Na Mwandishi Wetu, Handeni
NEEMA imeanza kuonekana katika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, baada ya kupata ufadhili kutoka Benki ya
Dunia (WB), kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa mabwawa ya maji katika vijiji 17 vilivyoko
wilayani hiyo ili kupambana na tatizo la shida ya maji.
Mkuu wa Wilaya Handeni, Muhingo Rweyemamu
Hayo yameelezwa na Mkurungezi wa Halmashauri hiyo, Dk. Khalfany
Haule wakati akisoma taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa mwaka
2012/2013, kwenye kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika wilayani
hapo, huku ukiwa ni mpango mzuri kwa wilaya hiyo.
Alisema pamoja na ujenzi huo, vijiji viwili vya Misima na
Gendagenda vimepata ufadhili wa Sh milioni 360 kutoka Shirika la Chakula na
Kazi la Japan kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa mawili.
Ujenzi unatarajiwa kuanza hivi karibuni.
Haule aliongeza kuwa, Shirika la DANIDA limeweza kufadhili ujenzi
wa visima virefu sita katika vijiji vya Manga, Mkata Mashariki, Mkata
Magharibi, Kwamkonga, Kwedizinga na Michungwani.
“Licha ya ufadhili wote huo, halmashauri yetu bado inakabiliwa na
changamoto ya uchakavu wa mitambo ya kusukuma maji na ukosefu wa umeme wa
uhakika pamoja na wizi wa miundombinu hiyo unaofanywa na wananchi,” alisema
Haule.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,
Ramadhani Diliwa, aliwataka madiwani kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa
miradi hiyo pamoja na utunzaji wa vyanzo vya maji ili wasiviharibu na
kusababisha tatizo kuwa kubwa.
No comments:
Post a Comment