Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NI siku nyingine tena tunapokutana katika safu hii inayokujia kila
Jumamosi, huku nikiamini kuwa tutaendelea kuwa pamoja tukielezea mambo ya
uhusiano na maisha.
Wawili wapendanao wakitafakari love yao.
Nitakuwa mchoyo wa fadhira kama nitashindwa kukushuru wewe
unayeguswa na safu hii kiasi cha kutufanya tuwe wote kila wiki tukichambua
mambo haya ya uhusiano.
Hakika ndio furaha yangu, maana bila wewe safu hii haiwezi kuwa na
mashiko kwa namna yoyote ile. Baada ya kusema hayo, nirudi kwenye mada yangu ya
wiki hii.
Siku za nyuma nilielezea kujirahisi na namna inavyoleta
mkanganyiko kwenye jamii. Kutokana na ugumu wa msichana kumwambia mwanaume kuwa
anampenda, baadhi yao hujikuta wakiingia kwenye wasiwasi mkubwa.
Kwa mfano, mwanamke anayemwambia mwanaume kuwa anampenda, siku
zote anabaki kwenye presha. Hawezi kujidai katika uhusiano huo.
Pia wapo wanaume wanaotumia udhaifu huo kuwanyanyasa wasichana wa
watu kisa wamelazimishwa mapenzi. Ndio hao ambao wanamuachia msichana kila
kitu.
Hata msichana akitamani kutoka out na mpenzi wake huyo, dume zima
linaweza kujibu sipo tayari, au sina pesa leo. Anajibu hivyo akiamini kuwa
mwanamke atatoa yeye.
Haya ndio madhaifu, maana mwanaume huyo anafanya hivyo kwasababu
ameyafutwa yeye. Ila kama yeye mwenyewe ndio amesumbuka kumpata mwanamke huyo,
hakika angekuwa na nidhamu kwa mpenzi wake.
Linapotokea suala hilo, wasichana wengi wanajikuta wakiishi kwenye
wasiwasi wa aina yake. Hawajidai hata kidogo katika uhusiano huo.
Ndio maana kuna kila sababu ya sisi jamii kuwa makini katika suala
zima la uhusiano kwa ajili ya faida yetu. Na inapotokea mmoja wetu anaona
hapewi ushirikiano kwa mtu anayempenda, basi akubali matokeo.
Kinyume cha hapo atakuwa mtu wa presha siku zote na hata hayo
mapenzi hawezi kuyafurahia hata kidogo. Ndio kwanza mtu anaweza kukonda.
Hawezi kuona raha ya mapenzi kama yanavyosemwa na baadhi yao,
maana utamu huu una pande mbili. Huu ndio ukweli wa mambo, hivyo tuangalie mara
mbilimbili.
Kwa mfano, kuna baadhi ya wasichana ambao siku zote kazi yao ni
kuhudumia wanaume. Hii ni kwasababu waliweka mbele sana matamanio yao kwa watu
hao.
Ama wao ndio waliojilengesha ili wapendwe au ndio waliojitoa
kuwarubuni wanaume hao. Haya ni matatizo makubwa katika suala zima la uhusiano.
Ingawa kila mmoja ana nafasi ya kusema kwa mwenzake anapoona
ameshikika kihisia, ila hatuwezi kujilainisha hata kwa wale wasiokuwa tayari.
Kuna haja gani kujitoa kwa mtu asiyekuwa na walau robo ya upendo
wa dhati kwa mwenzake? Nini maana ya raha ya upendo, kama faida yetu ni
kutumika zaidi hasa kwa suala zima la pesa na matunzo kwa wapenzi wetu?
Hadi leo wapo wanaume wanaotegemea mifuko ya wasichana,
wakijilainisha kwasababu wao ndio walioombwa kuingia kwenye uhusiano mahali fulani.
Hii sio kweli na kuna kila sababu ya kujiangalia upya kama tuna
lengo la kuishi kwa furaha, maana si kila mahali kunastahili kuanzisha uhusiano
wa kimapenzi.
Kwa kulijua hili, nadhani jamii hasa wasichana watatambua namna
gani wapo na wanaume kwenye uhusiano wakati wenzao hawana thamani ya upendo.
Huu ndio ukweli wa mambo na kuna kila sababu ya kujiangalia upya
kwa faida yetu, maana kama hatujajipanga katika uhusiano, basi hata maisha yetu
yanakuwa ya mashaka.
Tukutane wiki ijayo.
+255 712 053949
No comments:
Post a Comment