Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WADAU wa soka nchini Kenya wapo kwenye shangw za aina yake,
baada ya Victor Mugabe Wanyama kusajiliwa kwenye klabu ya Southampton ya Uingereza
kwa Paundi Milioni 12.
Mrisho Ngassa, nyota wa Yanga na Taifa Stars
Wanyama ametokea katika klabu ya Celtic ya nchini Scotland,
huku akifanikiwa kuwapa imani watu wa Kenya kuwa atafika mbali katika maisha
yake ya soka.
Hii si furaha kwa watu wa Kenya tu, ila Afrika nzima
tunawajibu wa kumuombea mchezaji huyo ili afike mbali zaidi katika maisha yake
ya soka duniani.
Amefanya vizuri huku kujituma kwake hatimae kukimpeleka
katika soka lenye ufundi na ushindani wa aina yake nchini Uingereza.
Nikiacha kumuangalia nyota huyo na mafanikio yake, kiu
inanijia kuwageukia wacheza soka wa Tanzania. Hawa ambao hamu yao kubwa ni
kwenda na kurudi katika timu za nyumbani.
Raha yao kubwa ni kusajiliwa Simba ama Yanga, bila kuangalia
mbele, licha ya kufahamu utajiri mkubwa unaoweza kupatikana endapo watacheza
soka la kulipwa.
Kumekuwa na kasumba za aina yake Tanzania. Wapo wachezaji
wanaojiweka nyuma kujiandaa ili wafikie malengo yao. Mchezaji anakosa ratiba
kamili ya mazoezi.
Mchezaji wa Tanzania hata kama ana uwezo, ila anajinyima
kula, ama kuwa mwepesi kutega mazoezi yake. Wapo wachezaji ambao kila siku ni
wategaji, wakisingizia kuumwa.
Mchezaji wa aina hiyo kufika malengo ya soka la Kimataifa ni
ndoto, hata kama awe vipi. Kwa mfano, mchezaji kama Mrisho Ngassa licha ya
kuonekana ni hodari Tanzania, ila kwenye soka la Kimataifa hana nafasi ya
kucheza huko.
Akiingia kwenye vipimo anaonekana ni mwepesi. Makocha wenye
kuangalia ubora, ni wazi atamuona hafai, hivyo kurudi tena Tanzania kwa ajili
ya kucheza Simba au Yanga.
Na ndio maana kila siku tunawaona wanavyoona furaha kwenda
Yanga kusajiliwa Simba, bila kujua kuwa wanavyoendelea kung’ang’ania soka la
Tanzania, maendeleo yao yanachelewa.
Hakika siwezi kuvumilia. Siwezi Kuvumilia kuona kila siku,
wachezaji wetu wa Tanzania wanashindwa kuwa na mbinu zenye kuwafikisha mbali
ili iwe sehemu ya maendeleo yao.
Kwanini wachelewe? Je, lini watajiandaa kucheza soka la
kulipwa? Ni lini wachezaji wetu watajenga miili yao kwa kujisimamia imara
katika mlo na mazoezi?
Nadhani ni wakati wao sasa kuinuka na kuona wamekalia noti
kwa kushindwa kujituma na kusaka namba Ulaya. Tunao wachezaji wengi wazuri na
wakijiwekea mikakati watafika mbali.
Na wachezaji wa Tanzania lazima wajuwe kufika timu
zinazocheza ligi Kuu Uingereza au Italia si jambo rahisi. Haiwezi kutokea kwa
Mrisho Ngassa, Juma Kaseja, Mwinyi Kazimoto kulala na kuamka ameitwa katika
timu za Mataifa hayo.
Hata kama wakiitwa huko, basi itawalazimu kuanza katika ligi
ndogo, maana katika soka ni jambo la kawaida. Nadhani wacheza soka wa Tanzania
waongeze bidii.
Vijana kama vile Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu, Henry
Joseph Shindika na wengineo wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi waongeze
bidii ili wafike mbali.
Ndio mpango unaoweza kuitangaza Tanzania katika soka la
Kimataifa, ukizingatia kuwa sasa Kenya kwa kufanikiwa kuwa na nyota anayecheza
soka nchini Uingereza, watu wengi watakuwa wanaiangalia nchi hiyo pamoja na
wachezaji wao.
0712 053949
No comments:
Post a Comment