https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Friday, July 26, 2013

Taifa Stars hakuna kulala kesho mechi na wenyeji wao Uganda

Na Boniface Wambura, Uganda
MOJA ya mikakati ya Taifa Stars kwenye mechi ya kesho (Julai 27 mwaka huu) dhidi ya Uganda kuwania kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Tatu za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini ni kushambulia kwa muda mwingi wa mchezo.
Msemaji wa TFF, Boniface Wambura
Kocha Kim Poulsen amesema maandalizi ya Taifa Stars jijini Mwanza kwa ajili ya mechi hiyo ambayo Uganda inaongoza kwa bao 1-0 yalikuwa mazuri, lakini mabao ni muhimu hivyo watashambulia bila kusahau kulinda lango lao.

“Unapocheza mechi za aina hii za nyumbani na ugenini, huku mwenyeji akiwa anaongoza mabao yana maana kubwa katika mechi. Mabao yanabadili mchezo na pia wachezaji kifikra,” amesema Kim akizungumza na waandishi wa habari kwenye hoteli ya Mt. Zion ambayo Stars imefikia.

Amesema katika mechi ya kwanza walitengeneza nafasi nyingi lakini hawakuzitumia, hivyo wamekuwa wakifanya mazoezi ya kushambulia, jinsi ya kutengeneza nafasi, na jinsi ya kumalizia.

“Hivyo tuko hapa (Kampala) kwa ajili ya kufunga, ni lazima tufunge ili tuweze kuendelea na mashindano. Lakini ngome yetu nayo ni lazima iwe makini ili kutoruhusu bao,” amesema Kim na kuongeza kuwa kikosi chake cha kwanza ni lazima kitakuwa mabadiliko kutoka na Mwinyi Kazimoto kuingia mitini na Shomari Kapombe kwenda kwenye majaribio Uholanzi.

Amesema angalau kutakuwa na mabadiliko kwa kuingiza sura mbili mpya katika kikosi cha kwanza, na kuongeza kuwa wachezaji wanafahamu umuhimu wa mechi hiyo kwani timu ikienda kwenye Fainali za CHAN itakuwa manufaa kwao binafsi.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imefanya mazoezi ya mwisho leo jioni Uwanja wa Mandela ulioko Namboole ambao utatumika kwa ajili ya mechi hiyo kesho.

Mechi hiyo itaanza saa 10 kamili jioni kwa saa za Afrika Mashariki na itachezeshwa na waamuzi kutoka Madagascar wakiongozwa na Kanoso Abdoul Ohabee wakati mwamuzi msaidizi namba moja ni Andirvoavonjy Pierre Jean Eric. Mwamuzi msaidizi namba mbili ni Jinoro Velomanana Ferdinand huku Andriamiharisoa Hubert Marie Bruno akiwa mwamuzi wa mezani (fourth official). Kamishna wa mechi hiyo namba 38 ni Ismail Kamal kutoka Ethiopia.

Stars inatarajiwa kupangwa hivi; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, David Luhende, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Athuman Idd, Salum Abubakar, Frank Domayo, John Bocco, Amri Kiemba na Mrisho Ngasa.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...