Na Kambi Mbwana, Dar
es Salaam
NI jambo la
kumshuruku Mungu kuona anaendelea kutupigania kwa kutubariki kila jema na
kusukuma gurudumu la maisha yetu.
Picha ya wawili wapendanao
Hakuna anayepaswa
kushukuriwa isipokuwa yeye, maana kila tunalofanya hapa chini ya jua kunatokana
na mazuri yake na upendo wake kwa binadamu wote duniani.
Na kwa wale
wanaosumbuliwa na matatizo ya hapa na pale, pia ni mipango yake hivyo badala ya
kumkufuru tutaje jina lake mbele kwa kuwa ndio kila kitu katika maisha yetu.
Baada ya kusema hayo,
leo napenda kuzungumzia matatizo ya baadhi ya wapenzi wanavyoweza kujichanganya
kwa kuzoeshana pesa kama karata ya kuwafanya waishi kwa amani tele.
Si vibaya kupeana
pesa au thamani nyingine, ila inapotokea huna si lazima ufanye kila uwezalo,
ikiwapo kukopa au kukwapua kwa ajili ya kuwaridhisha wapenzi wetu, hata kama
tuwapende kiasi gani.
Katika Dunia ya leo,
kitu kinachoongoza kuwatenganisha watu kwenye mapenzi yao basi suala la pesa
linashika nafasi ya kwanza. Hizi ndio zinazoweza kufanya kila kitu, hivyo
wachache wao kujikuta wakifarakana.
Ndugu msomaji wangu
mpendwa, hupaswi kutanguliza pesa kwa mtu wako, hasa unapoanzana naye katika
uhusiano wenu. Jifanye kama huna, ili ufahamu uhalisia wa huyo unayetaka kuwa
naye.
Kwanza wapenda hela
wengi wao hawawezi kuvumilia njaa, lazima atafanya vituko akiamini huna cha
kumhonga. Huyo yupo kimaslahi zaidi. Anaangaliaa fedha ili ajikimu katika
maisha yake.
Nasema hivyo
kwasababu kama utatanguliza pesa na kufanikiwa kuwa naye, kesho anaweza
kukuacha kama mtoto yatima utakapopunguza huduma kwake, maana amefahamu wewe
ndio ATM yake.
kIla anachotaka kwako
unampa. Tena zile anazotaka na wakati mwingine kwa ujinga wako unamuongezea
mara mbili yake. Kwa bahati mbaya, kesho unaingia kwenye mgogoro wa kifedha,
unalazimika kupunguza au kusitisha kabisa kumpa pesa kama ulivyomfanyia mwanzo.
Suala hilo haliwezi
kumfurahisha hata kidogo. Lazima ajuwe umesitisha kwasababu umemchoka. Kama
hivyo haitoshi, wengine huamua kuangalia upande mwingine, kwa wenye fedha zao.
Hilo ni tatizo kubwa
linaloanzisha mfarakano katika uhusiano wa kimapenzi, hivyo wakati mwingine
kuwatenganisha wawili hao. Angalia, licha ya kutumia gharama zako nyingi kwa
mtu huyo, awe mwanamke au mwanamume, lakini unaachana naye na kila mtu
kuangalia maisha yake.
Ni kama vile
ulimaliza kuni kwa kuchemsha mawe. Hupaswi kuishi hivyo na mtu unayetaka
kuanzisha naye uhusiano wowote, ukiwapo ule unaoweza kuzalisha ndoa kama
wanavyofanya vijana wa leo.
Nadhani huu ni wakati
wetu kujua kuwa si lazimaa tutangulize fedha kwa wale tunaohitaji kuwa nao
kimapenzi. Tunaweza kuwafanyia kila kitu, sambamba na kuwanunula magari, lakini
wasituweke moyoni.
Wanasema upendo wa
kweli unatoka moyoni. Kujikweza, kujifanya tunazo fedha ni njia za kutumia
gharama ambazo si muda wote zinaweza kutuletea amani, hasa pale tutakapoingia
kwenye hatua mbaya za kiuchumi.
Pale tutakaposhindwa
kupata fedha za kuwapa wapenzi wetu kama tulivyowazoesha awali, hivyo
tuliangalie suala hili kwa kina kwa ajili ya kutufanya tuwe na amani moyoni.
Tusipokuwa makini,
tutaweka mbele pesa ili kuwaridhisha wapenzi wetu, huku wao wakiwa wepesi
kutumia nguvu zetu na kuwapatia wale wanaowapenda kwa dhati na kuharibu
mpangilio mzima wa maisha yetu.
Tuzinduke na kuishi
kama Mungu alivyotujalia na hakuna haja ya kutumia nguvu kubwa kuwapatia pesa
watu, ingawa sio vibaya kuwapa chochote kitu watu wetu kwa namna moja ama
nyingine.
Nawatakia Mfungo
mwema wa Ramadhan Waislamu wote duniani, hasa wale watakaojaliwa kufunga katika
siku za hivi karibuni.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment