Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KILA mtu anajua kuwa sheria na haki ni vitu viwili
tofauti. Usilazimishe kupata haki, kwasababu sheria imeonyesha juu ya madai
yako.
Kufanya hivyo ni kujipotezea muda wako unaoweza kuutumia
katika kazi nyingine za maendeleo yako.
Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi 'Sugu'
Waziri Mkuu Mizengo Pinda
Pamoja n ayote hayo, lakini wakati mwingine si sahihi
kujificha kwenye mhimili wa kisheria kwa kufanya mambo ambayo ni tofauti katika
jamii.
Kila mmoja anapaswa kuishi kwa upendo bila kuweka u-mimi,
vyama vyetu na mengineyo pia.
Nasema haya baada ya Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph
Mbilinyi, maarufu kama ‘Sugu’kutoka (CHADEMA)kuachiwa huru na Mahakama ya
Wilaya ya Mkoa wa Dodoma, kwa madai kuwa hati ya mashitaka ina mapungufu
kisheria.
Sugu alipandishwa kizimbani katika mahakama hiyo, mbele
ya Hakimu Mfawidhi wa Mkoa wa Dodoma, Elinaza Luvanda na kusomewa shitaka
linalomkabili kuhusu kutoa lugha ya matusi katika mtandao wa kijamii, moja ya
vitu vinavyotumiwa vibaya na watu wengi.
Katika mitandao hiyo, kila mmoja anaandika kile
anachojisikia, bila kujali faida au hasara inayopatikana kwa kuandika upupu
wake.
Sugu aliandika hivi;”Tanzania haijawahi kupata Waziri
Mkuu mpumbavu kama Pinda”.
Kauli hii ilisababisha maswali mengi kwa Watanzania, hasa
wakiamini kuwa imetokana na matamshi ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kuwataka
watu wapigwe watakapokaidi amri halali za jeshi la Polisi.
Bila kuangalia sheria inasemaje juu ya sakata hilo,
lakini kiubinadamu, Sugu hakaupaswa kuandika maneno ya matusi dhidi ya Pinda.
Nasema hivi kwasababu Sugu kama mbunge wa Tanzania,
alikuwa na nafasi kubwa ya kukataa agizo la mtu yoyote, kwa kutangaza bungeni.
Angeweza hata kushawishi kutokuwa na imani na Pinda, kama
wabunge wengi walivyowahi kufanya.
Lakini Sugu alifanya haya kihuni tu. Akiamini kuwa
mihemko ya kisiasa au sheria zitambeba.
Mambo kama haya yanasababisha kutokuelewana katika jamii.
Leo hii kama sheria hazitamki wazi juu ya kosa hilo, basi yoyote anaweza
kufanya anavyojisikia bila kuogopa chochote.
Je, mwingine ajitokeze mchana kweupe, kuandika au kusema
kiongozi mfano wa Pinda ni mpumbavu?
Je, serikali hii inaongozwa na wapumbavu? Je,Msajili wa
Vyama vya siasa, John Tendwa naye ni mpumbavu?
Kiubinamu ukilizungumzia neno upumbavu, hasa kwa viongozi
wetu ni jambo la kutia kichefu chefu.
Sugu angeyasema hayo kwa watu anaofanana nao, iwe kicheo
au kiumri. Umri wa Sugu na Pinda haufanani kamwe.
Hivyo kuusema upumbavu wa Pinda hadharani ni kumvunjia
heshima kupita kiasi. Tuukatae hadharani.
Mtindo huu ukidhihiri hauwezi kudumisha ut una uungwana
wetu. Siku zote uungwana ni vitendo.
Angalia, mwendesha mashitaka ambaye ni Wakili wa
Serikali, Harieti Lopa alidai mtuhumiwa alitenda kosa la kutoa lugha ya
matusi kwa Waziri Mkuu, Pinda Juni 24, mwaka huu eneo la Manispaa ya Dodoma.
Alifika mbali zaidi kwa kudai mshitakiwa huyo, ambaye ni
Sugu aliandika ujumbe huo bila kuutaja, ambao unaleta uvunjifu wa amani kwa
Waziri Mkuu, hivyo ni kosa la jinai kwa mujibu wa Sheria kifungu kidogo namba
89 (a).
Sakata hili wakati linaendelea kuchambuliwa kwa mujibu wa
sheria zetu, mshitakiwa alikana shitaka ndipo Wakili wa Serikali kuiomba
mahakama itaje tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo.
Hata hivyo, Sugu alitetewa na mwanasheria wake, ambaye
pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, alikataa kesi hiyo kupangiwa
siku nyingine, akisema hati ya mashitaka ni mbovu na haikukidhi matakwa ya
sheria ya jinai.
Lissu anasema “Hati ya mashitaka, inatuhumu kosa ni
kutumia lugha ya matusi kifungu cha 89 (i) kifungu kidogo (a) katika Sheria
zetu ambapo matusi yenyewe hayajatajwa, bali yanatolewa maelezo ya kosa kuwa
lugha ya matusi ambayo inaweza kuvunja uvunjifu wa amani kwa Pinda, hiyo lugha ya
matusi ni ipi,” Lissu alihoji.
Lissu alifika mbali zaidi kwa kusema kuwa upungufu
mwingine wa kisheria ni hati ya mashitaka ipo kimya, hivyo kushangaa mshitakiwa
atajitetea kwa lipi na ataandaa utetezi namna gani, wakati anachodaiwa kukiweka
mtandaoni kikiwa hakijasemwa?
Maneno ya mwanasheria huyu yalipatiwa ufumbuzi na hakimu
kujiridhisha kisheria na kukiri kuwa ni kweli hati hiyo ina upungufu wa
kisheria kwa mujibu wa kifugungu cha Sheria Namba 132 sura ya 20 na hivyo
kuifutilia mbali hati hiyo ya mashitaka ikiwa ni pamoja na kumuachia huru
Mbunge huyo.
Pamoja n ayote hayo, si malalamiko yangu kuachiwa kwa
Sugu, ila namna watu watakavyoweza kutumia udhaifu huo kuwatendea wengine.
Kila mtu anaweza kufanya kama alivyotenda Sugu, dhidi ya
mwingine. Nani anaweza kukamatwa leo akiandika kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Willbroad Slaa ni mpumbavu kwasababu ameacha
upadre na kuhamia kwenye siasa, tena Chadema?
Ni kutokana na hilo, nadhani kuna haja sasa wanasiasa
wetu, akiwamo Sugu kuona kuwa siasa haziwezi kumfanya ajipachike uwendawazimu.
Lazima ajuwe kuwa heshima ni kitu ch abure, hivyo
aihusudu ili afike mbali zaidi katika harakati zake.
Sina chuki dhidi ya wanasiasa hawa.Kila mtu anataka
mabadiliko ya kisiasa na kiutawala, ila si kwa njia ya uvunjifu wa amani.
Kwa sasa wapo watu ambao hawataelewa uvunjifu wa amani
utatokea wapi juu ya sakata la Sugu na Pinda.
Lakini Pinda kama Waziri Mkuu pia ni kiongozi kutoka
Chama Cha Mapinduzi (CCM), chini ya Mwenyekiti wake Jakaya Mrisho Kikwete.
Ukiacha uongozi wake katika chama na serikali, anabaki
kama binadamu wa kawaida mwenye ndugu au marafiki.
Hivyo basi, katika sakata hili, kuna siku baadhi yao
watashindwa kukubali utu wa mtu unavyotolewa kwa ajili ya siasa za maji taka.
Hao watagoma kusubiri. Watataka kulipiza kisasi, hivyo
kuashiria kuwa usalama utakuwa kwenye mashaka makubwa.
Haya si ya kukubali yaendelee kufanyika katika Taifa hili
linalokabiriwa na sekeseke la siasa.
Tusikubali kabisa, hivyo Sugu kama Mbunge alipaswa
kujiheshimu na kuheshimu wengine, akiamini kuwa chochote atakachosema
kitaonekana.
Mitandao ina nguvu kubwa mno. Watu wengi sasa wamekuwa
humo. Ndio maana maandishi machache aliyosema, lakini yameibua mzozo hadi
kufikishwa polisi.
Kuukosoa uamuzi wa mahakama juu ya kutukanwa kwa Pinda,
hakuendi sambamba na kuwalimisha kumfikisha tena Sugu mahakamani, ila kumfanya
ajuwe anapaswa kujichunga na anachokisema.
Hati ya mashtaka kama ina makosa, mapungufu, inaweza
kuwekwa sawa, lakini hatua hiyo itaendeleza kujenga uhasama kati ya viongozi
hawa.
Suala hili la Pinda juu ya amri yake kwa polisi ni
tatizo, ila hakumfanyi atukanwe kama mtoto.
Ndio maana alipotoa tamko hilo wanaharakati walilipinga,
ila si kwa njia ya kumvunjia heshima kama alivyofanya Mbunge Sugu.
Nadhani tunawajibu wa kuishi kwa upendo na kuheshimiana,
ukizingatia kuwa kutaleta maendeleo ya kweli.
Tusitumie udhaaifu wa mapungufu kaatika sheria zetu
kuwakandamiza wenzetu, maana leo kwa Pinda kesho Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa
Chadema na Mbunge wa Hai, Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa
Ibrahim Haluna Lipumba, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na viongozi
wengine.
kambimbwana@yahoo.com
+255 712053949
No comments:
Post a Comment