Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
IDDI Mubarak msomaji wangu mpendwa, huku
nikiamini kuwa tutaendelea kuwa pamoja siku ya leo, kama ilivyokuwa kawaida
yetu ya kukutana kwenye kona hii kujadili mambo mbalimbali ya uhusiano na maisha.
Raha kwenda mbele
Nakushukuru kama wewe ni miongoni mwa wasomaji
wa ukurasa huu, unaokujia kila Jumamosi, huku wiki hii ikiangukia katika
Sikukuu ya Idd, baada ya kipindi cha mwezi mzima ndani ya mfungo wa Ramadhan.
Ndugu msomaji wangu mpendwa, kuna vitendo vinavyoumiza
kichwa, hivi ni kuona baadhi ya watu wanajenga ukaribu wa kupitiliza kwa
wapenzi wao wa zamani kiasi cha kuzua hofu kwa wenzi wao.
Ukiacha wale waliopata mtoto katika kipindi cha
uhusiano, au wanandoa walioachana huku wakiwa na mtoto, hao wanaruhusiwa
kuwasiliana mara kwa mara kulea mtoto. Ubaya upo kwa wale walioachana, lakini
muda wote wapo katika mawasiliano makubwa, huku wakiwa hawana chochote
kinachowaunganisha.
Wakati mwingine hualikana chakula cha mchana au
usiku, muda mwingine huchukuana na kwenda katika majumba ya starehe, kama vile
bado wapo kwenye mapenzi kama ilivyokuwa awali.
Hii ni mbaya sana, maana kama mlishaachana huo
ukaribu uliojenga kwa sasa ni ishara gani? Ndio kusema bado mnapendana? Kama
hivyo ndivyo, kwanini mliachana?
Je, huoni sasa ni wakati wako kurudiana na huyo
mpenzi wako wa zamani, ili kumuondolea jakamoyo mpenzi wako mpya? Haya ni
maswali ambayo tunapaswa kujiuliza kila mara.
Kuna baadhi ya watu ambao baada ya kuachana na
wapenzi wao wa zamani, hushindwa kujizuia na kutafuta mahala kwa kujiegemeza,
ili watulize majonzi ya kuachwa.
Kwa bahati nzuri wakapata watu wanaowapenda kwa
dhati, ambao wamekuwa wakiwajali kwa kila wanachokitaka katika suala zima la
mapenzi wanayoyapata, wanatembea kifua mbele wakithaminiwa na wapenzi wao
wapya.
Lakini kutokana na ujinga, anajikuta anaingia
tena katika urafiki na yule aliyeachana naye kipindi cha nyuma, sasa unabaki
unashangaa chanzo na mwelekeo wake.
Si kila mtu anahitaji kuona mchumba wake
aliyekuwa naye ana ukaribu na mpenzi wake wa zamani, hakuna anayependa suala
hilo. Ni wazi wapenzi wa zamani wanapokuwa na ukaribu wa kupitiliza, suala la
ngono kwao ni lazima.
Kama watafanya ngono, si kweli kama wataogopana
kiasi cha kuweza kujikinga katika suala hilo, zaidi wataingiliana kimwili bila
tahadhari yoyote, matokeo yake ni kupeana maradhi.
Hapo ndipo utakuta cheni kubwa ya maambukizi,
kwani wakishaambukizana maradhi huwapelekea wapenzi wao hao wapya, ukiwa ni
mtindo usiokuwa na mashiko hata kidogo. Ni jukumu letu kujua hakuna ulazima wa
kudumisha ukaribu na wapenzi wetu wa zamani.
Watu wabakie kulea watoto, kama katika hatua ya
mapenzi yao walibahatika kupata zawadi hizo kutoka kwa Mungu. Na kama unaona
kuna ulazima wa kuwa na ukaribu na mtu wako wa zamani, basi jaribuni kuzungumza
namna ya kurudiana, ili usilete mkanganyiko kwa wengine.
Kuachana kupo, lakini pia kurudiana si jambo
geni duniani, ukiona huwezi kukaa bila kumuona mpenzi wako wa zamani, kumpigia
simu au kuwasiliana naye muda wowote, mpigie magoti mrudiane.
Kinyume na hapo, utasababisha maswali mengi
kutoka ndani ya moyo wako na jamii kwa ujumla, utampa presha uliyekuwa naye,
maana anaona ujinga wako, kimekushinda mwenyewe mwanzo na sasa unajirudisha
kienyeji.
Katika jamii wapo watu wengi wenye tabia hizo, wanaachana
na wapenzi wao lakini muda wote wapo pamoja. Baadaye wanaanzisha tena uhusiano
na kuendelea na uchafu wao.
Wanasababisha presha kwa wengine, hivyo hakuna
haja ya kujinyima kama kweli waliachana kwa bahati mbaya, basi rudisheni tena
penzi lenu ili watu wajue moja, kuliko kusumbua wenzenu.
Huo ndio ukweli, maana wengi wamekuwa wakiwaza
na kuumiza kichwa kuona waliokuwa nao, wana ukaribu wa kupitiliza na wapenzi
wao wa zamani, hivyo kuwachanganya kisaikolojia.
Nimeandika makala haya kama majibu ya baadhi ya
wasomaji wangu, waliohoji uhalali wa wapenzi wao, wachumba wao kuwa na ukaribu
na wapenzi wa zamani, tena wengineo wakiandikiana hadi meseji za mapenzi.
Hii sio haki na kuna ulazima wa jamii, kutambua
huo ni mpango mbaya na unaweza kudhalilisha watu wengine.
Tukutane wiki ijayo.
+255 712 053949
No comments:
Post a Comment