Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
TIMU ndogo ya vijana ya Coastal Union yenye maskani yake
jijini Dar es Salaam, jana imefanikiwa kupenya nusu fainali ya mashindano ya
Rolling Stone yanayofanyika jijini Arusha.
Coastal imetinga nusu fainali baada ya kuwafunga bao 1-0
timu ya Dereda, lililowekwa kimiani na Ayubu Semtawa dakika ya 64 na kufanikiwa
kupenya hatua hiyo muhimu na kuwapa raha mashabiki wao wa soka, hususan wa
mkoani Tanga.
Akizungumza jana kwa njia ya simu, Meneja wa Coastal Union,
Abdulrahman Ubinde, alisema wanashukuru kwa vijana wao kufanya vizuri katika
mashindano hayo na kutinga nusu fainali.
Alisema kuwa wanaamini wataendelea kujiweka sawa katika
kuiandaa timu hiyo ya vijana ili waendelee kufanyaa vyema katika mashindano
hayo ya vijana yenye umuhimu mkubwa.
“Tunashukuru kwa vijana wetu kuendelea kuwapa raha wadau wa
soka wa Tanga na Tanzania kwa ujumla, baada ya kupania kurudia historia ya
mwaka jana walipotinga fainali nchini Burundi.
“Lengo ni kutinga fainali kwa ajili ya kunyakua Kombe hilo
ambalo kwa mwaka huu linafanyika hapa jijini Arusha, hivyo tutaendelea na
harakati zetu na kuwapaa moyo wachezaji wetu,” alisema Ubinde.
Timu ya Coastal Union ni miongoni mwa klabu zilizoweka
mikakati kabambe ya kuwekeza katika soka la vijana, jambo linaloleta picha
nzuri ya kukuza soka hapa nchini.
No comments:
Post a Comment