https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Tuesday, July 09, 2013

Chadema watetea msimamo wao wa kujitoa katika Kongamano la kujadili amani kwa kusema kuwa halina jipya



CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetetea msimamo wake wa kususia kongamano la Amani lililoitishwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (Tanzania Center For Democracy).
Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe.

Kongamano hilo lilipangwa kufanyika leo Julai 9 hadi kesho Julai 10 katika Hoteli ya White Sands ya jijini Dar es Salaam, ambapo kingehudhuriwa na watu mbalimbali kutoka katika vyama vya siasa.

Tamko lililotolewa na Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo, Benson Singo Kigaila, ilisema kuwa kongamano hilo la amani kama lilivyotajwa  na TCD, lina mapungufu mengi, hivyo wao hawawezi kushiriki na hili ndio tamko lao.

Litafuguliwa na Mwenyekiti wa TCD, Mbunge wa kuteuliwa na Rais, Mheshimiwa James Mbatia na litafungwa na Rais Jakaya Kikwete.

Baadhi wa shiriki, ni pamoja na mawaziri, viongozi wakuu wa vyama vyenye wabunge ambavyo ni wanachama wa TCD – Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Wananchi (CUF), United Democracy Party (UDP), Tanzania Lebour Party (TLP), NCCR- Mageuzi na Chadema.

Aidha, chama cha UPDP nacho kitashiriki mkutano huo kwa niaba ya vyama vingine ambavyo havina wabunge. Ndugu waandishi wa habari, Chadema kikiwa mmoja wa wadau wakubwa wa TCD, kimepokea mwaliko wa kutano huo. 

Hata hivyo, tunapenda kutumia nafasi hii, kupitia kwenu, kuutangazia umma na wote wanaotutakia mema na
kulitakia mema taifa, kwamba hatutashiriki mkutano huo kwa sababu zifuatazo: Kwanza, Mwenyekiti wa TCD, Mheshimiwa Mbatia kwa makusudi amekiuka maazimio ya kikao ya kuteuwa muwezeshaji wa mkutano huo na badala yake akafungamana na CCM kuteuwa watu anaowataka wao.

Pili, Chadema haitashiriki mkutano huo kwa kuwa Amani haijadiliwi. Amani inatengenezwa na kuwapo kwa mazingira ya haki na usawa; na kwamba aliyebobea katika uvunjaji wa haki hizo, ni serikali yenyewe.

Katika mazingira haya, Chadema inaona hakuna
umuhimu wa kushiriki kwenye mkutano ambao washiriki ni wale wale wanaotuhumiwa kuvunja
haki za binadamu.

Tatu, Amani siyo ya vyama vya siasa pekee yake.
Amani inahusisha wadfau mbalimbali wakiwamo
viongozi wa kidini, taasisi za kiraia na mashirika
yasiokuwa ya kiserikali. Taarifa zilizopo, ni kwamba mkutano huu haukushirikisha viongozi wa kidini, na
hivyo, tunadhani kuwa siyo jambo zuri kama kweli
tunataka kutafuta amani ya taifa. 

Nne, Chadema haitashiriki mkutano huo kwa kuwa aliyepanga, aliyefadhiri na aliyeitisha mkutano huo kwa mgongo wa TCD, ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, Mizengo Kayanza Peter Pinda, ambaye ndani ya nafasi yake, haonekani kuwa na dhamira ya dhati ya kuwapo amani katika taifa letu.

Ndugu waandishi wa habari; Ninyi ni mashahidi wa jinsi Waziri Mkuu Pinda alivyo mstari wa mbele katika kuhubiri kauli za chuki, uhasama, uchochezi, ubabe na ukiukwaji wa haki za
binadamu nchini.
Siyo mara moja wala mbili, Waziri Mkuu Pinda amesikika, tena ndani ya Bunge, akihamasiha vyombo vya usalama kuvunja sheria kwa kupiga, kuteka na kung’oa meno watu
wanaotumia haki zao za kikatiba kushinikiza serikali
kuchukua hatua dhidi yamaovu. 

Tano, Chadema haitashiriki katika mkutano huo kwa kuwa Serikali ya CCM inayofadhiri mkutano huu,  imejaa unafiki kwa kuhubiri amani mchana, wakati usiku inachochea uhasama wa kidini, kisiasa na inawagawa Watanzania kwa misingi ya imani za kidini na vyama. 

Chadema inao ushahidi usio na chembe ya mashaka, kwamba mifarakano mingi inayotokea kwenye jamii, mapigano katika koo mbalimbali, ugomvi wa kugombea ardhi kati ya wakulima na wafugaji, machafuko kwenye mikutano ya hadhara ya vyama
vya upinzani, sababisho kuu ni CCM kuvitumia vyombo vya dola, kutaka kukibeba chama hicho. 

Tunataka umma utuelewe, kwamba tuna dhamira ya dhati ya kuona Tanzania inakuwa kisiwa cha amani, lakini hatutakubali kushiriki katika vikao ambavyo wanaoviongoza hawana dhamira hiyo. 

Ili amani iweze kupatikana, ni sharti tuwe kuwepo mijadala
inayoingia kwenye viini vinavyosababisha amani ikosekane na hatua hiyo ianze kuchukuliwa na ione inachukuliwa na serikali.

Chadema kiko tayari, kufanya kazi ya kutafuta amani
na wale wanaopenda demokrasia. Chadema haifanyakazi na wanafiki wa amani.
Imetolewa na: Benson Singo Kigaila, Mkurugenzi wa Oganaizesheni ma Mafunzo, Dar es Salaam



No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...