Na Kambi Mbwana, Dar
es Salaam
MWENYEKITI wa Kamati
ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Pope, amesema kwamba bado kunahitajika beki
na mshambuliaji ili kuifanya klabu yao iwe na uhakika wa kufanya vizuri katika
michuano ijayo.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage
Katika mchezo wa
kirafiki dhidi ya timu ya URA ya nchini Uganda, Simba walifungwa bao 2-1 na
kuleta majonzi kwa mashabiki wao.
Akizungumza mwishoni
mwa wiki, Hans Pope alisema kuwa bado kuna umuhimu wa kuongeza wachezaji kwa
ajili ya kuifanya timu yao iweze kufanya vizuri katika michuano ijayo, ikiwamo
Ligi ya Tanzania Bara.
Alisema japo
wachezaji waliocheza mechi dhidi ya URA wanaonyesha kiwango, ila wakiongeza
nguvu kulingana na mapengo yanayoonekana, mambo yatakuwa mazuri.
“Tunahitaji kuwa na
kikosi imara kwa ajili ya kuwapa shangwe mashabiki wetu, hivyo
tunakusudia kuendelea kutafuta wachezaji kadhaa kabla ya ligi kuanza.
“Tumeona wote bado
kuna nafasi zinahitajika, ikiwamo beki bora na mshambuliaji kabla ya ligi
kuanza, ukizingatia kuwa tunataka tufanye vyema katika michuano itakayoanza
Agosti 24 mwaka huu,” alisema.
Ligi ya Tanzania Bara
inatarajiwa kuanza Agosti 24 mwaka huu kwa kushirikisha timu 14 ambazo zimeanza
mazoezi kwa ajili ya patashika hiyo.
No comments:
Post a Comment