingatia Sheria NA 12 ya 1967 na marekebisho yake NA 6
ya 1971 ya Baraza la Taifa la Michezo pamoja na
Kanuni za Baraza la Michezo la Taifa
na Kanuni za Usajili NA 422
za1999.
Katiba pia ni nyaraka ya kisheria hivyo chombo
chenye mamlaka kisheria hapa Tanzania ya kuitafsiri ni Mahakama pale pande
mbili zinapotofautiana juu ya tafsiri ya Katiba.
Ndio maana kwa kuzingatia haya, hata msajili wa
vyama vya michezo amechelewa mno kubariki mkutano huo wa TFF ili chachu ya
kuelekea kwenye Uchaguzi huo.
Yote haya yamekuwa
yakisababishwa na udhaifu wa Rais Tenga, ukizingatia kuwa ndio kila kitu. Tenga
akishindwa kusimamia masuala ya soka, hakuna anayeweza kuweka mambo sawa.
Hili ni tatizo kubwa, hivyo Tenga anapaswa kuona
namna gani heshima yake iliyojengeka katika jamii inaendelea kuchanua. Huo ndio
ukweli. Vinginevyo, hakuna kiongozi atakayechekwa zaidi ya Tenga.
Akiwa Rais wa TFF, Tenga amekuwa akipata bahati ya
kuungwa mkono na kila mtu Tanzania. Wananchi wamekuwa wakiingia kwa wingi
katika viwanja vya soka kuangalia mechi za timu ya Taifa au klabu.
Mamilioni ya shilingi yanapatikana. Wadau na
makampuni yanaendelea kumwaga fedha za kutosha. Tenga anataka nini tena? Kwa
kutumia wadau hawa tu, soka la Tanzania lingechanja mbuga.
Lakini hakuna kitu. Ni malumbano usiku na mchana.
Watu wamekuwa wakitoana macho mchana kweupe. Wenyewe wanasema
wanashughulikiana. Siasa zimeingizwa katika masuala muhimu ya mpira wa miguu.
Makalla akiwa kama Naibu Waziri anaona haiwezekani
Tenga na TFF yake wafanye mambo bila kufuata sheria. Wakati yeye anaaamini
hilo, TFF wao wanacheka wakiangalia tamko la FIFA, kuwa serikali haipaswi
kuingilia masuala ya soka. Tamko hili linawabeba. Wataendelea kufanya ‘madudu’
yao miaka nenda rudi.
Nani
wa kuwakosoa? Huu ni ubabaishaji wa aina yake. Hatuwezi kusonga mbele kamwe.
Soka la Tanzania litabaki kama lilivyo kama mmea unaoshambuliwa na wadudu.
Pamoja
na yote hayo, bado lawama zitabaki kwa Tenga na viongozi wenzake, akiwamo
Sunday Kayuni, Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, ambaye hana anayempenda.
Taasisi
za serikali zinazochukiwa kwa sasa, TFF inaongoza. Japo wakiambiwa hili
watakataa. Ni wakati wao kujirekebisha kama wanahitaji kunyanyua soka la
Tanzania.
Waache
ubabaishaji. Tenga anapaswa kukumbuka namna gani Watanzania walivyompenda
kwenye nafasi hiyo. Leo amesahau? Nani amemroga Tenga hadi kuchafua historia
yake?
Kuna
kila sababu ya kufahamu namna ya kulikomboa soka letu. Kila mtu awe na utu
pamoja na mapenzi mema na masuala ya michezo, hususan mpira wa miguu unaopendwa
duniani kote.
0712
053949
Mwisho
No comments:
Post a Comment