Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NI jambo lisilowezekana hata kidogo kukaa wiki moja au mbili
bila kuona tamko lolote kutoka kinywani mwa Waziri wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki, Samuel Sitta.
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ambaye pia ni
Mbunge wa Monduli, akizungumza jambo. Lowassa ametajwa katika mbio za urais
mwaka 2015.
Mwenyekiti wa CCM, akiwa kwenye kazi za chama chake. Jakaya Kikwete pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Sitta ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki kwa tiketi ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliwahi kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania katika kipindi cha mwaka (2005-2010).
Kiti cha sita baadaye kilikaliwa na Spika Anne Makinda,
ambapo bila woga wala soni, Sitta aliwaambia wafuasi wake kuwa nafasi yake
imehujumiwa kwasababu ya kuchukia ufisadi.
Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, akizungumza na Mwana CCM mwenzake, Rostam Aziz kushoto. Rostam aliachia ngazi nafasi zake ukiwamo ubunge kwa madai ya kuchafuliwa.
Waziri Sitta amesema hayo, akiamini kuwa mafisadi wamehujumu
cheo chake kwa kisingizio cha jinsia. Yani mwanamke ashike nafasi hiyo ambayo
yeye hakutaka iwe hivyo.
Mengi amekuwa akisema, lakini anasahau kuwa hata yeye
alipoingia katika nafasi hiyo mwaka 2005, ililazimika kumuondoa Spika Pius
Msekwa, akiitwa ‘Agano la Kale’.
Samuel Sitta, pichani
Nani asiyejua utawala wa Sitta bungeni ulivyokuwa na mshike
mshike mwingi kiasi cha kumlazimisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa
ajiuzulu nafasi hiyo mwaka 2008, akisema kuwa tatizo ni Uwaziri Mkuu.
Nimekuwa nikifuatilia kwa kina maneno ya Sitta kila wakati,
huku nikiamini kuwa mengi anayotoa, anayatumia kama mtaji wake kisiasa, akiwashughulikia
wabaya wake kwa kisingizio cha kuuchukia ufisadi uliotuwama ndani ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) pamoja na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Sitta anapotembea magharibi na mashariki kupinga ufisadi wa
viongozi wengine wa serikali inayoongozwa na chama chake, hakika kinachekesha
watu walionuna.
Ni kiongozi wa serikali kwa kupitia CCM anayoituhumu usiku
na mchana bila kujua athari zinazoweza kukiangusha chama chao.
Ni kutokana na hayo, naendelea kupekua huku na kule
kuutafuta utukufu wa Sitta, ndani ya CCM na serikali kwa ujumla.
Inawezekana wapo watu ambao ni wachafu, ila kwa ujasili huo
huo anaousema mtaani, basi angeutumia kuwataja watu hao ama kupeleka ushahidi wake
mahakamani ili tufanye kazi kivitendo zaidi badala ya porojo zisizokuwa na
tija.
Kwanini Sitta amekuwa akiidhalilisha CCM, japo mwenyewe kwa
utashi wake anaamini unafurahisha baadhi yao?
Usafi wa Sitta unatoka wapi? Haiwezekani. Hii ni kwasababu Sitta
ni miongoni mwa watu wanaotumia fedha nyingi bungeni wakati Watanzania wengi
wanaishi kwa kubangaiza.
Sijamuona Sitta akipinga ulaji huo kwa wanasiasa ambao wengi
wao wapo bungeni kulala, kupiga makofi, kufanyiana fitina na kusaini posho za
vikao, wakati walimu, askari polisi, madaktari wanaofanya kazi ngumu ya kuokoa
roho za watu wakiishi kwa mshahara mdogo.
Watu hawa hawajui kesho yao itakuwaje na ndio maana
tumeshuhudia walimu wengi wakishindwa kuhudhuria sehemu zao kazi kutokana na
changamoto wanazokutana nazo.
Akiwa kama Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ana fursa
ya kuingia katika vikao mbalimbali vya Baraza la Mawaziri, ameridhika na
kuingizwa kwa hoja ya kulipia simcard kwa Sh 1000 kwa mwezi.
Mpango huu umekuwa mchungu kwa Tanzania kwa sasa, huku vyama
vya siasa na viongozi mbalimbali wakipaza sauti zao, akiwamo Katibu wa Itikadi
na Uenezi CCM, Nape Nnauye, John Mnyika, Mbunge wa Ubungo kwa tiketi ya Chama
Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na wengineo kutoka chama tawala na
upinzani.
Sitta anajua kuwa vipo vijiji vingi vinavyostahili umeme
lakini tangu nchi ipate uhuru havijawahi kupewa huduma hiyo muhimu na kila siku
yamekuwa yakisemwa katika kila vikao vya Bunge?
Je, anajua kuwa watoto wa wapiga kura wake kule Urambo
wanasaga na rumba, wakivuja jasho, huku yeye akibaki mjini kutoa matamko ya
kuwatusi au kuwadhalilisha viongozi wenzake?.
Huu ni mgogoro gani kama kweli upo kati ya Sitta na viongozi
wengine kutoka ndani ya serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Jakaya Mrisho
Kikwete, moja ya viongozi wanaofanya kazi nzuri kiasi cha kuwafanya waje
kukumbukwa usiku na mchana?
Lowassa ambaye pia ni mbunge wa Monduli, alijiuzulu uwaziri
mkuu wake huku akitoa lawama kwa baadhi ya watu waliokuwa wakitolea macho
nafasi yake hiyo, kabla ya kuhusishwa na kashfa ya Kampuni tata ya kufua Umeme ya
Richmond.
Ndio hapo matamko mengi ya Sitta yanapoingizwa kwenye kejeli
kwa Lowassa, hasa kwa hoja zake za ufisadi, akiamini zitakuwa mbeleko katika
mchakato wake kisiasa.
Labda hayo yanapamba moto kutokana na spidi ya Lowassa,
mmoja wa watu wenye wingi wa watu wanaomuunga mkono. Kila pembe ya nchi anatajwa
usiku na mchana.
Ingawa si mjuzi wa vuta nikuvute ya machaguo ya urais hasa
ndani ya CCM, ila ni ngumu mno kumfanya Lowassa ashindwe kwenye mchakato huo
kama atahitaji nafasi hiyo mwaka 2015.
Japo hajatangaza wazi juu ya adhma hiyo, lakini Lowassa anatajwa
sambamba na wanachama wengine wa CCM, akiwamo Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Sitta asiyelala kwa ajili ya
kutangaza mabaya ya wenzake, bila kujua kuwa kauli zake ni kama bomu kwa chama
chake.
Ni kwasababu Watanzania wengi siku hizi tumezoea kuishi kwa
kukariri. Ama tunaishi kwa mazoea. Kama hivyo sivyo, basi mmoja ajitokeze
hadharani kumuuliza Sitta juu ya kukaa kwenye CCM ya mafisadi na wenye majungu?
Kama Rais Kikwete alimuhujumu kwenye uspika, kwanini alikubali
uwaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki?
Nafasi ambayo ni muhimu hasa katika kipindi hiki ambacho
Watanzania wenzetu, hasa wale wanaofanya kazi ya kutoka nje ya mipaka yetu
katika Bara hili wanaishi kwa kuhabatisha.
Watanzania hao wakiwapo madereva wanaishi kwa manyanyaso ya
aina yake, hasa nchi za Uganda, Rwanda, Malawi, Burundi, pale watu hao
wanapotaka kuingia au kutoka.
Ningetaka kuona utendaji kazi wa Sitta juu ya manyanyaso ya
Watanzania hao kwa kuimarisha ushirikiano kama cheo chake kinavyosema, badala
ya kuikandamiza CCM miaka nenda rudi.
Ndio, Sitta ametangaza kung’atuka katika ubunge ifikapo
mwaka 2015, ila sitaki kuamini kuwa hana ndoto za kuona chama chake kinaendelea
kuwa lulu ya Watanzania wote.
Ama Sitta anataka CCM ife? Najua Sitta ni miongoni mwa
wanasiasa makini, ila si sahihi kuendelea na malumbano yasiyokijenga chama
chake, akiamini ndio njia ya kuwasulubu wabaya wake.
Tunahitaji kauli thabiti na utendaji kazi uliotukuka kutoka
katika kinywa cha Sitta. Endapo anaona chama kinakwenda ndivyo sivyo, basi awe
wa kwanza yeye kusimama hadharani na kukemea na sio kubaki nusu kuzimu na nusu
peponi.
Nayasema haya nikiamini Sitta ataona jambo jema la kufanya
kwa ajili ya Tanzania. Hatuhitaji tena kupoteza muda.
Tunahitaji vitendo, maana siasa zisizokuwa na tija ndio
zilizotufikisha hapa. Kuna mengi ya kufanya kwa ajili ya kufanikisha maisha
bora kwa kila Mtanzania.
Mnyukano unaofanywa na Sitta dhidi ya serikali yake una
faida gani? Anajenga au anabomoa? Sitta ana mapenzi na CCM au lengo lake ni chama
hicho kutoweka katika historia ya Taifa letu?
Waswahili wanaamini kuwa mwanamke anayetumia muda wake
mwingi kuunadi upungufu wa mume wake basi huyo si muungwana. Hana sifa stahili
za kuwa mke wa ndoa.
Huyo ana lake jambo. Ama ameingia katika ndoa hiyo kwa ajili
ya kuondoa mkosi au pia kuna kitu amefuata hapo, hasa maslahi.
Hili si tusi kwake, maana aliwahi kuitoa dhidi ya Rais
Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, akisema kuwa mara nyingi
yanayojiri baada ya ndoa huwa hayaonekanai kwenye uchumba.
Haya Sitta anayajua. Mnyukano wao kisiasa waufanye ndani ya
vikao halali vya chama, ili apate nafasi ya kuwatumikia Watanzania.
Huo ndio ukweli wa mambo. Japo kuusema kunahitaji moyo,
ukizingatia kuwa hali ya siasa ilivyokuwa sasa, imeongeza joto na kuzalisha
makundi ya kutisha.
Hao ndio wanaopita huku wakituhumu upande mwingine, huku
hoja ya ufisadi ikitumika tofauti kwa kila mtu asiyekubaliana naye.
Hatuwezi kwenda hivyo. Tujaribu kuwa waungwana, maana maneno
mengi yanayotolewa katika jamii yamekuwa hayana tija.
Tunatumia vibaya nafasi zetu na kuwapotezea muda wao bure,
huku tukijua fika ugumu wa maisha wanaokutana nao mtaani kwao.
Tutumie fursa zetu vizuri kwa ajili ya maisha ya Watanzania
kwa kuhakikisha kuwa rasilimali watu, rasilimali fedha na maliasili zote kwa
Taifa zinanufaisha watu wote.
Hata iweje, bado siwezi kumtofautisha mbunge yoyote ndani ya
CCM au Waziri, hasa wale wanaotumia muda mwingi kutusi wenzao ili waonekane
wapo sahihi.
Watu watajiuliza na baadaye kupata majibu sahihi, hasa kwa
kukiwajibisha chama tawala CCM.
Ama hajui kuwa maneno yanaumba na wapo watakaofuata ushauri
wake, matusi yake dhidi ya viongozi wenzake na chama kwa ujumla, wakati siku
zote tunaambiwa samaki mmoja akioza ni wote?
Je, huo utukufu wa Sitta utaendelea kubaki mioyoni mwa
Watanzania hata kama muda wake mwingi aliutumia kumtusi Kikwete, Lowassa na
wengine anaopingana nao ndani ya CCM?
+255 712 053949
No comments:
Post a Comment