Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Chadema, Freeman Mbowe.
MUHTASARI
Ili kukabiliana na vitendo vya fujo
vinavyofanywa na vijana wa CCM dhidi ya wagombea, Wanachama na viongozi wa CHADEMA,
Kamati Kuu imeagiza kwamba kitengo cha ulinzi cha Chama “Red Brigade” kiimarishwe zaidi kwa kuhakikisha
kuwa vijana wote wa Red Brigade Nchi nzima wanapewa mafunzo maalum ya UKAKAMAVU
yatakayoandaliwa katika Makambi maalum katika mikoa yote.
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MAAMUZI YA
KIKAO CHA KAMATI KUU YA CHAMA KILICHOFANYIKA TAREHE 06-07/07/2013 KATIKA HOTEL
YA BLUE PEARL, DAR ES SALAAM.
Kamati kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo ilikutana katika Kikao cha
dharura kuanzia tarehe 06-07/07/2013 katika Hotel ya Blue Pearl Dar es salaam
kujadili pamoja na mambo mengine Rasimu ya Katiba mpya na hali ya Siasa nchini.
Kamati kuu imejadili na kuyatolea maamuzi mambo mbalimbali kama ifuatavyo:
1:0. Hali ya Siasa Nchini.
Kamati kuu imepokea taarifa ya hali ya siasa nchini na kuzingatia mambo
yafuatayo:
a) Shambulio la Bomu Arusha.
ü Kamati Kuu
imesikitishwa na kulaani kwa nguvu zote tukio la Bomu Arusha lililosababisha
watu wanne kuuwawa na zaidi ya watu 70 wengine kujeruhiwa vibaya.
ü Kamati Kuu
imeridhika kwamba shambulio hilo lililenga kuwaua viongozi wakuu wa CHADEMA
akiwamo Mwenyekiti wa Taifa Mheshimiwa Freeman A. Mbowe na Mbunge wa Jimbo la
Arusha Mjini na Mjumbe wa Kamati Kuu, Mheshimiwa Godbless J. Lema na viongozi
na wanachama wengine wa CHADEMA waliohudhuria Mkutano wa kufunga kampeni za
udiwani katika Jiji la Arusha pamoja na kuvuruga Uchaguzi huo na kuinyima
CHADEMA ushindi mkubwa;
ü Kamati Kuu
imeridhika kwamba ushahidi uliopo wa vielelezo na wa mashuhuda wa shambulio
unaonyesha ushiriki wa moja kwa moja wa Jeshi la Polisi katika shambulio hilo;
ü Kamati Kuu
imefadhaishwa na kauli ya Serikali bungeni iliyolenga kulikosha Jeshi la Polisi
kwa kuhusika kwake na shambulio hilo dhidi ya CHADEMA na wananchi wa Jiji la
Arusha na kuilaumu CHADEMA wakati CHADEMA ndio mhanga wa shambulio hilo;
ü Kamati Kuu
imeshangazwa na kitendo cha Serikali kupuuza maafa yaliyowafika wananchi wa
Arusha kwa kushindwa kushiriki katika mazishi ya wahanga wa mauaji ya Soweto na
kuwashambulia kwa mabomu ya machozi, vipigo na maji ya sumu waombolezaji
waliokusanyika kuwaaga marehemu waliouawa kwenye shambulio;
ü Kamati Kuu
imesikitishwa na Rais Kikwete kuendelea kukaa kimya juu ya shambulio la Arusha
na kushindwa kwake kuunda Tume huru ya Kimahakama kuchunguza kwa uwazi
shambulio hilo. Aidha, Kamati Kuu inaamini kwamba ukimya huu wa Rais Kikwete na
kushindwa kwake hata kuwatembelea wafiwa na wahanga wengine wa shambulio hilo
ni ushahidi mwingine wa kuhusika kwa vyombo vya ulinzi na usalama vya Serikali
katika kupanga na kutekeleza shambulio la Arusha;
ü Kamati Kuu
imefadhaishwa na kitendo cha Bunge la Jamhuri ya Muungano kuendelea na vikao
vya Bunge kama kawaida; kukataa kutoa mchango wowote kwa wahanga na kushindwa
kupeleka ujumbe wa Bunge kuwatembelea na kuwafariji wahanga na waathirika wa
shambulio kinyume na utaratibu uliozoeleka wa Bunge kutambua na kushiriki
katika majanga na misiba ya aina hii.
Kamati Kuu inautaka uongozi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano uwaeleze Watanzania
kama maafa ya shambulio la Arusha yalikuwa na tofauti yoyote na maafa ya
shambulio la bomu la Olasiti, au na maafa ya mabomu ya Gongo la Mboto, ajali ya
MV Skargit au maafa mengine yaliyosababisha Bunge la Jamhuri kuahirisha
shughuli zake, kutoa michango kwa waathirika pamoja na kupeleka ujumbe wa Bunge
kuwafariji wafiwa na wahanga wa matukio hayo;
Kutokana na maelezo hayo hapo juu Kamati kuu imeazimia kuwa:
• Iwapo Rais ataendeleza msimamo wa kutokuunda tume huru ya kimahakama,
Ushahidi uliopo juu ya tukio la kurushwa Bomu Arusha utawekwa wazi muda
utakapofika kwa wananchi wa Tanzania; vyama na mashirika ya kiraia ya haki za
binadamu hapa nchini na ya nje ya nchi; ofisi za kibalozi za mataifa rafiki na
Tanzania pamoja na jumuiya ya kimataifa ili yaishinikize Serikali kuunda Tume
huru ya Kimahakama kuchunguza shambulio hilo na matukio mengine ya mauaji yenye
sura ya kisiasa ambayo yamehusishwa na Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya
usalama vya Serikali au vya Chama cha Mapinduzi;
2:0. Hali ya Wananchi wa Mtwara.
Kamati kuu imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa juu ya unyanyasaji, utesaji,
ubakaji na uonevu wanaofanyiwa wananchi wa Mtwara hivi sasa na vyombo vya dola
huku serikali ikikaa kimya juu ya jambo hili bila kukemea. Kamati kuu imejadili
kwa kina namna wananchi wa Mtwara wanavyofanyiwa na vyombo vya dola na kufikia
maazimio yafuatayo;
ü Vyombo vya dola
vitimize wajibu wake wa kulinda amani na mali ya raia na siyo kuwatesa na
kuwapiga wananchi kwa kuwasababishia vifo kinyume na Haki za Binadamu.
ü Serikali iwasikilize
wananchi wa Mtwara na siyo kutumia ubabe, unyanyasaji, uonevu na mateso kama
mbinu za kuhalalisha kukubalika kwake kwa wananchi.
ü Rais Kikwete
alitangazie taifa “hali ya hatari” kwa mkoa wa Mtwara kama anaona kuwa Mtwara
ni hatari kwa kiasi hicho cha kulitumia JWTZ kuzunguka mitaani na silaha za
kijeshi ili taifa liweze kujua,Aidha kama jeshi la polisi limeshindwa kutimiza
majukumu yake kwa mujibu wa sheria atangaze kulivunja jeshi hilo mara moja.
ü Serikali iunde tume
huru ya kuchunguza matukio ya mauaji,ubakaji,utesaji na ukiukwaji wa haki za
binadamu yaliyofanywa na vyombo vya dola na waathirika wote waweze kufidiwa kwa
mujibu wa sheria.
3:0. Kauli ya Waziri Mkuu.
Kamati Kuu imejadili kwa kina kauli ya Waziri Mkuu Bungeni kwamba ni sahihi kwa
Jeshi la Polisi nchini kuwapiga Wananchi wote wanaotumia haki zao za Kikatiba
kupinga sera au maamuzi ya Serikali. Kamati Kuu imeazimia kuwa:
ü Kauli ya Waziri Mkuu
imekiuka Katiba na sheria za nchi yetu zinazokataza Jeshi la Polisi kutumia
nguvu dhidi ya raia wasiokuwa na silaha na ambao wanatumia haki zao za kikatiba
kufanya maandamano;
ü Kamati Kuu inaamini
kwamba kauli ya Waziri Mkuu inatoa Baraka kwa Jeshi la Polisi kuendeleza
vitendo vya ukatili na mauaji dhidi ya wananchi ambayo yamelifanya Jeshi la
Polisi la Tanzania kutangazwa kuwa moja ya majeshi katili ya polisi katika
Afrika Mashariki;
ü Kamati Kuu inaungana
na wananchi, taasisi na mashirika ya kitaifa na kimataifa ambayo yamelaani
vikali kauli hiyo ya Waziri Mkuu na inawataka wananchi, taasisi na mashirika
hayo kuendelea kumlaani vikali Waziri Mkuu kwa kauli hiyo;
ü Kamati Kuu inaamini
kwamba Waziri Mkuu amepoteza sifa za kuendelea kuwa Waziri Mkuu na inaungana na
wananchi na taasisi ambazo zimedai Waziri Mkuu awajibike au awajibishwe kutokana
na kauli yake hiyo. Aidha, Kamati Kuu inawaelekeza Wabunge wote wa CHADEMA
washirikiane na Wabunge wengine wote wenye mapenzi mema na nchi hii na ambao
wanaamini katika utawala wa sheria waanzishe mchakato wa kumpigia kura ya
kutokuwa na Imani Waziri Mkuu kupitia Bunge;
ü Kamati Kuu imewataka
Jeshi la Polisi kama sehemu ya jamii ya watanzania kupuuza kauli ya Waziri Mkuu
katika utekelezaji wa kazi zao kwa kuwa kauli hiyo ni ya uvunjifu wa Katiba na
Sheria na inachochea uvunjifu wa amani.
4:0. Uchaguzi wa Madiwani.
Kamati Kuu imepokea taarifa kuhusu ushiriki wa CHADEMA katika Uchaguzi wa
Madiwani uliofanyika tarehe 16/06/2013 katika kata 22.
ü Kamati Kuu
imeipongeza Sekretarieti na uongozi wa Kanda mbalimbali za CHADEMA kwa
maandalizi mazuri katika Uchagzuzi huo uliosababisha CHADEMA kuwapokonya CCM
ushindi katika kata 4 ilizokuwa imeshinda katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Kamati Kuu imewapongeza wananchi kwa kuipatia CHADEMA kura asilimia (47.7%)
dhidi ya CCM (49%) na (3.3%) za CUF.
ü Kamati kuu imesikitishwa
na vitendo vya fujo walivyofanyiwa viongozi, wagombea pamoja na Wanachama
mbalimbali katika sehemu mbalimbali palipo fanyika Uchaguzi. Kamati Kuu
imesikitshwa na kulaani vitendo hivyo vikiwemo vya watu kukatwa mapanga ,
kuchomwa visu na kubakwa kwa akina Mama na vijana wahuni walioandaliwa na Chama
cha Mapinduzi.
ü Kamati Kuu imelaani
vitendo hivyo vya kinyama vilivyofanywa mbele ya jeshi la polisi na Wakuu wa
Wilaya.
ü Ili kukabiliana na
vitendo vya fujo vinavyofanywa na vijana wa CCM dhidi ya wagombea, Wanachama na
viongozi wa CHADEMA, Kamati Kuu imeagiza kwamba kitengo cha ulinzi cha Chama
“Red Brigade” kiimarishwe zaidi kwa kuhakikisha kuwa vijana wote wa Red Brigade
Nchi nzima wanapewa mafunzo maalum ya UKAKAMAVU yatakayoandaliwa katika Makambi
maalum katika mikoa yote.
ü Kamati Kuu imejadili
maandalizi ya Uchaguzi wa madiwani katika kata nne (4) katika Jiji la Arusha.
Kamati Kuu imepokea kwa masikitiko taarifa juu mipango inayofanywa na jeshi la
polisi kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Magesa Mulongo na viongozi
wengine wa CCM mkoani Arusha katika kuhujumu zoezi la Uchaguzi kwa kuwatisha
wapiga kura kwa kutumia polisi na vijana wa Green Guard siku ya uchaguzi.
ü Kamati Kuu inamtaka
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) kuchukua hatua stahiki kuzuia harakati za polisi
na CCM za kuvuruga Uchaguzi na kutaka kujipatia ushindi kwa njia za hila. Aidha
Kamati kuu imelitaka jeshi la polisi kuheshimu maadili ya uchaguzi
yaliyosainiwa na Serikali, Tume ya uchaguzi na vyama vya siasa.
ü Kamati Kuu imesikitishwa
na Tume ya Uchaguzi kushindwa kuwazuia CCM kuendelea na kampeni za Uchaguzi
huku wakiwa wamezuia kampeni hizo kwa vyama vingine.
ü Kamati Kuu
imeendelea kuwapa pole wananchi wa Arusha kwa matukio mabaya wanaofanyiwa na
serikali ya CCM mkoani humo, na imewapongeza kwa kusimama kidete katika kulinda
haki na ukweli.
ü Kamati Kuu imewaomba
wananchi wa Arusha wajitokeze kwa wingi siku ya kupiga kura tarehe 14 Julai
2013, na imewataka wabunge wote washiriki katika kusimamia zoezi la upigaji
kura na uhesabuji kura siku ya Uchaguzi na wananchi wajitokeze kwa wingi
kulinda kura bila hofu.
5:0. Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Kamati Kuu imejadili kwa kina sana maudhui yaliyomo katika Rasimu ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba;
• Kamati Kuu imetambua kazi kubwa iliyofanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba
katika kukusanya na kuchambua maoni ya wananchi na kuandaa Rasimu ya Katiba
Mpya;
• Hata hivyo, Kamati Kuu imetambua na kuainisha mapendekezo mengine ya msingi
ambayo yanastahili kuboreshwa zaidi katika Rasimu hiyo;
• Msimamo na maazimio ya Kamati Kuu juu ya Rasimu ya Katiba Mpya yameainishwa
na kuchapishwa katika kijitabu maalumu ambacho kitazinduliwa katika Mkutano wa
hadhara utakaofanyika siku, tarehe na mahali patakapo tangazwa hapo baadaye.
Imetolewa na:
……………………….
Freeman A. Mbowe, (MP)
Mwenyekiti Taifa
Kamati kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo ilikutana katika Kikao cha dharura kuanzia tarehe 06-07/07/2013 katika Hotel ya Blue Pearl Dar es salaam kujadili pamoja na mambo mengine Rasimu ya Katiba mpya na hali ya Siasa nchini.
No comments:
Post a Comment